Mikoba ya kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula kocha wa timu hiyo Roberto Oliveira ataamua ampe Beno Kakolanya ama Ally Salim, robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Wanamsimbazi wakicheza dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.
Ipo hivil; Manula hatakuwepo kabisa kwenye mpango wa Simba kwenye mechi zilizosalia msimu huu, kulingana na tatizo lake la nyonga, benchi la ufundi halina namna nyingine zaidi ya kufanya maamuzi nani atadaka CAF kati Kakolanya na Salim.
Salim alicheza vizuri dhidi ya Yanga, Simba ikashinda mabao 2-0 lakini hajawahi kucheza mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu ngumu kama Wydad huku Kakolanya akimzidi kwa uzoefu ingawa kuna tetesi kwamba amegoma kusaini mkataba mpya akihesabu siku kutua Singida Big Stars.
Habari za ndani zinasema "Ni ngumu kwa Manula kumaliza msimu huu kwani ana tatizo la nyonga ndio maana hadi sasa hajaanza mazoezi na timu. Manula tangu alipoumia kwenye mechi dhidi ya Ihefu FC hajajiunga na wenzake kwaajili ya mazoezi mchezaji ambaye ameanza mazoezi kwa waliokuwa majeruhi ni Henock Inonga ambaye alicheza mechi Jumapili na Sadio Kanoute ambaye maendeleo yake ni mazuri."
"Tuna mchezo Jumapili ni muhimu kwetu lakini ni asilimia kubwa kukosa huduma ya Manula tena hivyo mpango wa kocha kumtumia Beno Kakolanya au Ally Salimu ambaye alionyesha kiqwango kizuri dhidi ya watani zetu Yanga." kilisema chanzo cha ndani ya Simba ingawa imekuwa ikifanywa siri kubwa.
Manula amekosekana kwenye mechi mbili za ligi za hivi karibuni dhidi ya Ihefu FC na watani zao Yanga ambazo zote timu yake imeibuka na ushindi na langoni akikaa Ally Salimu kipa namba tatu wa timu hiyo.
REKODI YA MANULA Manula amekuwa na misimu minne bora akichukua tuzo ya kipa bora wa msimu mara zote, mara tatu akiwa na Simba na mara moja akiwa kwenye kikosi cha Azam FC.
Manula pia alikuwa sehemu ya mafanikio kwenye kikosi cha Simba baada ya kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pia tangu ajiunge Simba 2017 amechukua ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo huku akiwa ndiye kipa namba moja kwenye kikosi hicho na kujenga imani kubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo.
Manula alikuwa katika kikosi cha Taifa Stars kilichocheza fainali za Mataifa Afrika 2019 nchini Misri akicheza mechi mbili na timu ya Tanzania ilitolewa katika hatua ya makundi.
Manula alikuwa ni miongoni mwa wachezaji walioipa Simba mafanikio ya kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018/19, msimu wa 2019/20 waliishia raundi ya awali wakitolewa na UD Songo ile yaLuis Miquissone kabla ya msimu wa 2020/21 kurejea makali yao na kufika tena robo fainali.