Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manula: Huyu Milton ni balaa zito!

Manula Pic Data Manula: Huyu Milton ni balaa zito!

Wed, 24 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KIPA wa Simba na Taifa Stars, Aishi Manula ni miongoni makipa ambao wanaaminiwa kwa kiasi kikubwa kukaa langoni kwa miaka ya hivi karibuni ukiachana na kipa mkongwe Juma Kaseja ‘Tanzania One’.

Tanzania One ni jina ambalo limekuwa likitumiwa na makipa wanaofanya vizuri ambapo alikuwepo Idd Pazi na Mohamed Mwameja ambao waliitwa jina hilo kwa nyakati tofauti ingawa hivi sasa kuna baadhi ya wati wanamfananisha Manula na makipa waliomtangulia na kufanya vizuri.

Manula ambaye alianzia kucheza soka lake Azam FC kwenye timu ya vijana hadi kuwa tegemeo katika kikosi cha wakubwa hadi Simba walipomsajili msimu wa 2017/18.

Katika kuonyesha kuwa Manula ni bora kukaa langoni ametwaa tuzo ya kipa bora wa msimu mara nne mfululizo huku msimu wa 2019/20, hakukuwa na tuzo pengine nayo angeibeba kutokana na ubora wake.

Manula amekuwa tegemeo kikosi cha kwanza cha Simba licha ya ubora wa Benno Kakolanya pamoja na Ally Salim lakini pia hata Taifa Stars licha ya ubora wa baadhi ya makipa waliokuwa ndani na nje ya Tanzania.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Manula alifunguka baadhi ya mambo kwenye maisha yake ya soka.

“Pengine kama nisingekuwa katika uwezo bora kama ambao wao wanahitaji labda nisingekuwa nakutana na lawama za hapa na pale,” anasema Manula ambaye ni moja wa makipa wenye uwezo wa kucheza mikwaju ya penati.

UMOJA NA WENZAKE

Manula anasema miongoni mwa silaha ambayo inaweza kuwa faida kwenye eneo lolote na ukafanikiwa kuwa na upendo, ushikamano na imani kwa wote ambao mnashirikiana katika kutimiza jukumu husika.

“Inawezekana watu hawafahamu ndani ya kikosi chetu tukianza na makipa tunapendana tena zaidi ya sana na huwa tunatenga muda wa kuelekezana wenyewe mahala ambapo mmoja wetu ameonyesha mapungufu.

Ndio maana utaona muda wote makipa huwa tunashirikiana na kuhamasishana ili yule ambaye anacheza afanye vizuri kwani ndio faida kwa upande wetu, lakini si kwetu bali timu nzima mpaka benchi la ufundi,” anasema na kuongeza

“Tunaishi kama watoto wa familia moja ambavyo tunapendana na kuishi bila tatizo lolote ingawa muda mwingine kuna changamoto za kibinadamu,” anasema Manula.

MILTON AMBEBA

Kiwango cha wastani kilichoonyeshwa katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prison na Ruvu Shooting, kiliwakwaza mabosi wa timu hiyo ambao walifikia maamuzi ya kuvunja benchi la ufundi.

Maamuzi ambayo waliamua kuachana na aliyekuwa kocha wa makipa, Muharami Mohammed ‘Shilton’ aliyeondolewa mwishoni mwa mwaka jana nafasi yake kuchukua, Mbrazil Nienov Milton.

Milton Nienov alitambulishwa Januari 23 mwaka huu amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuboresha viwango vya makipa wa timu hiyo.

Moja ya kazi ambayo imeonekana kuzaa matunda kwa Mbrazili huyo ni kuhakikisha Manula kutokufungwa mabao ya krosi na mashuti ya mbali ya mara kwa mara kama ilivyokuwa kabla hajafika.

Milton anasema amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanya kazi hiyo si kwa Manula bali kwa makipa wake wengine wote ambao kila siku wameonesha kuwa na uelewa mkubwa wa kile ambacho wanakitoa.

Manula anasema lazima mabadiliko ya kocha yanapofanyika kuna mambo ya kiufundi ambayo yanachukuliwa kwa yule aliyetoka na kumuonyesha aliyekuwepo wakati huo.

“Naheshimu makocha wangu wote ambao nimewahi kufanya nao kazi katika maeneo tofauti kwani wao ndio wamechangia ubora ambao ninao wakati huu.

“Kuna mambo mengi ambayo tunafundishwa na Milton na yanakwenda kujitokeza kwenye mechi na tunakuwa na mabadiliko katika kuokoa mashambulizi ya timu pinzani,” anasema Manula.

MAKOSA YAKE

Wakati huu inaelezwa Manula kuna baadhi ya makosa yake amekuwa akiyafanyia kazi na kutokuruhusu mabao ya namna hiyo kwenye mechi tofauti.

