Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manchester City na Girona, sijui itakuwaje

Manchester City.jpeg Manchester City na Girona, sijui itakuwaje

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ulaya mpira ni biashara kubwa sana. Wafanyabiashara wakubwa wanawekeza pesa zao kwenye mpira kama wale wa Tanzania kwa mfano wanavyowekeza kwenye biashara nyingine kama mabasi au vituo vya mafuta.

Utakuta tajiri mmoja ana mabasi yanayoenda Mwanza, Tanga, Mtwara au Kigoma.

Au ana vituo vya mafuta katika kila mkoa wa nchi hii, na wengine hadi nje ya nchi.

Basi na wenzetu huko wanafanya hivyo kwenye mpira.

Watu wanawekeza kwenye ligi mbalimbali, kama wale jamaa wa Red Bull na timu zao za RB.

Kuna RB Leipzig ya Ujerumani, RB Salzburg ya Austria, New York Red Bulls na Red Bull Brasil.

Lakini katika watu hao, hakuna aliyewekeza namna hii kama matajiri wa Manchester City ya England.

Jamaa hao ni City Football Group Limited (CFG), kampuni hodhi inayoendesha klabu kadhaa duniani.

Kampuni hii inamilikiwa na taasisi tatu tofauti lakini mwenye hisia nyingi zaidi ni Abu Dhabi United Group wenye asilimia 81.

Wengine ni Kampuni ya Kimarekani ya Silver Lake yenye asilimia 18 na kampuni mbili za Kichina za China Media Capital na CITIC Capital zenye asilimia 100 kwa pamoja.

Kwenye biashara zenye asili ya kibepari kama hizi, mwenye hisia nyingi ndiye mwenye sauti kubwa.

Kwa hiyo hapa utabaini moja kwa moja kwamba Manchester City kwa kifupi inamilikiwa na Abu Dhabi United Group kwa sababu ndiyo wenye asilimia nyingi ya hisa.

Abu Dhabi United Group ni kampuni inayomilikiwa na Sheikh Mansour bin Zayed Al Nahyan, mwana familia ya kifalme ya Abu Dhabi Royal Family na waziri wa mambo ya kirais ya Falme za Kiarabu.

Kupitia kampuni yake ya City Football Group, mwamba huyu pia anamiliki timu za New York City ya Marekani, Melbourne City ya Australia, Yokohama F. Marinos ya Japan, Montevideo City ya Uruguay, Sichuan Jiuniu ya China, Mumbai City ya India, Lommel SK ya Ubelgiji, Troyes ya Ufaransa, EC Bahia ya Brazil, Club Bolivar ya Bolivia na Girona ya Hispania.

Kwa kifupi Sheikh Mansour anamiliki timu katika Mabara ya Ulaya, Asia, Australia na Amerika zote...kasoro Afrika tu.

Lakini kwa mujibu wa sheria ya Shirikisho la Soka la Ulaya, UEFA, timu mbili tofauti zinazomilikiwa na mtu au taasisi moja haziruhusiwi kushiriki mashindano ya aina moja.

Hii ni kwa mujibu wa ibara ya tano ya uadilifu wa mashindano (Uefa Article 5 - Integrity of the competition)

Sasa hapa ndipo kwenye utata kwa City Football Group na Sheikh Mansour wake.

Timu ya Girona ya Hispania inafanya balaa kwenye La Liga na hadi sasa inaongoza.

Ushindi wa ugenini wa mabao 4-2 dhidi ya Barcelona umewashtua wengi na kuwafanya waendelee kujikita kileleni mwa msimamo.

Mambo yakiendelea hivi hadi mwisho wa msimu maana yake Girona itafuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani.

Na endapo Manchester City ya England itafuzu pia maana yake tayari kutakuwa na timu mbili za mtu mmoja kwenye mashindano ya aina moja.

Ibara ya tano itahusika...ndipo kwenye swali, sijui itakuwaje?

Wale wenzao wa Red Bull ambao wana timu za RB Leipzig ya Ujerumani na Red Bull Salzburg ya Austria walishayashtukia haya mapema.

Walipogundua kwamba hii itawapa shida, wakaifanyia mabadiliko ya kimuundo klabu ya RB Salzburg ya Austria na wao kujiweka pembeni na kubaki kama wadhamini, siyo wamiliki.

Hii ilikuwa kabla ya msimu wa 2017/18 pale timu hizo zote zilipofuzu kwa mara ya kwanza kushiriki kwa pamoja Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Walipoona kwamba yawezekana timu zote zikafuzu, wakachanga karata zao vizuri na kutafuta pa kujifichia.

Hawa jamaa wako makini sana kwenye kuzikwepa sheria kwa mujibu wa sheria. Kwa mfano, Ujerumani hairuhusiwi timu za michezo kutumia majina ya biadhaa za kibiashara.

Lakini wao timu zao zote wanazomiliki lazima zitumie jina lao la Red Bull, au RB kwa kifupi.

Kwa hiyo ili kuikwepa sheria hii kwa timu yao ya RB Leipzig, wakajifanya ile RB pale siyo Red Bull bali ni kifupisho cha RasenBallsport ambayo maana yake ni timu ya mchezo wa kwenye nyasi.

Nembo yao ni ile ile na hata uwanja wao unaitwa Red Bull Arena...ila tu kwenye timu, RB ndiyo eti siyo Red Bull.

Hii ilikuwa chenga ya mwili kwa sheria za Ujerumani.

Lakini kwa City Football Group na Sheikh Mansour kwao ni tofauti.

Hadi sasa hawajafanya chochote kilicho wazi kuona wataiepuka vipi hii sheria.

Na kama hawataiepuka, maana yake watakubali timu mojawapo katika hizi mbili, Manchester City na Girona, isishiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Na au labda wanasubiri hatima ya Manchester City kwenye zile kesi zao za kukiuka sheria ya matumizi ya fedha (FFP).

Au labda kutokana na mwenendo wao wa kusuasua kwenye Ligi Kuu ya England, wanaweza wasifuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Hayo yote ni kama...yaani kama alivyoimba Mnyalu Mike Tee.

Swali kinabaki, itakuwaje endapo Girona watafuzu kwa ligi ya mabingwa, na Manchester City wakafanya hivyo.

Chanzo: Mwanaspoti