Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapro Ligi Kuu wahamishia soka kitaa

Mwamnyeto Job Kibwana Mapro Ligi Kuu wahamishia soka kitaa

Thu, 29 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hwawapoi. Ndivyo unaweza kusema baada a mastaa wa Ligi Kuu kuhamia kitaa na kuendelea kucheza mechi za soka na timu zao nyingine licha ya kwamba ligi imemalizika na wengine walitakiwa kuwa mapumziko.

Mastaa mbalimbali waliotamba kwenye Ligi Kuu msimu uliomalizika kwa Yanga kuwa bingwa wamekuwa wakijikusanya na kuunda timu tofauti ambazo zinacheza mechi kwa sababu mbalimbali.

Zipo timu zinazocheza mechi hizo za kitaa katika viwanja vya kitaa ili kujifurahisha, kuweka miili sawa na kudumisha umoja na ushirikiano baina ya wahusika lakini zipo pia zinazocheza mechi hizo kama kurudisha kwa jamii.

Achana na ile ya kolabo la nahodha wa timu ya taifa ya Mbwana Samatta na mfalme wa Bongo Fleva, Ally Kiba iliyopigwa Jumanne ya wiki hii pale Uwanja wa Azam Complex lakini kumekuwa na mechi nyingine za mastaa wengine zinazoendelea kitaa.

Kwakuwa Mwanaspoti hatutaki upitwe na tukio lolote la kimichezo, basi kupitia makala haya tunakuletea baadhi ya mechi za mastaa wa Ligi Kuu ambazo zimechezwa na nyingine zinatarajiwa kupigwa zikiwemo za kujifurahisha, kuburudisha, kudumisha umoja na hisani.

Timu Bangala vs Timu Molinga

Hii ilikuwa mechi iliyopigwa Juni 14, mwaka huu uwanja wa Chuo cha Sheria Dar es Salaam ukizihusisha timu Bangala inayomilikiwa na kiungo wa Yanga, Yanick Bangala na Timu Molinga inayemilikiwa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga David Molinga wote raia wa DR Congo.

Mechi hiyo ilikuwa na mvuto wa aina yake huku mastaa kibao wakicheza ambapo Bengala, Benard Morrison, Joyce Lomalisa na Djuma Shaban wote wa Yanga walikuwa timu moja sambamba na Victor Akpan, Nelson Okwa ambao wameachwa na Simba, Yacouba Sogne na Pascal Kitenge wa Mtibwa na Francis Kazadi wa Singida Big Stars walikuwa timu moja.

Katika mechi hiyo, Timu Bangala iliyojaa mastaa wa ligi iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Timu Molinga iliyokuwa na watu kazi wengi wasio na majina makubwa.

Timu Bangala vs Timu Ajibu

Baada ya Timu Bangala kuwafunga timu Molinga, 'mabosi' hao waliungana na kuwa timu moja lakini ikiendelea kuitwa timu Bangala na mechi iliyofuata walicheza na Timu Ajib mchezo uliopigwa uwanja wa chuo cha Sheria, Juni 17 mwaka huu na Timu Ajibu kushinda 2-1.

Timu Ajibu ina mastaa wengi akiwemo Ajib mwenyewe, Saidi Ndemla kutoka Singida Fountain Gate na Edward Songo wa JKT Tanzania, Pius Buswita na Adam Oseja wa Namungo, Gadiel Michael aliyeachwa na Simba na Abdallah Shaibu Ninja wa Yanga.

Kwa upande wa timu Bangala walicheza kina Jesus Moloko, Molinga, Bangala, Djuma, Lomalisa na wengine kibao.

Job vs Kibwana

Hii ni mechi ya hisani inayopigwa wikiendi hii ambapo inaundwa na timu mbili kwa maana ya Timu Dickson Job na Timu Kibwana Shomari wote mabeki wa Yanga, ikienda kwa jina la 'Wape Tabasamu'. Mchezo huo ulipigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro na kujaza mashabiki wengi, ukiwa unahushisha wachezaji wa Ligi Kuu na wale wa Championship.

Kibwana na Job wameuandaa mchezo huo ikiwa ni mara ya pili kufanyika kwa ajili ya kusaidia watu wenye uhitaji.

"Sisi kama familia ya michezo tunaungana na Watanzania wote kusaidia jamii yenye uhitaji na kurejesha tabasamu kwao ikiwa ni msimu wetu wa pili," alisema Kibwana.

Fei Toto vs Makame

Mastaa wa zamani wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto' aliyejiunga na Azam pamoja na Addulaziz Makame 'Bui' aliyehuru kwa sasa nao waliandaa mechi yao ikienda kwa jina la 'Saidia Wazazi' iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mao Zanzibar wikiendi iliyopita.

Miongoni mwa mastaa walioshiriki kwenye mechi hiyo ni kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, Fiston Mayele, beki wa Simba, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr', Novatus Dismas kutoka Ubelgiji, Abdul Seleman 'Sopu' kutoka Azam na Ibrahim Bacca wa Yanga, timu Fei ilishinda kwa penalti 4-2 baada ya sare ya bao 1-1 dakika 90.

Mwamnyeto vs Mauya

Pia huenda wakazi wa Tanga na maeneo ya jirani wakapata burudani ya namna hiyo kutoka kwa nahodha wa Yanga Bakari Mwamnyeto na kiungo wa timu hiyo Zawadi Mauya ikienda kwa jina la 'Mwamnyeto Foundation'.

Wawili hao wako kwenye hatua za mwisho kupiga mechi hiyo inayotajariwa kuchezwa wikiendi Ijayo Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Mastaa kibao wa Ligi Kuu na Championship wanatarajia kushiriki katika mchezo huo ambao lengo lake ni kutoa burudani na kusaidia watu wenye uhitaji, hapa napo wanatajwa mastaa kadhaa kuwa watashiriki wakiwemo wale wa Yanga na Simba.

Sambamba na hao, wapo mastaa wengine kibao ambao baada ya msimu kumalizika walirejea nyumbani kwao na mara kadhaa wamekuwa wakipasha na timu za kitaa kwao na kucheza baadhi ya mechi.

Huo umekuwa utaratibu wa wachezaji wengi na umekuwa ukitoa fursa kwa watu wengi zaidi kujumuika, kufahamiana, kujifuna na kufaidika kwa namna moja ama nyingine kupitia kwa mastaa hao.

Chanzo: Mwanaspoti