Daktari wa Simba, Edwin Kagabo ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya mlinda lango Aishi Manula anayetarajiwa kufanyiwa vipimo vya mwisho na pengine akaruhusiwa kujiunga na wenzake katika mazoezi ya timu.
Manula amekuwa nje tangu mwishoni mwa mwezi wa tano, baada ya kufanyiwa upasuaji Afrika Kusini, amefanya program maalum za kumuimarisha na sasa yuko tayari kurejea katika majukumu yake
"Alipewa mazoezi tiba na kuyafanya vizuri, ameimarika kwa haraka sana na baada ya vipimo vya mwisho anaweza kujiunga na wenzake," alisema Kagabo.
Manula anaweza kuwa sehemu ya kikosi cha Simba katika mchezo wa kwanza wa robo fainali African Super League dhidi ya Al Ahly utakaopigwa Oktoba 20, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Hii ni habari njema kwa Simba ambayo bado unaweza kusema haijapata utulivu eneo la golikipa tangu alipoumia licha ya Ally Salim kuendelea kuimarika na kufanya vizuri pamoja na ujio wa Ayoub Lakred.