Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manula aivuruga Simba

Manula X Cadena Manula na Kocha Cadena

Sat, 27 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha wa makipa wa Simba, Dani Cadena amekiri kwamba kiwango bora cha Aishi Manula kwenye fainali za mataifa ya Afrika (Afcon), kinamuweka katika wakati mgumu kuamua kipa wa kuanza kikosini pindi ligi na mashindano mengine yakirejea.

Lakini, mbali na kukiri kuwa kichwa kinamuuma katika kuamua nani apate nafasi ya kucheza kutokana na ubora wa makipa wengine Ayoub Lakred, Ally Salim na Hussein Abel,  Cadena ametamba kuwa ushindani unalihakikishia usalama zaidi lango la timu hiyo katika mechi za mashindano.

Licha ya kufungwa mabao manne katika mechi tatu alizocheza kwenye Afcon kabla ya Stars kutolewa katika hatua ya makundi, Manula alionekana kurejea kwenye ubora wake ikiwa ni siku chache baada ya kutoka kuuguza majeraha ya muda mrefu aliyoyapata Aprili 7, mwaka jana katika mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Ihefu SC ambayo Simba ilishinda kwa mabao 5-0 katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Katika Afcon, Manula ni miongoni mwa makipa waliofanya vizuri katika hatua ya makundi ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na mtandao wa fotmob.com kipa huyo ameshika nafasi ya nne katika chati ya makipa waliookoa hatari nyingi akifanya hivyo mara 10 huku kinara akiwa ni Babacar Niasse wa Mauritania ambaye aliokoa hatari 12.

Cadena alisema anafurahishwa na ubora aliouonyesha Manula kwenye Afcon na sasa hiyo itakuwa chachu kwa makipa wengine wa Simba ndani ya klabu hiyo.

“Manula amecheza vizuri, nimefurahi amerejesha utimamu wake wa mwili na hali ya kujiamini sasa rasmi makipa wetu wote wapo tayari kwa mechi,” alisema Cadena.

Kocha huyo aliongeza: “Ni jambo jema ukiwa na makipa zaidi ya watatu na wote wakawa kwenye ubora wao, sasa tuna Manula, Ayoub (Lakred), Ally (Salim), Abel (Hussein) na Feruz (Teru), wote ni wazuri wanachotakiwa kufanya ni kuonyesha ubora na kwakuwa tunashiriki michuano mingi basi ni faraja kwetu na kila mmoja atapata nafasi kutokana na aina ya mechi.”

Tangu Manula amepona majeraha amecheza mechi nne za mashindano na akianza dhidi ya Yanga na kuruhusu mabao 5-1, kisha mechi za Afcon alioanza kwa kuruhusu mabao 3-0 dhidi ya Morocco, bao moja kwenye sare ya 1-1 mbele ya Zambia na kutoa hati safi ‘Cleansheet’ dhidi ya DR Congo mechi iliyomalizika kwa Suluhu.

Mchezaji wa zamani wa Taifa Stars, Juma Pondamali ‘Mensah’ alisema kurejea kwa Manula kutaongeza uimara langoni kwa Simba na kwa makipa wenzake.

“Sio tu kuimarisha lango la Simba, pia itakuwa chachu kwa makipa wengine wa Simba kuwa bora zaidi kwani watatakiwa kuonyesha ushindani mkubwa ili kupata nafasi.

“Lakini pia Manula kwa sasa ni miongoni mwa makipa wazoefu zaidi kwa hawa ambao bado wanacheza hivyo uwepo wake kuna vitu makipa wengine watajifunza kutoka kwake,” alisema Pondamali.

Tangu Aishi aumie, Sinba imekuwa ikiwapanga makipa Ayoub na Ally Salim kwa kupishana ambapo katika mechi za kimataifa amekuwa akicheza Lakred mara kwa mara huku zile za mashindano ya ndani akiwa anacheza Salim.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live