Kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' kimeanza vibaya mechi za kirafiki 'Fifa series' baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Bulgaria.
Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Dalgha Maedakan jijini Baku nchini Azerbaijan hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika hakuna timu iliyopata bao, huku timu zote zikionekana kumiliki mpira zaidi eneo la katikati ya uwanja.
Stars itajilaumu yenyewe kupoteza nafasi bora ya kutangulia kufunga dakika ya 28 kupitia nafasi ya wazi ya winga Kibu Denis ambaye shuti lake akitokea kuwakimbiza umbali mrefu mabeki wa Bulgaria limegonga mwamba na kumkuta tena Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye amepaisha kwa shuti.
Kipa Aishi Manula dakika ya 30 alilazimika kutolewa baada ya kupata maumivu na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na Kwesi Kawawa aliyekwenda kumalizia dakika 60 za mchezo huo.
Bao lililoamua mchezo huo lilipatikana dakika ya 51 kwa njia ya mpira wa adhabu ndogo likifungwa na kiungo na nahodha wa Bulgaria, Kiril Despodov limetosha kuamua mshindi.
Haikuwa siku nzuri kwa Fei Toto kwenye mchezo huo baada ya kupoteza nafasi nyingine ya wazi katika dakika ya 72 akiunasa mpira uliotokana na kujichanganya kwa mabeki wa Bulgaria, lakini shuti lake akiwa uso kwa usok na kipa wa wapinzani akapaisha.
Mabadiliko ya kocha Hemed Morocco kipindi cha pili kuwatoa Maino Danilo, Haji Mnoga, Tarryn Allakakhia na Kibu na nafasi zao kuchukuliwa na Clement Mzize, Lusajo Mwaikenda, Abdul Selemani 'Sopu', Charles M'mombwa yaliibadilisha Stars na kuanza kuishambulia kwa nguvu Bulgaria lakini ikashindwa kutumia nafasi kadhaa ilizopata.
Matokeo hayoa yanaifanya Stars kubakiza mchezo mmoja wa mwisho dhidi ya Mongolia utakaopigwa leo Machi 25 ambao utakamilisha ratiba ya mechi za kirafiki.