Klabu ya Manchester United imeamua kutompa mkataba wa kudumu kiungo wa kimataifa wa Morocco, Sofyan Amrabat pale uhamisho wake wa mkopo utakapomalizika.
Hiyo ni kutokana na kwamba Man United imefurahishwa na maendeleo mazuri ya kiwango cha kinda Kobbie Mainoo, kwa mujibu wa ripoti.
Man United ilimsajili Amrabat kwa mkopo uliogharimu Pauni 8.6 milioni kwanza, kwa lengo la kumpa mkataba wa kudumu kwani ana kipengele cha kununuliwa kwa Pauni 21 milioni mkopo utakapomalizika.
Hata hivyo, taarifa zimeripoti, Man United haina mpango wa kumsajili katika dirisha la uhamisho la kiangazi, na sasa imepania kumpa nafasi kinda wao mwenye umri wa miaka 18, ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika mechi chache alizocheza hivi karibuni.
Ripoti hiyo inadai zaidi kwamba ingawa klabu hiyo inamchukulia mchezaji huyo wa kimataifa wa Morocco kama kiungo bora, hata hivyo haina uhakika kama anafiti Ligi Kuu.
Naye kocha Erik ten Hag amefurahishwa na kiwango cha Mainoo, anafikiria kumpa majukumu makubwa katika eneo la dimba la kati licha ya umri wake kuwa mdogo.
Mabosi wa Man United wameanza mchakato wa kumtunza mchezaji wao aliyekulia katika kituo chao cha kukuzia vipaji, kwa kuongeza mshahara wake wa kila wiki.
Kwa upande wa Amrabat, tangu alipojiunga usajili uliopita, amecheza mechi 17 katika mashindano yote, ikijumuisha mechi 10 za Ligi Kuu ya England.
Licha ya kucheza nafasi ya kiungo, Amrabat ametumika pia kama beki wa kushoto kutokana na kikosi cha Ten Hag kusheheni wachezaji wengi majeruhi kwenye safu ya ulinzi.
Baada ya mechi mkali dhidi ya Liverpool ambayo waliambulia sare ya 0-0, watashuka dimbani leo dhidi ya West Ham huku wakipania kupata pointi tatu muhimu.