Haji Manara ameweka sawa ufafanuzi baada kuandika makala ya kumsifia mtangazaji wa soka wa Azam TV, Gharib Mzinga huku mchambuzi wa soka nchini Jemedari Said akiibuka na kudai kuwa kitendo hicho ni jitihada za kumshusha Baraka Mpenga.
Manara amesema kuwa, watu wanaosema anamshusha Mpenja wana chuki zao binafsi na wanataka kumgombanisha na mtangazaji huyo ambaye wanaheshimiana miaka mingi huku akiongeza kuwa, wanaosema hivyo wanamuogopa kwani amebakiza miezi minne tu kumaliza kifungo chake cha TFF kutojihusisha na masuala ya soka.
"Nimefanya dhambi kumsifu Gharib Mzinga? Hata Baraka Mpenja nina asilimia 90 za kumsifu, vipi iwe dhambi kumsifia Gharib? Wakati namsifu Baraka vipi nilikuwa na uhasama na Pascal Kabombe au Hasheem Ibwe? Au nilikuwa namshusha nani, baruani Muhuza ama Charles Hilary?
"Nimeshaandika makala nzuri kuhusu Dickson Job, Diarra, Aziz KI na Pacome Zouazoua kama nimefanya kwa hiyo namchukia Maxi? Hakuna mtu mwenye haki ya kunipangia kumsifia mtu yoyote na Baraka hakuna mtu yoyote aliyemuandika makala kuliko mimi mtandaoni, hakuna.
"Hao wanatafuta trends, Baraka unafanya kazi nzuri, endelea kufanya kazi yako kwa weledi, usikubali kuingizwa kwenye maneno yasiyo na kichwa wala miguu, usiwasikilize watu, kwenye soka maneno yapo tu, hata mimi sijaanza kutukanwa leo," amesema Manara.