Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manula anaenda kumaliza tatizo Azam FC

Manula Arudi Langoni.jpeg Aishi Manula

Wed, 10 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Inaelezwa msimu uliopita ilibakia kidogo tu, kipa Aishi Manula arudi Azam FC.

Dili hilo lilikuwa hivi, Simba ilikuwa inamtaka kiungo Sospeter Bajana. Azam FC haikuwa na shida, ikataka irudishiwe Manula. Dili lilikwama.

Unajua nini kilitibua dili hilo?

Awali mabosi wa Azam hawakuwa na shida ya kumruhusu Bajana kwenda Simba, kwa sababu waliamini Kenneth Muguna atabaki kwenye kikosi chao. Ghafla mambo yakageuka, Muguna aliwekwa kwenye orodha ya wachezaji wanaopaswa kuondoka ioli kupisha nyota wapya waje.

Kutokana na hilo, viongozi wa Azam walirudi kwa wenzao wa Simba kuwaambia dili la Bajana limekufa, hivyo nao wakakutana na majibu ya mabosi wa Simba kwamba, dili la Manula pia halitakuwapo tena kwa sababu, Beno Kakolanya ameondoka kwenda Singida Fountain Gate.

Hivyo dili hilo likafika hapo.

Azam imekuwa ikimtaka Manula arudi kikosini, kwa sababu tangu alipoondoka Agosti 2017, timu hiyo bado haijampata mbadala wake. Azam imekuwa ikisajili na kuacha makipa karibu 10 sasa ili kuziba pengo la kipa huyo aliyekuzwa katika Akademia ya klabu hiyo akitokea Morogoro kabla ya kuanza kuitumikia rasmi Julai, 2012.

KWANINI SASA

Tangu alipoondoka Manula kutua Simba sambamba na nyota wengine watatu akiwamo kiungo Erasto Nyoni, beki Shomary Kapombe na mshambuliaji, John Bocco 'Adebayor' Azam imekuwa ikipokea makipa wa kila aina ambao hata hivyo wameshindwa kufanya maajabu.

Alikuja Mathias Kigonya kutoka Uganda akachemsha, amepita Razack Abalora kutoka Ghana naye alikuwa maji kupwa maji kujaa kutokana na kukosa utulivu.

Hadi David Mapigano Kisu naye amepita Azam. Usimsahau kapita Benedict Haule, Wilbol Maseke,

Ahmed Ali Suleiman 'Salula'.

Azam ikaamua kumleta kipa kutoka Ulaya, Ali Ahamada aliyekuwa Ufaransa. Lakini hakuwa na maajabu kivile, hivyo wakamuongezea nguvu kwa kumshusha Mghana Iddrisu Abdulai.

Makipa hao kwa sasa wote ni majeruhi na tumaini la Azam lipo mikononi mwa Zuberi Foba aliyeongezewa nguvu kwa kuletewa kipa kutoka El Merrikh ya Sudan, Mohammed Mustafa akisajiliwa kwa mkopo.

Kitendo cha makipa wawili tegemeo na wa kigeni, Ahamada na Addrisu kuwa majeruhi kunailazimisha Azam sasa kumhitaji zaidi Manula kuliko wakati mwingine. Kingine ni kwamba zipo taarifa za chini chini kwamba makipa hao wawili wote wanaweza kupigwa chini kutokana na kuwa na gharama kubwa.

Hivyo, Manula akiwa kipa mzawa na mtoto wa nyumbani, ana uwezo mkubwa wa kuziba nafasi zao kwa ufanisi na kuibeba Azam kuliko hata makipa hao wa kigeni ambao walikuwa wakifanya makosa yaliychangia Azam kushindwa kufanikisha ndoto zao kwenye mechi kadhaa walizodaka.

Ukiachana na hilo la kutaka kutemwa kwa kina Ahamada, pia Azam hadi sasa haina uhakika na kipa Mustafa ambaye hajaanza kucheza tangu aliposajiliwa hivi karibuni, lakini Foba amekuwa akifanya makosa yaliyoigharimu timu hiyo kwenye mechi kadhaa zilizopita.

Huwezi kumlaumu sana Foba, kwani hana uzoefu wa kutosha, lakini anafanya makosa ya kawaida sana kwa kipa anayeidakia timu kubwa kama Azam. Ukiyaangalia mabao mawili iliyofungwa Azam katika mechi ya Nago ya Jamii dhidi ya Yanga jijini Tanga, utaelewa kwanini maana ya hili.

