Rafiki yangu Murtaza Mangungu ambaye ni Mwenyekiti wa Simba SC anapitia nyakati ngumu katika kitu chake pale Msimbazi.
Tangu Simba SC wapoteze mechi yao na Yanga SC, rafiki yangu Mzee Mangungu amewekwa kikaangoni na mashabiki wake, Wanamtaka ajiuzulu.
Huwa inatokea Tanzania tu, Simba SC wakishinda mechi zao, sifa haziendi kwa Mangungu. Zinaenda kwa viongozi wengine.
Ni kikundi kidogo cha watu kinachoweza kumpongeza Mangungu, lakini kundi kubwa linawapongeza viongozi wengine na wachezaji. Imetokea mara nyingi hii.
Ni kama ilivyokuwa kwa Mshindo Msola na Yanga SC, Katika muda mwingi ambao Mshindo alikuwa Mwenyekiti wa Yanga SC alikuwa akiwekwa kikaangoni na mashabiki timu ikipoteza mechi zake.
Msola ameishi hivi muda mrefu katika kiti chake pale Jangwani. Ni siku chache alizokuwa na amani Yanga SC wakipoteza mechi zake.
Muda mwingi roho ilikuwa mkononi siku Yanga SC wakipoteza mechi. Sijui kama Msola anatamani tena kuwa Mwenyekiti wa Yanga SC katika zama hizi.
Hivi sasa Mzee wangu Mangungu anapitia njia hii pale Msimbazi. Namuonea huruma Nafahamu mapenzi yake na Simba SC.
Mangungu ni Simba SC kweli kweli. Sijawahi kuwa na mashaka na Usimba wake, Ni vile tu, watu wamechagua kumuita jina baya Mbwa wasiyempenda.
Kuna njia mbili ya kumaliza hili lililoko, Njia ya kwanza ni Simba SC kurudi katika njia kuu haraka sana. Njia nyingine ni Mangungu mwenyewe kuachia ngazi kweli kama wanavyotaka watu wanaomsumbua.
Nafahamu kilichofanyika mpaka Lyod Nchunga alivyoondoka Yanga SC nyakati zile katika kiti chake cha Uenyekiti.
Kuna kundi la Makomandoo lilikwenda nyumbani kwa Nchunga usiku wa manane. Stori ikaishia hapo, kesho asubuhi Nchunga bila kugasiwa alitangaza kuachia madaraka yake Jangwani.
Maneno ya Mkunga Abdul Mkeyenge.