Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, umefunguka kwa mara ya kwanza sababu za kumuajiri Kocha wa viungo kutoka nchini Hispania Don Daniel De Castro.
Kocha Castro anayechukua nafasi ya Adel Zrane raia wa Tunisia, alitambulishwa rasmi juzi Jumatatu (Novemba 15) kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za klabu ya Simba SC.
Mwenyekiti wa klabu ya Simba SC Murtaza Mangungu, amesema kuajiriwa kwa kocha Castro, ni sehemu ya kukidhi matarajio ya klabu hiyo, sambamba na masharti yaliyowekwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ na lile la Tanzania ‘TFF’.
“Tumemchukua kwa sababu ya kukidhi matarajio ya klabu yetu, tumeona atatufaa, lakini kikubwa ni masharti ya CAF na TFF wanaotaka wataalamu hao ni lazima wafike viwango fulani, kwa hiyo sisi pamoja na kwamba tumeridhika naye, pia vigezo vyake vinakidhi na kukubaliana na masharti yaliowekwa na wanaoongoza soka,” amesema Mangungu.
Elimu ya Castro ni shahada ya utaalamu wa elimu ya mwili (UEFA-A) aliyoipata katika Chuo cha Laguna, Hispania mwaka 2010, huku pia akiwa na shahada ya mafunzo ya utimamu wa mwili katika soka aliyoipata 2018/19 kwenye chuo cha Madrid.
Pia amefanya kozi ya mafunzo ya uchambuzi wa viwango katika soka kutoka Chuo Kikuu cha Plytechnic Madrid mwaka 2018.
Kuhusu wasifu wa kocha huyo, msimu wa 2018 alikuwa kocha msaidizi wa Real Madrid wa vijana chini ya miaka 18 ambayo ilitwaa ubingwa wa Hispania, msimu wa 2020/21 alikuwa kocha msaidizi wa viungo wa timu ya Politehnica ya Romania na 2019/20 alikuwa kocha msaidizi wa viungo wa timu ya Rapid Bucharest ya Romania pia.