Miongoni mwa makosa ambayo amekuwa akiyafanya na kuruhusu mabao, kufungwa mabao ambayo yanatokana na mashuti ya mbali pamoja na kushindwa kucheza mipira ya krosi.

“Unajua huwa najisikia vibaya na kuumia kuona kuna jambo ambalo ni changamoto na naonekana nashindwa kulifanyia kazi ili kulimaliza na si katika mpira bali hata maisha ya kawaida,”



“Hivyo basi si kama nimebadilisha mazoezi bali ni yale yale ambayo nimekuwa nikifanya nikiwa na timu pamoja na muda wangu binafsi ili kumaliza shida ambazo zimekuwa zikinisumbua.

“Kwenye ratiba yangu ya mazoezi nashukuru kuna mabadiliko ambayo hata mwenyewe nayaona na ili kuwa bora zaidi mbali ya yale ambayo napokea kutoka kwa makocha wangu nitaongeza ya binafsi,” anasema .

MAISHA YA SIMBA

“Hakuna mahala ambapo hakuna changamoto na hata hapo Simba wanakutana nazo lakini ni moja ya timu ambayo naishi nayo katika mazingira sahihi na kuna baadhi ya ndoto zangu nimepitia kupitia wao,” anasema na kuongeza kuwa;

“Unapokuwa katika timu ya daraja kama la Simba lazima ukubali kukutana na presha tena wakati ambapo inatokea mnafanya vibaya mara nyingi anatafutwa mbaya lakini yote kwa yote ndio maisha ya soka yalivyo.

“Nafurahia maisha ya Simba kwani ni timu ambayo kila panapokucha kuna malengo ya kufikia mafanikio ambayo hata wachezaji ambao wapo hapa wanatamani kuwa sehemu ya kutoa mchango na kile ambacho tumepanga kukifikia,” anasema.

KUONDOKA AZAM

Mwaka 2017, Simba iliwasajili wachezaji wanne kwa mpigo kutoka Azam FC, Manula, John Bocco, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe ambao walikuwa roho ya timu hiyo.

Manula anasema kuondoka kwenye timu hiyo haikuwa kwa ubaya bali ni masuala ya kazi mkataba wake ulipomalizika aliangalia namna ya kwenda kutafuta changamoto nyingine.

“Katika kufanya maamuzi ya kutafuta changamoto nyingine baada ya mkataba wangu na Azam kumalizika maamuzi yangu yakaamua kuja Simba ambayo ilikuwa moja ya timu nyingi kati ya zile ambazo zilikuwa zinanihitaji.

Ila hakuna jambo lingine lolote ambalo unaweza kusema lilichangia maamuzi yangu ya kuondoka na Azam na kuja Simba ambapo naamini ni mahali sahihi kwangu kutokana na mafanikio ambayo nimeyapata kwa muda niliokuwa hapa,” anasema Manula.

MENEJA WAKE

Manula ni miongoni mwa wachezaji ambao wanafanya vizuri nchini na Meneja wao ni mchezaji wa zamani wa Kariakoo Lindi, Jemedari Kazumari ambaye pia anafanya kazi na nyota wengine kama Shomary Kapombe.

“Miongoni mwa mambo ambayo najivunia ni kuwa na mtu ambaye anasimamia masuala yangu ya maslahi katika soka kwa umakini mkubwa anatamani kuona mchezaji wake nafanikiwa zaidi.

“Meneja wangu kwa sasa anafanya kazi katika chombo cha habari na katika kutaka kuniona nakuwa bora ikitokea siku nimekosea huwa si kuniambia tukiwa wawili bali katika kazi yake.

“Anafanya hivyo si kwa ubaya ila anataka kuona mabaya niliyonayo yanabadilika kwa maana ya kujirekebisha ili kuwa bora ndio maana nikiangalia nikifungwa bao kutokana na uzembe wangu anasema kweli,” anasema.

AIR MANULA

Manula anasema ilikuwa kama misimu mitatu nyuma iliyopita katika mechi ya Ligi Kuu Bara wakiwa ugenini dhidi ya Ndanda ndio jina hilo liliibuka.

“Nakumbuka mechi ile ilimalizika kwa suluhu na kuna shambulizi moja ambalo Ndanda walilifanya kuna mpira wa juu pembeni nilikwenda kuokoa nikapigwa picha ambayo niliiweka katika mitandao ya kijamii.



Nilivyoweka picha hiyo ambayo niliokoa shambulizi pamoja ndio jina na Air Manula lilianzia hapo kwani niliweka na ujumbe huo pale chini ya picha,” anasema na kuongeza kuwa;

“Tangu hapo kuna wachezaji wenzangu wa timu tofauti, mashabiki, ndugu na jamaa wakaanza kuniita jina hilo ambalo limekuwa kubwa mpaka wakati huu na nalitumia,” anasema Manula.
Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz