Licha ya kuwa ni pambano la utangulizi, waandaaji wa pambano la Karim 'Mandonga' Said na Daniel Wanyonyi walilazimika kulifanya kuwa kama ndilo pambano kuu, usiku wa kuamkia jana, Mandonga akishinda kwa Technical Knock Out (TKO).
Mandonga aliibuka kinara raundi ya sita baada ya mpinzani wake kusalimu amri na kutorudi ulingoni kuanza kwa raundi ya saba kwenye ukumbi wa KICC katika pambano hilo la lililokuwa la raundi 10 la uzani wa middle na la kwanza la kimataifa kwa Mtanzania huyo.
Msaidizi wa ulingo na kocha wa Mandonga, Juma Ndambile ameiambia Mwanaspoti moja kwa moja kutoka Kenya kwamba, Wanyonyi kama asingesoma alama za nyakati alikuwa anapigwa kwa Knock Out (KO).
"Nilimwambia Mandonga, raundi ya saba nenda ukamalize kazi, ilikuwa tunampiga vibaya, akawa mjanja hakurudi ulingoni," alisema kocha huyo mpya wa Mandonga huku akichambua raundi sita za pambano hilo zilivyokuwa.
"Tulipoanza raundi ya kwanza nilimwambia amsome mpinzani wake hadi raudi ya pili, raundi ya tatu tuliporudi nilimtaka aanze kupigana akimzunguka kupitia upande wa kulia, alinisikiliza, japo guard yake ilikuwa wazi.
"Raundi ya nne nilimsisitiza kucheza akificha uso, alifanya vizuri na kuongoza hadi raudi ya tano, ya sita ilikuwa ni nusu kwa nusu, wote walipigana, tulipokwenda mapumziko nikamwambia raundi ya saba ni ya kumaliza mchezo, lakini mpinzani wake aliona mambo magumu na kutorudi tena ulingoni," alisema Ndambile. Mandonga alibadilishiwa mpinzani mwishoni, awali ilikuwa azichape na Denzel Okoth
UBORA ULINGONI
Tangu pambano la Novemba mwaka jana alipomchapa Said Mbelwa, Mandonga ameoneka kuimarika na kushinda mfululizo, jambo ambalo mwenyewe alisema ni kubadili ratiba ya mazoezi huku Ndambile akifichua kwamba awali bondia huyo mwenye tambo hakuwa na mbinu na ufundi.
"Nilipoanza kumfundisha, alikuwa anacheza tu, hakuwa na tageti ya ngumi, kubalansi pumzi, wala hakuwa na mbinu, yeye alikuwa akijipigia tu ngumi, nilimwambia bondia hatakiwi kuanza tu kupigana, nilimpa programu ya mazoezi ambayo ameizingatia na inampa matokeo," alisema.
AITEKA KENYA
Mashabiki wa ndondi nchini Kenya wengi walikuwa 'team' Mandonga, licha ya mabondia wa nchi hiyo akiwamo mmoja wa mastaa wao wa ndondi, Rayton Okwiri kucheza usiku huo, waandaaji walilazimika kufanya pambano la Mandonga kuwa la mwisho likitanguliwa na pambano kuu la Okwiri na Mtanzania, Shaban Ally Ndaro aliyepigwa kwa pointi.
"Asilimia kubwa ya mashabiki walikuwa wakimshangilia Mandonga ukumbini, walianza tangu Jumatatno tulipowasili hadi siku tunapima uzani na kwenye pambano, Wanyonyi alikuwa kama anapigana ugenini," alisema Ndambile.
Kwenye mitandao ya kijamii baadhi ya mashabiki Kenya waliandika,waandaaji wagawane pesa na Mandonga sababu ameifanya kwa mara ya kwanza Kenya nzima kufuatilia mchezo wa ngumi, mwingine kabla ya pambano aliandika Mandonga anakuja kupigana na Mkenya anaitwa Wanyonyi ambaye hatumfahamu, tuasikia pambano hilo ni la utangulizi lakini hadi sasa hatujajua pambano kuu ni la nani na nani?.
BILA SH15 MILIONI HAPIGANI
Baada ya pambano hilo, Ndambile alisema Mandonga sasa amepata ofa za kwenda kupigana Uingereza, Msumbiji na Maurtius hivyo wanaangalia watakapopewa ofa nzuri ndipo atakwenda.
"Dau lake kwa sasa si chini ya Sh 15 Milioni, Mandonga alianza kulipwa vizuri kwenye pambano na Kaoneka (Shaban ambalo alipigwa) na lile la Said Mbelwa (alishinda) hata hili la Kenya amelipwa vizuri pia," alisema.
Akizungumzia kupigana mfululizo, Ndambile alisema hakuna athari kwa bondia huyo kwani kabla ya kusaini mkataba anapimwa kama hana tatizo kwenye ngumi za kulipwa anapigana," alisema.
Bondia huyo aliwasili nchini jana saa nne usiku akitokea Kenya ambako amesema yuko tayari kurudi tena nchini humo kuzichapa na bondia yoyote akiwamo Wanyonyi kama atahitaji marudiano.