Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manula, Bacca, Mao wafuata nyayo za Ronaldo

Taifa Stars Msk Manula, Bacca, Mao wafuata nyayo za Ronaldo

Mon, 8 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ukitaka mafanikio iga waliofanikiwa, wahenga walisema. Ila hatuna hakika kama na hii imo kwenye kipengele hicho. Nyota wa Taifa Stars wameiga mambo ya Cristiano Ronaldo huko Misri.

Hii ilikuwa katika mechi ya kirafiki kati ya timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' na timu ya taifa ya Misri 'The Pharaos' iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, ambayo Stars ililaa 2-0.

Nyota wa Stars walioiga nyendo za Ronaldo ni kipa Aishi Manula, beki Ibrahim Bacca na kiungo Himid Mao Mkami, ambapo wakati wa kupiga picha ya kikosi kabla ya kuanza kwa mechi hiyo, walionekana wote wamesimamia ncha za viatu vyao.

Jambo hilo limekuwa kifanywa mara kwa mara na Ronaldo, ambaye anasemekana anataka kuonekana mrefu zaidi ya urefu halisi alionao.

Shabiki mmoja alisema: "Ronaldo licha ya mafanikio yote aliyonayo bado anataka zaidi. Yaani licha ya kuwazidi wenzake uwezo wa kusakata boli, pesa, umaarufu na rekodi za mabao, bado anataka awazidi hadi urefu."

TURUDI KWA STARS SASA

Kikosi cha Taifa Stars kitakachoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 kilikumbana na kipigo hicho kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, wakati kocha Adel Amrouche alipokuwa akitesti mitambo kabla ya kwenda kuliamsha Afcon.

Mohmoud Trezeguet alifunga bao la kwanza la Misri katika dakika ya 32 akimalizia pasi ya Mohamed Salah, bao liliodumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa Stars kubadilisha wachezaji wanne kwa mpigo kabla ya kuongeza wengine wawili baadaye na kuifanya timu icheze soka la ushindani.

Dakika ya 73 Aishi Manula alijikuta akitumbukiza mpira wavuni baada ya Mohamed Salah kupiga penalti iliyogonga besela na kumgonga kipa huyo mgongoni kuiandikia Misri bao la pili.

Licha ya kipigo hicho, Stars ikiongozwa na nahodha Mbwana Samatta na Simon Msuva ilicheza vyema na kuonyesha uwezo japo mastaa wa timu hiyo walikosa umakini kwenye kutumia nafasi walizozitengeneza.

Nahodha Mbwana Samatta alisema mechi dhidi ya Misri ilikuwa ni kipimo sahihi kabla ya kuivaa Morocco katika mechi yao ya ufunguzi wa kundi F Januari 17, akiongeza kwamba benchi la ufundi litafanyia kazi udhaifu uliojitokeza katika mechi hiyo dhidi ya timu bora ya Misri inayoongoza kwa kutwaa mataji saba ya Afcon.

Fainali za 34 za Afcon zitaanza Jumamosi hii ya Januari 13 kwa wenyeji Ivory Coast kuwaalika Guinea Bissau saa 5:00 usiku.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live