Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapenzi ya Mbappe na ulevi wa matajiri wa PSG

Skysports Al Khelaifi Mbappe 5781402 Mapenzi ya Mbappe na ulevi wa matajiri wa PSG

Sat, 9 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna msemo unasema ‘heri wali maharage kwenye amani kuliko kula pilau vitani’. Inawezekana ukawa na tafsiri nyingi sana lakini moja kati ya hizo ni heri upate hata kidogo lakini uwe na furaha kuliko kupata kizuri na kingi halafu ukawa huna furaha.

Waarabu ni miongoni mwa binaadamu waliojaaliwa sana utajiri, haijalishi iwe ni fedha ama rasilimali lakini waarabu kote huko utawakuta wanamiliki vitu vingi vya thamani.

Ukienda kwenye nchi zao hata hapa Afrika basi utastaajabu jinsi zilivyokuwa na miundombinu ya kisasa na mandhari mazuri, yote hiyo ni kuakisi utajiri wao.

Kuanzia miaka ya 2010, waliamua kuingia kwenye soko la dunia la mpira wa miguu, walinunua timu nyingi ikiwemo Manchester City, walitumia pesa nyingi kuhakikisha timu hizo zinafanya vizuri.

Moja wapo kati ya timu hizo ni Paris Saint-Germain waliyoinunua mwaka 2011. Katika vipindi tofauti tofauti PSG imekuwa ni timu shindani ikisajili baadhi ya mastaa wakubwa kwenye soka.

Walifanikiwa kwa mtu kama Ronaldinho, David Beckham na wengineo.

Waarabu wanaoimiliki hii timu wanatoka Qatar, wao haja yao ni kuona majina makubwa yanachezea timu yao, ndio maana walidiriki hata kumsajili Lionel Messi akiwa anaenda ukingoni, Sergio Ramos, Kayle Navas, wote hawa walionekana kama wameshamalizana na soka la kiushindani na hawana njaa ya mafanikio.

Lakini Nasser Al Khelafi na bodi yake waliidhinisha bajeti ya kuwasajili.

Hata wakati wanamsajili Beckham naye tayari alikuwa anaenda kwenye nyakati za mwisho za maisha yake ya soka.

Wao hawakujali kikubwa zaidi kwao ni kuona mchezaji mwenye jina kubwa kama yeye akikanyaga ardhi ya Parc de Princess akiwa na jezi yao.

Ndio maana hawakujali kutoa zaidi ya Euro 150 milioni kwa ajili ya kumsajili Neymar kutoka Barcelona mwaka. Kwa sababu walihitaji kuona jina kubwa la mchezaji mkubwa kama yeye linaichezea timu yao.

Huo ndio ulevi wao, wanahisi furaha sana moyoni wakiona kuna kundi la wachezaji mastaa wanaotajwa duniani likiwa kwenye kiwanja chao cha mazoezi cha Camp des Loges wakishikana na kutaniana.Hawajali kuhusu pesa watakazotumia, waarabu hawa wanainjoi matukio kama hayo.

Kwa muda sasa walikuwa wanamiliki mmoja kati ya wachezaji bora duniani. Kylian Mbappe, kabla ya kusaini mkataba mpya ilibaki kidogo aondoke atue Real Madrid lakini PSG ikambakisha na kumpa pesa nyingi.

Hapa ndio kuna utofauti wa mitazamo, Mbappe hana furaha ya kuendelea kuichezea PSG kwa sababu haoni kama atashinda mataji makubwa ama ataonekana kama mchezaji bora duniani akiwa hapo. Ndoto na mawazo yake yote yapo Madrid.

Licha ya PSG kuwa na uwezo wa kumpa pesa nyingi zaidi ya zile ambazo Madrid imemuahidi, Mbappe haonekani kujali sana kuhusu hilo yeye wali na maharage kwenye amani ndio chaguo lake kuliko Pilau sehemu ambayo hana furaha.

Alipokuwa anasaini mkataba mpya mwaka 2022, PSG ilipambana sana kuhakikisha hilo linafanikiwa, kuna wakati hadi serikali ya Ufaransa kupitia kwa Emmanuel Marcon iliingilia kati na staa huyo akaombwa aendelee kuichezea timu hiyo.

Lakini sasa inaonekana kufikia ukomo. Mbaya zaidi kwa PSG ni kwamba mbali ya Mbappe kuwa ni jina kubwa kwenye timu yao, pia amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu.

Katika mechi nne zilizopita Mbappe amecheza tatu tu ambapo mbili alianzia benchi na moja alicheza kipindi cha kwanza kisha akatolewa kipindi chapili kiliporejea. Mechi mbili hizo ni kuanzia kwa Rennes na Monaco ambazo zote PSG haijapata matokeo mazuri.

Kuna muda wamejaribu kujiaminisha wanaweza kuziba pengo lake lakini inaonekana kuwa ngumu jambo linalowachanganya zaidi.

Rais wa timu hiyo amedaiwa kulazimisha hadi dakika ya mwisho ili Mbappe akubali kuendelea kuichezea timu yao walau kwa msimu mmoja zaidi lakini amekataa na taarifa zinadai tayari mama yake amaeshaanza kutafuta nyumba huko Jijini Madrid.

Msimu huu staa huyu wa kimataifa wa Ufaransa amefunga mabao 21 kwenye mechi 22 za Ligue 1. Ndio mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye kikosi cha PSG na Ligi Kuu Ufaransa kwa ujumla.

Mbappe anawahukumu mabosi wa PSG kwa kuwanyima starehe yao, ndio maana wanahusishwa kuwa kwneye mpango wa kumsajili Victor Osimhen ambaye ni habari ya mjini kwa sasa. Ndio, wanataka kumsajili ili akazibe pengo la Mbappe pia ni kwa sababu hawawezi kuvumilia kuishi bila yakuwa na jina kubwa linalosumbua barani Ulaya hata moja kwenye timu yao.

Ukiondoa matamanio yao, lakini Mbappe na jina lolote kubwa linalotua kwenye kikosi chao huwa na msaada mkubwa sana kiuchumi.

Mastaa kama Lionel Messi waliipatia timu hiyo pesa nyingi kutoka kwenye mauzo ya jezi ndani ya muda mfupi, pia makampuni mengi yakatamani kutangaza na PSG ikiaminika watu wengi watakuwa wanaifuatilia kwa sababu yake.

Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa Mbappe, mbali ya kupoteza nyezo muhimu kwenye timu lakini pia wanaenda kupoteza walau asilimia 10 ya pesa ambazo walikuwa wakizipata wakati staa huyu anaichezea timu yao.

Vile vile, ukiondoka ulevi wa mabosi wa PSG na hasara watakazopata, pia kuondoka kwa Mbappe kunakwenda kuathiri pia mamlaka za soka nchini Ufaransa kwa sababu Mbappe ni taswira ya Ligue 1 na mpira wa Ufaransa kwasasa, kitendo cha kuondoka kwake pia kinakwenda kuathiri pande nyingi kwenye soka hilo, kuna baadhi ya makampuni yalikuwa yamewekeza ama kutamani kuwekeza kwa sababu ya uwepo wake.

Chanzo: Mwanaspoti