Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mangalo aiwahi Simba, aipiga mkwara mzito

Mangaloo  Majid Mangalo aiwahi Simba, aipiga mkwara mzito

Sat, 9 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Singida Fountain Gate kinaendelea kujiandaa na pambano lijalo la ugenini dhidi ya Simba, huku eneo la ukuta likipata mzuka kutokana na kurejea kwa beki kisiki, Abdulmajid Mangalo aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu kuliwahi pambano hilo, huku akiwatuliza mashabiki kwamba licha ya matokeo mabaya, lakini wapo tayari kupambana.

Singida iliyohamishia maskani jijini Mwanza itakuwa wageni wa Simba keshokutwa, huku nahodha huyo wa timu hiyo akitamba kwamba anashukuru amerejea na atashirikiana na wenzake kuhakikisha wanapata matokeo mbele ya Mnyama na mechi nyingine ili kujiweka pazuri, kwani wamerejea kwenye ligi na mguu mbaya kti kinachowasononesha.

Nahodha huyo aliyekuwa nje kwa muda mrefu na kukikosa mechi tano zilizopita akiuguza jeraha la mguu tangu alipoumia katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2024 dhidi ya Simba iliyopigwa Januari 10 visiwani Zanzibar.

Mangalo aliyewahi kuwika na Biashara United kabla timu hiyo haijashuka daraja kwenda Ligi ya Championship, ameishuhudia timu hiyo ikirejea kwenye ligi tangu mwanzoni mwa mwezi uliopita ikicheza mechi tano mfululizo ikiambulia sare moja ya 1-1 dhidi ya Tabora United na kupoteza minne mbele ya Kagera Sugar (1-0) sawa na Azam, ikalala 3-1 kwa Tanzania Prisons 3-1 kisha kuchapwa 2-0 na Mtibwa Sugar 2-0 na kuporomoka hadi nafasi ya 10 kutoka ya tano iliyokuwa ikiishikilia awali kabla ya ligi kusimama kupisha Kombe la Mapinduzi na Afcon 2023.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mangalo amesema tayari ameanza mazoezi mepesi na huenda mchezo ujao dhidi ya Simba Machi 12 akaonekana uwanjani kuipambania timu yake ambayo hali yake haijawa nzuri.

Amesema matokeo wanayopitia kwa sasa yanaumiza kichwa akieleza kuwa anaamini kwa ushirikiano na wenzake huenda kuanzia mechi zijazo wakaanza kurejesha ubora wao.

“Nimeanza mazoezi naamini hadi mechi ijayo naweza kuwa fiti tayari kwa kurejea katika majukumu yangu, matokeo siyo mazuri lakini kwa ushirikiano wa wenzangu tunaweza kubadili upepo,” amesema Mangalo.

Amesema licha ya mabadiliko kikosini kuchangia hali ya matokeo, lakini anaamini timu hiyo itafanya vizuri kwani mpira hutoa matokeo matatu na sasa Singida FG imepitia pagumu ila mambo yatakaa sawa.

Singida itaikabili Simba katika pambano la nne katika Ligi Kuu tangu ipande daraja msimu uliopita ikifahamika kwa jina la DTB kabla yua kubadilishwa na kuwa Singida Big Stars, huku ikiwa haijawahi kupata ushindi, kwani katika mechi tatu zilizopita imepoteza mbili, huku mchezo mwingine ukiisha kwa sare.

Lakini itakutana na Simba ambayo jioni ya leo itakuwa ugenini jijini Tanga kuvaana na Coastal Union, huku ikiugulia maumivu ya kipigo cha mabao 2-1 nyumbani kutoka kwa Tanzania Prisons na kutibua hesabu za ubingwa kwa wababe hao walitwaa mataji 22, saba pungufu na iliyonayo Yanga tangu Ligi ya Bara ilipoasisiwa mwaka 1965.

Pia Singida itavaana na Simba ikiwa na benchi jipya la ufundi chinui ya Ngawina Ngawina baada ya uongozi kulivunja lililokuwepo lililokuwa chini ya Msauzi, Thabo Senong na mechi ya mwisho baina ya timu hizo Singida ililala nyumbani kwa mabao 2-1.

Chanzo: Mwanaspoti