Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manchester United yagongwa na Brighton

Brighton Vs Man United Manchester United yagongwa na Brighton

Sat, 24 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Manchester United tabu iko palepale. Ndicho unachoweza kusema baada ya kuruhusu bao la dakika za majeruhi, wakati Joao Pedro alipofunga dakika 95 kuipa ushindi Brighton wa mabao 2-1 dhidi ya Man United kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika uwanjani Amex.

Danny Welbeck aliifungia Brighton bao la kuongoza dakika ya 32, lakini Amad Diallo alikuja kusawazisha kwa shuti la kubabatiza kwenye kipindi cha pili. Wakati mechi hiyo ikionekana kama ingemaliza kwa sare, Pedro alikuja kuamua matokeo ya mwisho baada ya kufunga kwa kichwa kufuatia krosi maridadi ya Simon Adingra na hivyo kuipa pointi zote tatu Seagulls.

Man United ilipoteza nafasi ya kufunga bao mapema tu kwenye kipindi cha kwanza baada ya Amad kushindwa kumalizia vyema krosi ya Diogo Dalot kwa kuamua kuunganisha kwa mguu badala ya kupiga kichwa.

Wakati Man United ikionekana kuishika mechi, mambo yamebadilika baada ya Brighton kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Welbeck kufuatia krosi safi ya mpira wa chinichini iliyopigwa na Kaoru Mitoma dakika chache baada ya Marcus Rashford bao lake kukataliwa.

Man United ilikuwa na kipindi cha kwanza kizuri, lakini walijikuta wakiwa nyuma hadi mapumziko kwa bao hilo la Welbeck, ambalo lilikuwa la 100 kwake kwenye maisha yake ya soka la ngazi ya klabu.

Brighton nusura ifunge bao la pili kupitia kwa James Milner baada ya Diogo Dalot kuokoa mpira huo kwenye mstari, kabla ya Welbeck kupiga mpira kichwa uliotoka sentimita chache kutoka kwenye goli la Man United.

Man United ilisawazisha kwenye dakika 60 baada ya shuti la chinichini la Amad kumbabatiza beki wa Brighton, Jan Paul van Hecke. VAR ilihusika kutazama bao hilo kama kutakuwa na tukio la kuotea, lakini lilikubalika na kufanya ubao wa matokeo kusomeka 1-1.

Man United ilidhani kwamba imefunga bao la pili kupitia kwa Alejandro Garnacho kwenye dakika ya 70, lakini bao hilo lilikataliwa baada ya mpira kumgonga Joshua Zirkzee, aliyekuwa kwenye eneo la kuotea kwenye mstari wa goli la Brighton na hivyo bao hilo kukataliwa.

Baada ya hapo kila timu ilikuwa inapambana kutafuta bao la pilii na hapo ndiyo Brighton ilipojitofautisha na Man United kwa bao la kichwa la mchezaji Pedro kufuatiwa pasi maridhawa ya Adingra, aliyeingia dakika chache kutokea benchini.

Joao Pedro alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo, ambao uliwafanya Man United kupoteza mechi yao ya kwanza kwenye mechi mbili ilizocheza kwenye Ligi Kuu England kstika msimu huu wa 2024-25.

TAKWIMU ZA MCHEZO - BRIGHTON VS. MAN UTD

-Umiliki mpira: Brighton 47.7%, Man United 52.3%

-Mashuti golini: Brighton 5, Man United 4

-Mashuti yote: Brighton 14, Man United 11

-Kugusa mpira: Brighton 642, Man United 669

-Pasi zote: Brighton 463, Man United 507

-Kuokoa hatari: Brighton 11, Man United 10

-Kona zote: Brighton 4, Man United 4

Chanzo: Mwanaspoti