Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mangungu, Asha Baraka wawasha moto Simba

Asha Baraka Kdmd Mangungu, Asha Baraka wawasha moto Simba

Sat, 21 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Simba unaotarajiwa kufanyika Januari 29, mwaka huu jijini Dar es Salaam wameendelea kumwaga sera huku Murtaza Mangungu, mwenyekiti anayetetea nafasi yake, amesema anahitaji kuendeleza mazuri aliyoyafanya katika miaka minne iliyopita.

Katika nafasi hiyo, Mangungu anachuana na Moses Kaluwa.

Akizungumza jijini jana, Mangungu, alisema bado klabu iko katika mchakato wa kujenga uwanja wa kisasa ambao pia utakuwa na kumbi mbalimbali za mikutano.

“Wanachama naombeni ridhaa yenu ya kuongoza kwa mara nyingine, kuongoza nafasi hii ya uenyekiti wa klabu ya Simba ili kuendeleza mikakati ya maendeleo inayotarajiwa hasa kwa timu yetu kucheza hatua ya nusu au fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Nikipata nafasi hii tena ndani ya Simba, niwahakikishie nitaendeleza pale tulipoishia. Hatuna muda wa kujadili kwa sababu yanaonekana kutokana na ushirikiano mkubwa wa baadhi ya klabu kubwa Afrika ikiwamo Al Ahly ya Misri na CSK Moscow katika mambo ya kiufundi,” alisema Mangungu.

Aliongeza mipango ya bodi ya klabu hiyo ni kuifanya Simba kuwa bora zaidi na kujenga mifumo mizuri katika kuongeza mapato pamoja na kusimamia vyema soka la vijana.

“Kuhusu kukosa furaha hasa mechi na Yanga, msimu uliopita tulipoteza, sio kwa uzembe wa uongozi bali ilikuwa bahati mbaya, nitatumia nafasi inayofuata kufanya vizuri katika michuano yote tunayoshiriki bila kuangalia timu tunayokutana nayo,” Mangungu alisema.

Naye Asha Baraka anayetetea nafasi ya Mjumbe Mwanamke katika Bodi ya Wakurugenzi alisema anawaomba  wanachama wampe dhamana ya kuongoza tena katika nafasi hiyo ili aendelee kuwapa furaha.

Asha alisema anajivunia mafanikio ambayo Simba Queens imeyapata katika miaka minne aliyokabidhiwa timu ambapo ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania kwa misimu mitatu mfululizo.

“Nimefanikiwa kwa kipindi chote kutwaa mataji mbalimbali kama Ligi Kuu, CECAFA ambayo mara ya kwanza tulikosa kwa kutofanya vizuri kutokana na ugeni wa mashindano lakini msimu uliopita niliongoza timu vyema na kufikia malengo yetu na kutetea ubingwa, lakini kwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika," alisema Asha.

Selemani Haroub, anayewania nafasi ya ujumbe kwa awamu nyingine anawaomba ridhaa wanachama ili kukamilisha kazi nzuri waliyoianza pamoja na viongozi waliokuwa madarakani.

“Mafanikio yaliyopatikana Simba ni kutokana na ushirikiano wenu wanachama, kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa, Simba kuwa katika nafasi ya 10 katika anga za kimataifa, kwa sasa malengo yetu ni kutwaa ubingwa Afrika, naomba ridhaa yenu ya kuwaongoza kwa mara nyingine ili kufikia malengo haya.

Naombeni nafasi nyingine ili kufanikisha ushindi na kufikia malengo, kutokana na kuwa ni sehemu ya watu waliofanikisha baadhi ya wachezaji wa Simba kutoka katika kituo changu akiwamo Beno Kakolanya na Oppa Clement,” alisema Selemani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live