Beki, Sergio Reguilon amerudishwa kwenye klabu yake ya Tottenham Hotspur baada ya mkataba wake wa mkopo huko Manchester United kusitishwa.
Man United ilimsajili beki huyo wa pembeni kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kwa mkataba wa mkopo wa miezi 12 ili kuimarisha safu yao ya ulinzi.
Lakini, staa huyo ameshindwa kumshawishi kocha Erik ten Hag na kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza jambo lililomfanya aanzishwe kwenye mechi saba pekee. Kwa ujumla wake amecheza mechi 12.
Kwa mujibu wa The Athletic, Man United imekifanyia kazi kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wa mchezaji huyo kinachowaruhusu kuvunja, hivyo kusitisha uhamisho huo wa mkopo katikati ya msimu.
Reguilon alisajiliwa ili kuwasaidia Luke Shaw na Tyrell Malacia kwenye beki ya kushoto. Lakini, Shaw amerejea uwanjani na Malacia anakaribia kupona kabisa, hivyo mabosi wa Man United wameona hakuna haja ya kuendelea kubaki na mchezaji huyo kwa kuwa timu imeshatupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Ligi.
Kocha Ten Hag alisema: “Tumefanya uamuzi wa mwisho kuhusu Reguilon. Lakini, wapo pia Spurs waliohusika kwenye majadiliano.”
Spurs kwa sasa ina huduma ya Destiny Udogie na Ben Davies kwenye upande huo wa beki ya kushoto, wakitamba chini ya kocha wao Ange Postecoglou.