Angalia bao alilofungwa juzi kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Mapinduzi 2024 dhidi ya Singida ndio utajua Manula ni lulu na anahitajika pale Azam kwa sasa kuliko wakati mwingine wowote.

MANULA MWENYEWE

Hata Manula mwenyewe naye anaihitaji Azam kwa sasa kuliko kipindi kingine chochote kutokana na kuishi maisha ya presha tangu alipotunguliwa mabao matano kwenye mechi ya Kariakoo Derby iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana.

Manula alikuwa hajawahi kufungwa idadi ya mabao hayo dhidi ya Yanga na hata kwenye mechi za Ligi Kuu Bara tangu alipoanza kucheza ligi hiyo.

Bahati mbaya alirejea uwanjani akitoka kuwa majeruhi wa muda mrefu na kukutana na dhahama hiyo ya kutunguliwa idadi hiyo wakati Simba ikifa kwa mabao 5-1 mbele ya Yanga.

Tangu alipofungwa mabao hayo, ile heshima na hadhi aliyokuwa nayo Msimbazi ni kama imepungua. Amekuwa akiandamwa na mashabiki mtandaoni, hali ambayo inamfanya aishi maisha ya presha kuliko kipindi chote cha misimu sita iliyopita aliyokuwa akiidakia Simba.

Hivyo kwa kutambua kuwa Azam sio timu ya presha, huenda hata yeye angependa kurejea ule usemi wa 'ng'ombe avunjikapo mguu malishoni, hurejea zizi' kwa kutamani arejee nyumbani ili apumue.

Huenda Manula anaamini akirejea Azam atarejesha ule uimara wake langoni kwani hatacheza tena kwa presha kubwa kama sasa. Na kwa vile Azam inamuamini na kumtumainia ni wazi atapata nafasi ya kucheza kama kipa namba moja na kurejesha hadhi ya Tanzania One ambayo kwa sasa ipo kama haipo tangu alipokuwa nje ya uwanja baada ya kuumia kwenye mechi ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) iliyopigwa Aprili mwaka jana.

Lakini, Manula anaijua miiko na tamaduni za Azam kwa sababu kwa misimu mitano aliyoichezea kabla ya kujiunga na Simba mwaka 2017 aliishi na kuitumikia miiko na tamaduni hizo kwa ufanisi.

Kadhalika kama ni ishu ya maokoto, Azam sio jambo la kuwa na shaka nalo kwa kuwa ni klabu yenye uwezo mkubwa na pengine itampa kadri atakavyo pengine kuliko alizokuwa akipewa Simba. Kuna kitu kingine hapa duniani kama kupata maokoto?

HATA SIMBA NAKO

Kadhalika Simba tayari imeonekana kupoteza imani kwa Manula kwa sasa, kulinganisha na misimu ya nyuma na bahati nzuri, Ally Salim anaonekana kuwa mrithi wake langoni, mbali na uwepo wa kipa kutoka Morocco, Ayoub Lakred.

Hii ina maana hata kama Manula ataamua kuondoka Msimbazi sasa, mabosi hawatakuwa na presha kubwa kwa vile makipa waliosalia wameonyesha wanaweza kuvaa viatu vya kipa huyo. Kumbuka mbali na Salim na Ayoub, klabu ya Simba pia ina Hussein Abel ambaye ni mmoja wa makipa hodari, hata kama hapewi nafasi kubwa kikosini.

Hivyo hata kama Manula ataondoka Msimbazi, hakutakuwa na pengo kubwa kivile, lakini kipa huyo ataenda kutatua tatizo linaloisumbua Azam kwa muda mrefu katika milingoti mitatu ya matajiri hao.

Akizungumzia ishu ya Manula kuhusu mpango huo wa kurudi Azam FC, gwiji wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni alisema kama nyota huyo ataondoka sio jambo la kushangaza sana kwani katika maisha ya kila siku mtu huangalia zaidi maslahi na sio vinginevyo.

"Kwanza atakuwa anarudi alikotoka na isitoshe ni kipa mzuri ambaye naamini atawasaidia sana, kwangu akiondoka Simba hawapaswi kujutia isipokuwa wanatakiwa kumpa baraka zote ili akapate kile ambacho alikuwa anakikosa akiwa kwao," alisema Kibadeni, mchezaji pekee anayeshikilia rekodi ya kufunga hat-trick kwenye mechi ya Kariakoo Derby, iliyopigwa Julai 19, 1977 wakati Yanga ilichapwa 6-0.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: