Wakati Simba inatarajia kuikaribisha Mtibwa Sugar katika mechi yake ya Ligi Kuu Tanzania Bara, nyota wake, Aishi Manula na Kibu Denis, wanatajwa kuwindwa na Azam FC ambayo imedhamiria kujiimarisha kwa ajili ya kufanya vizuri katika msimu ujao.
Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zinasema Azam inadaiwa kutenga dau la Sh. milioni 300 na kumpa mkataba wa miaka miwili Kibu, ikipanga kumlipa Sh. milioni 150 kwa mwaka.
Chanzo chetu kilisema matajiri hao wa Chamazi pia wameweka dau nono la kuhakikisha Manula anarejea katika timu yake ya zamani kwa sababu wanaamini nyota huyo mwenye uzoefu atawasaidia kufikia malengo katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao pamoja na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Chanzo hicho kilisema Azam ilipiga hodi Msimbazi baada ya kubaini mkataba wa Kibu umebakiza miezi sita sawa na Manula ambaye kwa sasa ni majeruhi.
"Ni kweli tunahitaji kuimarisha timu yetu na kulingana na mahitaji tuliyonayo ni pamoja na kuimarisha safu ya ushambuliaji na eneo la kipa, na hapo wanatajwa Kibu na Manula. Ofa zao zipo mezani na mambo yakienda vizuri msimu ujao watakuwa mali ya yetu,” kilisema chanzo chetu.
Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat', alisema wako katika mchakato wa kuboresha timu yao katika kila eneo lenye uhitaji.
Popat alisema wanahitaji kufikia malengo na watafika huko kwa kuhakikisha wanasajili wachezaji wenye ubora na uzoefu.
Alisema baada ya kufanikiwa kumnasa nyota, Frank Tiesse, kutoka katika Klabu ya Stade Malien ya Mali, sasa wako katika mchakato wa kukamilisha usajili wa nyota wengine wawili wazawa.
"Ni kweli sasa akili na nguvu zetu ni katika kujiimarisha, kwa sasa tunataka kukamilisha mchakato wa wachezaji wawili ambao ni raia wa hapa Tanzania. Ni wachezaji ambao watakiongezea nguvu kikosi chetu," Popat alisema.
Kuelekea mechi dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda, amesema hii ni ligi na hawawezi kuwajadili wapinzani wao na wataingia kwa tahadhari katika mechi hiyo.
Mgunda alisema licha ya kutokuwa na matokeo mazuri, Mtibwa Sugar ni timu ngumu na wamejiandaa vyema kuwakabili.
"Tutamkosa Chama (Clatous), katika mchezo wa kesho (leo) kutokana na adhabu aliyoipata, lakini Simba imefanya usajili wa wachezaji wengi na watapata nafasi ya kucheza na kuonyesha kitu kizuri. Vijana wapo vizuri na wanajua uzito wa mechi hii na umuhimu wake, wachezaji wapo tayari kwa mchezo kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwa kuvuna pointi tatu muhimu,”alisema Mgunda.
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, alisema mechi hiyo itakuwa ya ushindani kwa sababu wanakutana na Simba ambayo imetoka kugawana pointi na Namungo na leo wanahitaji kupata matokeo chanya.
Katwila alisema wamefanyia kazi na kusahihisha mapungufu yao na sasa wanaenda kukutana na wapinzani kwa tahadhari kubwa.
“Unapochsza na Simba haijalishi wanakosa wachezaji gani, hata sisi tunakosa baadhi ya wachezaji lakini tumejipanga, tuna presha ya kutafuta matokeo mazuri kama ilivyo kwa wapinzani wetu,” alisema Katwila.
Katika hatua nyingine Azam inashuka dimbani kuikaribisha Namungo FC katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA itakayochezwa leo.
“Tutaona namna gani ya mabadiliko na kuingia vipi katika mchezo huo ili kutafuta ushindi na kwenda kucheza nusu fainali, Namungo ni timu ngumu kucheza nao, tunatakiwa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu kwa ajili ya kupambania kombe hili,” alisema, Kocha Msaidizi wa Azam, Bruno Ferry.