Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mara paap... Yondani,Ajibu ,Manara kibao kimegeuka

98803 Simbayanga+pic Mara paap... Yondani,Ajibu ,Manara kibao kimegeuka

Fri, 13 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sayansi na teknolojia zinavyokua, ndivyo mambo yanavyobadilika, wakati kina Abdallah Kibadeni, Sunday Manara, Zamoyoni Mogella, Edibily Lunyamila wanacheza hakukua na mambo ya kuchukua video, yalitumika magazeti na redio kutangaza kazi zao.

Kwa sasa mambo yamebadilika, sio kama zamani ukikosa kwenda uwanjani utasikia redioni ama kusubiri kusoma magazeti siku ya kesho yake, mashabiki wanaweza kuangalia kupitia runinga, simu ama kuangalia marudio ya video zilizorekodiwa.

Kutokana na mambo kubadilika ndio maana wachezaji wa miaka ya sasa ambao walikuwa tishio kwenye mechi za watani wa jadi wamepwaya na kuonekana ni wakawaida machoni mwa mashabiki ambao kipindi cha nyuma waliwaona kama wafalme.

Ilikuwa ikifika dabi ya watani wa jadi kuna majina yalikuwa yanatamba na mengine yalichukuliwa kama ya kawaida sana mbele ya mashabiki wao. Ila kwa sasa mambo yamebadilika.

Mwanaspoti limefanya utafiti wa baadhi ya mambo yaliojitokeza katika dabi ya msimu huu na kugundua dunia inaenda kasi, wapo wachezaji wanaoendana na kasi na wengine wameshindwa.

IBRAHIM AJIBU -KAPOA

Pia Soma

Advertisement
Jina la Ibrahim Ajibu lilikuwa tamu mbele ya mashabiki, wakati alipohamia Yanga msimu wa 2017/18, Simba ilikuwa inajihofia angeweza kufanya madhara kwenye mechi ya dabi na aliweza kufanya vizuri.

Mambo yamebadilika kwake, msimu huu tangu ajiunge na Simba hajawa na namba ndani ya kikosi cha kwanza, tofauti na matarajio ya mashabiki kuona atafanya maajabu, badala yake benchi linaendelea kumzoea.

Ukiachana na hilo, katika mechi ya watani wa jadi iliyopigwa hivi karibuni, hakuwemo kwenye kikosi, aliishia kuwa mtazamaji, tofauti na jinsi ambavyo jina lake lilivyokuwa tishio msimu ulioisha akiwa na Yanga.

KELVIN YONDAN -KACHEZA DAKIKA TANO

Yule Yondani alikuwa tishio kwa Simba misimu iliopita,sio huyu wa juzi ambaye amepewa dakika tano tu za kucheza mechi ya watani wa jadi.

Taratibu Yondani ni kama ameanza kupoteza thamani mbele ya mashabiki wake, Kocha Luc Eymael ni mara chache kumuanzisha kwenye kikosi chake cha kwanza, jambo ambalo hata mashabiki hawalipigii kelele.

SAID MAKAPU -KAWA SHUJAA GHAFLA

Kama kuna mchezaji aliwachanganya mashabiki kabla ya kuanza mechi ya watani wa jadi ni Said Juma ‘Makapu’, hakuaminiwa mpaka alivyoanza kucheza na kufanya maajabu ndipo akashangiliwa.

Aliwashangaza kwa kiwango alichoonyesha, alicheza kwa utulivu na kuwafanya wakongwe kina John Bocco na Meddie Kagere kushindwa kufurukuta mbele yake, baada ya mechi akaiteka mitandao ya kijamii.

FEI TOTO- JASIRI MBELE YA SIMBA

Tangu ajiunge na Yanga msimu wa 2017/18 kila anapopangwa mechi ya watani wa jadi, anajiamini na kucheza kwa kiwango cha juu, ndivyo alivyofanya juzi timu yake ikiibuka na ushindi wa bao 1-0.

Haogopi kukabiliana na ushindani, usumbufu wake uwanjani ndio umemfanya staa wa Simba, Chama kumchezea rafu kisha kuomba radhi kwenye mitandao ya kijamii.

SAID NDEMLA -KAGEUKA MTAZAMAJI

Licha ya baadhi ya wadau kukiona kipaji kwa Said Ndemla lakini amekuwa akichomeshwa mahindi ndani ya kikosi cha Simba, amekuwa akicheza mara chache sana.

Katika mechi za watani wa jadi amegeuka mtazamaji, mfano mechi ya juzi ambapo kikosi chake kimepigwa bao 1-0 hakuwemo kwenye kikosi kabisa, badala yake alikaa jukwaani.

SHIZA KICHUYA -KAWA WA KAWAIDA

Miaka miwili iliopita, ulikuwa ukitaja mchezaji mwiba kwa Yanga watani walipokuwa wakikutana kwenye mechi zao, jina la Shiza Kichuya lilikuwa tishio kwao, kwa sababu alikuwa akiwafunga kila walipokuwa wakikutana.

Tangu alipokwenda Misri kucheza soka la kulipwa, amekuwa wa kawaida, mechi ya hivi karibuni hakuwa miongoni mwa kikosi kilichocheza.

HASSAN BUMBULI -KATEKA MITANDAO YA KIJAMII

Ni msemaji wa Yanga kwa sasa ni zamu yake kutamba kwenye mitandao ya kijamii kutokana na timu yake kuwashinda watani wao wa jadi bao 1-0.

Kila anachosema kwa sasa kinasikilizwa na kufuatiliwa kwa ukaribu na mashabiki wa Yanga ambao bado wana ile furaha ya kuwafunga Simba bao 1-0.

HAJI MANARA -ANAPOTEZEA

Laiti kama Simba ingeshinda mchezo huo, Haji Manara angekuwa ametawala kwenye mitandao ya kijamii na maneno yake ya shombo dhidi ya Yanga. Hakuuongelea sana mchezo huo ni kama vile hazijui kijeli zinazoelekezwa kweke na timu yake ya Simba.

SHARAF SHIBOBU -ALINUNA

Kiungo wa Simba, Msudan Sharaf Shibobu baada ya mechi kumalizika wakati wenzake wakiingia vyumbani yeye akakaa kwenye korido, huku akiwa amenuna baadaye kocha wake akamuita ndipo akaenda kuungana na wenzake.

Wakati anasajiliwa Simba ndiye aliyekuwa mchezaji tishio kwa timu pinzani kutokana na uwezo aliokuwa akiuonyesha tofauti na sasa ambapo anaonekana wa kawaida.

Chanzo: mwananchi.co.tz