Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manchester United waanza mbwembwe, wasema bado matatu yanakuja

WhatsApp Image 2023 03 01 At 14.jpeg Wachezaji wa Man United wakishangilia Ubingwa wa Carabao Cup

Wed, 1 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Goma linaendelea na Manchester United wanasema, yajayo yanafurahisha. Usiku wa juzi Jumapili, miamba hiyo inayonolewa na Mdachi, Erik ten Hag yenye maskani yake Old Trafford ilimaliza ukame wa mataji baada ya kubeba Kombe la Ligi baada ya kuichapa Newcastle United 2-0 kwenye mchezo wa fainali uliofanyika uwanjani Wembley. Mabao ya Casemiro na Marcus Rashford yaliyofungwa ndani ya dakika sita yalitosha kwa Man United kunyakua kombe hilo, ambalo ni taji lao la kwanza kwa msimu huu wa 2022/23.

Man United kwa msimu huu ipo kwenye msako wa mataji manne, moja tayari wameshabeba na yamebaki matatu. Man United ipo kwenye mbio za ubingwa wa Kombe la FA, Europa League na Ligi Kuu England.

Kombe la Ligi ni taji lao la kwanza tangu mwaka 2017 na huenda mwaka huu ukawa mtamu zaidi kwao kutokana na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kubeba mataji mengine wanayoshindania. Fainali hiyo ya juzi ni kama marudio ya fainali ya mwaka 1999, ambapo miamba hiyo miwili Man United na Newcastle United ilikutana kwenye Kombe la FA. Walipigwa 1999 na juzi walipigwa tena, hivyo Newcastle United ukame wao wa mataji unaendelea kwa miaka 54 sasa.

Man United imekuwa kwenye kiwango bora kabisa kwa sasa, ambapo ilikwenda Wembley ikiwa imefunga mabao 16 na kupoteza moja katika mechi 20 za mwisho, wakati Newcastle wao walikuwa wameshinda mechi sita kati ya 10 za mwisho.

Na baada ya Casemiro kufunga kwa kichwa kufutia friikiki ya Luke Shaw kwenye dakika 33, ilionyesha wazi kwamba hiyo ilikuwa siku bora kwa Man United kuanza zama mpya za mataji chini ya kocha wao Mdachi, Ten Hag.

Dakika tano baadaye, Sven Botman alibabatiza mpira wa Marcus Rashford na hivyo kumshinda kipa Loris Karius – na kutinga nyavuni na hapo, Man United wakaweka mikono kwenye taji lao la sita la Kombe la Ligi.

Mataji manne kwa Man United msimu huu bado inawezekana, ambapo miamba hiyo imepenya hatua ya 32 kwa ushindi wa kibabe kabisa mbele ya Barcelona, Alhamisi iliyopita na kutinga hatua ya 16 bora, ambapo wamepangiwa kukipiga na Real Betis kwenye hatua hiyo. Man United bado ina nafasi ya kunyakua taji hilo.

Man United imetinga pia raundi ya tano kwenye Kombe la FA na watakipiga na West Ham United, kesho Jumatano. Timu nyingine zilizotinga tano bora ya Kombe la FA - ni Leicester City, Blackburn Rovers, Stoke City, Brighton, Fulham, Leeds United, Bristol City, Manchester City, Southampton, Grimsby Town, Burnley, Fleetwood, Sheffield United na Tottenham. Hao ndiyo waliosimama kwenye njia ya Man United katika msako wao wa Kombe la FA.

Taji jingine wanalosaka ni la Ligi Kuu England. Kunyakua taji hilo kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 10 si kitu kinachoshindikana kwa mabingwa hao mara 20 wa England, ambapo kwa sasa wameachwa pointi nane na vinara Arsenal na bado kuna mechi 14 za kucheza, sawa na pointi 42. Endapo kama Arsenal itashinda mechi yake ya kiporo usiku wa kesho Jumatano dhidi ya Everton, basi pengo la pointi na Man United litakuwa pointi 11, lakini chama la Ten Hag litakuwa na mechi moja mkononi.

Kwa msimamo ulivyo kwa sasa, Man United imeachwa pointi sita na Man City kwenye msimamo wa ligi, lakini wapo mechi moja nyuma, hivyo wakishinda kutakuwa na pengo la pointi tatu - huku Man City na Arsenal bado zina mchezo mmoja wa kumenyana wenyewe kwa wenyewe.

Kwenye Europa League, ambako Man United bado inashindania ubingwa mbele yao timu zilizotinga hatua ya 16 ambazo italazimika kuchuana nazo ni Bayer Leverkusen, Ferencvaros, AS Roma, Real Sociedad, Sporting CP, Arsenal, Union Berlin, Union St Gilloise, Juventus, Freiburg, Sevilla, Fenerbahce, Shakhtar Donetsk na Feyenoord.

Kwenye Ligi Kuu England, mechi 14 ilizobakiza Man United kwenye msako wao huo wa pointi 42 watakipiga na Liverpool, Southampton, Brighton, Newcastle, Brentford, Everton, Nottingham Forest, Chelsea, Tottenham Hotspur, Aston Villa, West Ham, Wolves, Bournemouth na Fulham.

"Bado tumo," alisema Paul Scholes, kiungo wa zamani wa England na Man United, akiongeza. "Katika Ligi Kuu tano kubwa za Ulaya, sisi pekee yetu bado tupo kwenye vita ya kusaka mataji manne. Si unaona, ngumu lakini hakuna ajuaye."

Michael Owen, straika wa zamani wa Liverpool, Real Madrid, Newcastle United, Stoke City na Man United alisema: “Kila mtu anafahamu kuna kupanda na kushuka na mambo ya kushtua yanatokea. Hakuna anayewataja Man United.

Wanawafikiria Man City, lakini kama Man United watashinda mechi yao ya mkononi, pengo litakuwa pointi tatu nyuma ya Man City, hivyo huwezi kuwaondoa kwenye vita ya ubingwa Man United kwa kipindi hili. Lakini, Arsenal ndio watu wa kupoteza kwa sababu ndio walioshika usukani kwa sasa.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live