Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Man United yamtaka kocha Dortmund

Edin Terzic Kocha wa Borrusia Dortmund Edin Terzic

Sun, 9 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Manchezter United imeripotiwa kuongeza jina jipya kwenye orodha ya makocha inayowataka kwenda kurithi mikoba ya Erik ten Hag.

Siku moja kabla ya Man United kushinda 2-1 dhidi ya Manchester City kwenye fainali ya Kombe la FA, iliripotiwa tajiri mpya wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe atamfuta kazi Ten Hag bila ya kujali matokeo ya Wembley.

Bosi huyo wa kampuni ya INEOS amegoma kumpa sapoti hadharani kocha huyo Mdachi tangu alipokamilisha ununuzi wa klabu hiyo, ambapo atasimamia masuala ya maendeleo ya soka kwenye klabu hiyo.

Mashabiki wa Man United kwa sasa wanasubiri kitu gani kitatokea kwa kocha Ten Hag huku ikielezwa kwamba mabosi wa timu hiyo watafanya uamuzi muda wowote kuanzia sasa.

Licha ya kushinda mataji mawili katika misimu miwili, Ten Hag alishuhudia Man United ikifanya vibaya kwenye Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2023-24.

Kwa mujibu wa gazeti la Bild, Man United sasa imemweka kwenye orodha kocha wa Borussia Dortmund, Edin Terzic, wakihitaji huduma yake baada ya kuiongoza miamba hiyo ya Bundesliga kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Terzic, 41, alizitoa Atletico Madrid na Paris Saint-Germain kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kwenda kuchapwa na Real Madrid 2-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika uwanjani Wembley.

Terzic, aliyekuwa kocha msaidizi wa West Ham United mkataba wake huko Dortmund utafika tamati 2025, lakini kwa sasa kuna mazungumzo ya kuongeza mkataba mwingine, ambao anaweza kusaini kabla ya msimu ujao kuanza.

Licha ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Terzic hakuwa na wakati mzuri kwenye ligi ya ndani na kikosi chake cha Dortmund, ambapo timu hiyo ilimaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa Bundesliga, lakini bado ilipata fursa ya kufuzu mikikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ukimweka kando Terzic, makocha wengine ambao wamekuwa wakihusishwa na Man United ni Thomas Frank, Thomas Tuchel, Gareth Southgate na Mauricio Pochettino.

Ujio wa Terzic utamfanya Jadon Sancho kurudi Man United kwa moyo mmoja bila ya masharti yoyote.

Chanzo: Mwanaspoti