Kipa wa Simba na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Aishi Manula amesema alikosa matumaini ya kutwaa tuzo Mwanasoka Bora wa 2022 katika tuzo zilizotolewa na Baraza la Michezo la Tiafa (BMT) kutokana na ubora wa washindani wake.
Katika kipengele hicho, Manula alikuwa anachuana na mabeki wa Simba, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Akizungumza na Mwanaspoti, kipa huyo alisema hakuona dalili ya kutoboa katika tuzo hizo akizingatia kwamba alijiona kutokuwa na nafasi kubwa ya ushindi.
Alisema Kapombe na Tshabalala ni mabeki wazuri wa pembeni ambao wanavutia namna wanavyopambana wanapokuwa uwanjani, hivyo aliwapa nafasi kubwa ya kushinda tuzo hiyo.
“Tuzo ya BMT ni kubwa kwangu na ina maana pia. Kama tunavyofahamu kuwa BMT ndio baba wa michezo nchini. Nashukuru kutambua mchango wangu katika soka la Tanzania na timu ya taifa. Ni jambo kubwa mno kwenye safari yangu ya soka,” alisema.
Pia alieleza alivyojipanga kuipambania Stars ambayo inatarajia kukutana na Uganda kwenye mechi ya kwanza ya kuwania kuzufu Afcon ambapo timu hizo zitacheza Machi 24, mwaka huu.
“Mara zote kama Mtanzania nimekuwa nikipigania nchi yangu kwenye soka kwa jasho na damu ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliojiwekea,” alisema.
“Japo mara kadhaa tumekuwa tukikwama, ila sijawahi kuchoka kuipigania nchi yangu. Pia nawashukuru Watanzania kwa kuendelea kunipa nguvu ya kupambana.”