Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mangalo: Huyu Mayele apewe heshima yake

Mangalo Tenaaaa Mangalo

Sat, 19 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

BEKI na nahodha wa Biashara United, Abdoulmajid Mangalo, ni kati ya wachezaji wanaotajwa sana kwenda Simba au Yanga katika usajili.

Lakini usajili unapofungwa tu, basi jina lake halionekani Simba au Yanga, na mwisho wa siku anaendelea kubakia Biashara. Championi Ijumaa limefanya mahojiano maalum na Mangalo na kikubwa akizungumzia sababu za yeye kushindwa kutua katika klabu hizo kongwe hapa nchini.

MALENGO YENU NI YAPI MSIMU HUU?

Malengo yetu ni kurejesha heshima ambayo tulikuwa nayo katika msimu uliopita ya kumaliza ligi katika nafasi ya nne kwenye msimamo. Kikubwa wasikate tamaa mashabiki wetu na badala yake waendelee kutusapoti katika michezo hiyo ili tufanikiwe kufika mbali zaidi.

“Kama wachezaji, tuna nafasi kubwa ya kupambana na kurejesha heshima hiyo tuliyokuwa nayo msimu uliopita.

AFUNGUKIA KWENDA SIMBA AU YANGA

“Sisi wachezaji maisha yetu ya kimpira tunaangalia zaidi maslahi na siyo kitu kingine chochote, hivyo ni lazima tuangalie dau la usajili na mshahara tutakaokuwa tunapata katika kila mwezi.

“Kwani mpira ni maisha yetu, hivyo inapotokea nafasi ya kusajiliwa basi ni lazima uangalie maslahi yako binafsi kama yamekaa vizuri ndiyo ufanye maamuzi.

“Na mimi kwangu kuondoka hapa Biashara ni suala la muda pekee ambalo lipo hivi sasa chini ya wasimamizi wangu wanaosimamia katika soka.

“Ninaamini bado mambo yanakwenda vizuri katika usajili wa timu hizo mbili, Simba au Yanga, ni suala la muda tu, ninaamini kila kitu kitakaa sawa.

ILIKUWAJE UKASHINDWA KUSAJILIWA SIMBA NA YANGA?

“Hilo suala lipo chini ya uongozi wangu unaosimamia, wao ndiyo watakaotakiwa kunipa ripoti au taarifa za timu hizo mbili ambazo kila mchezaji anatamani kuzichezea. “Lakini viongozi hao hawawezi kuamua kila kitu, hivyo ni lazima wanishirikishe katika kila kitu mara baada ya kufikia muafaka mzuri na moja kati ya timu hizo mbili kubwa hapa nchini.

VIPI UTAENDELEA KUWEPO SANA HAPA BIASHARA?

“Hapana, katika hilo halitawezekana mimi kuwepo hapa milele, kwani mpira ni sehemu ya maisha yangu, hivyo timu itakayofikia muafaka wa kuhitaji saini yangu, basi nitaondoka.

“Hapa Biashara nipo kikazi pekee, ninafanya kazi kwa ajili ya kutengeneza maisha yangu ya baadaye, hivyo nitaendelea kuitumikia kwa kipindi chote nitakachokuwepo hapa.

APIGA HESABU KUCHEZA SOKA NJE YA NJE

“Kila mchezaji ana malengo yake na kubwa ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi baada ya kucheza soka la hapa nyumbani na kuonekana.

“Kwani bila ya kuonekana katika ligi ya hapa nyumbani, ngumu kupata mafanikio ya kwenda kucheza soka nje ya nchi kama ilivyokuwa kwa waliotutangulia katika soka.

“Nikiwa nawaniwa na baadhi za klabu hapa nchini, lakini bado kuna mipango mingine mizuri niliyonayo ya kwenda kucheza nje ambayo ipo chini ya menejimenti yangu inayonisimamia.

“Hivyo lolote linaweza kutokea mwishoni mwa msimu huu, iwe kucheza hapa nyumbani nje ya Biashara au nje ya nchi kwa maana ya kucheza soka la kulipwa. “Kikubwa ninaamini uwezo nilionao wa uwanjani wa kucheza soka, hivyo katika hilo ninaamini nitafanikiwa katika msimu huu.

“Katika nafasi hii ninayocheza ninaamini popote ninaweza kucheza, licha ya kuwepo wachezaji wengine wanaocheza nafasi hii wenye uwezo mkubwa ambao hautofautiani na mimi.

KUMBE KIRAKA BANA “Tofauti na uwezo wangu wa kucheza nafasi ya beki wa kati, lakini ninamudu kucheza nafasi zote za beki wa pembeni namba mbili na tatu.

“Pia kiungo mkabaji namba sita ambayo nimekuwa nikicheza hapa Biashara pamoja na nafasi zote za winga namba 7 na 11.

“Hivyo makocha wengi wanaokuja hapa Biashara wamekuwa wakinitumia kucheza beki wa kati, imetokana na kuvutiwa kuzimudu nafasi hizo.

AMTAJA MAYELE NDIO KIBOKO MSIMU HUU

“Kiukweli Mayele (Fiston) anahitaji kupewa heshima yake, kwangu ni kati ya washambuliaji bora katika msimu huu mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao.

“Mimi kila mshambuliaji au winga ninayekutana naye nimekuwa na tabia ya kuheshimu uwezo wake, hiyo ndiyo siri kubwa kwangu kuwamudu.

“Kwangu namsifu Mayele kwanza ana sifa kubwa ya kuwasumbua mabeki wa timu pinzani kutokana na kucheza na nafasi hasa akiwa uwanjani akisubiria pasi kutoka kwa viungo wake.

“Ili uweze kumzuia ni lazima umkabe ‘man to man’ na usifanye makosa kumpa nafasi ya kumiliki mpira ndani ya 18, ukimuachia nafasi basi hakuachi anakufunga ikiwemo kichwa, kumchambua kipa au kupiga shuti.

“Ukimpa nafasi ya kumiliki mpira kutokana na kontroo, kasi na uwezo wa kukokota mpira akiwa katika kasi kubwa ya kulishambulia goli la timu pinzani, kama una spidi ndogo haumpati, utashangaa yupo ndani ya 18.

“Na mzuri sana katika mipira ya vichwa, utamuona leo (juzi) alipiga mipira mingi ya vichwa ambayo ilikuwa hatari iliyotoka nje kidogo ya goli letu.

“Licha ya umbile langu kubwa, lakini yeye ndiye aliyepiga vichwa vingi kunizidi mimi golini kwetu mimi nikipambana kuokoa na yeye kufunga, kiukweli ni mshambuliaji hatari sana kwa upande wangu katika msimu huu, ni mshambuliaji wa kuchungwa sana na mabeki wa timu pinzani,” anasema Mangalo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live