Wakati mashabiki wa Yanga wakisubiri kwa hamu kumuona winga Mkongomani, Manu Labota Bola kutua katika kikosi cha timu hiyo, mambo yamebadilika ghafla baada ya mabosi wa Singida Fountain Gate kupindua meza na kumbeba nyota huyo wa FC Lupopo baada ya kuweka dau kubwa mezani lililomvutia.
Yanga ilikuwa na hesabu za kumchukua Labota ikitangulia kuonyesha nia ya kumsajili kabla ya kupunguza kasi kidogo kuwania saini yake.
Singida juzi ilicheza na akili kubwa kwa kumpiga hesabu kali kwa kuamua kumpandia ndege Labota na kwenda kumaliza dili hilo kimyakimya, huko huko kwao jijini Lubumbashi.
Labota bado alikuwa na mkataba na Lupopo ambapo Singida ikatumia nguvu ya kigogo wao mmoja kumaliza dili hilo kwa kuwasiliana na rais wa klabu hiyo Jacques Kyabula Katwe ambaye pia ni gavana wa jiji hilo.
Winga huyo amesaini mkataba wa miaka miwili kuja kuitumikia Singida baada ya kuwa na miaka mitatu ndani ya Lupopo.
Kumaliza dili hilo Mwanaspoti linafahamu Singida ilimsafirisha mmoja wa vigogo wa timu hiyo Ramadhan Nswazurimo kumalizia usajili huo na wakati wowote wiki hii Bola atatua nchini kuja kuanza maisha mapya.
Taarifa kutoka Lupopo zinasema Singida imelazimika kutumia zaidi ya Sh250 milioni kukamilisha dili hilo la Labota baada ya Lupopo kuwa na hesabu za kutaka kumuuza Afrika Kusini.