Kiwango matata cha uwanjani cha Manchester United chini ya Kocha Erik ten Hag kimeanza kumtisha shabiki wa Liverpool, Jamie Carragher.
Man United kwa sasa ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Leeds United usiku wa Jumatano iliyopita, huku kikosi hicho kikicheza mechi 16 bila ya kupoteza katika Uwanja wa Old Trafford katika michuano yote huku ikiwa kwenye michuano yote minne ikiwania mataji kuanzia Europa League, Kombe la Ligi, Kombe la FA na Ligi Kuu England.
Wakati sasa akiwa hawapi nafasi ya kushinda Ligi Kuu England, Carragher alisema Man United inavyojengwa kuna kitu kinakwenda kutokea.
“Naona kitu tofauti sana chini ya Erik ten Hag,î alisema Carragher. ìSiku zote niliona kuna mitazamo hasi ya makocha waliopita. Kipindi cha Jose Mourinho niliona kulikuwa na shida baina yake na bodi. Chini ya Louis van Gaal, aidhani kama mashabiki walimfurahia kwa staili ya soka lake. Na chini ya Ole (Gunnar Solskjaer), sidhani kama kuna mtu alifikiria kuwa ni kocha wa kuipa Man United taji.
“Lakini sasa nadhani wamepata kocha anayejua nini anafanya. Pia kuna hali furahi kwenye kikosi cha Man United ambayo ilitoweka kwa muda mrefu. Nadhani wanarudi. Kuna kitu kinatokea Man United ambacho kwa makocha wengine waliopita hakikuwepo. Wanaanza kunitisha!”
Carragher anaamini Top Four ya Ligi Kuu England itabaki hivyo hivyo hadi Mei 28. Hiyo akiwa na maana anaamini Arsenal wataendelea kubaki kileleni na kushinda ubingwa wa kwanza tangu mwaka 2004.
Wakati huo huo, matajiri watano wameonyesha dhamira ya dhati ya kununua klabu ya Man United. Klabu hiyo ya Old Trafford imewekwa sokoni tangu Novemba mwaka jana, wakati familia ya Glazer ikiakmua kuipiga bei hiyo kufuatia maandamano ya mara kwa mara ya mashabiki.
Familia ya Glazer inasubiri kuingiza Pauni 6 bilioni kwenye mauzo ya klabu hiyo, lakini mkwanja wa Pauni 4.1 bilioni hadi Pauni 4.5 bilioni unaweza kukubaliwa pia, huku Pauni 2 bilioni ya ziada ikitarajiwa kuwekezwa kwenye kuboresha miundombinu ya Old Trafford na Carrington.