Manchester United ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani Old Trafford imefanikiwa kuibana Liverpool na kwenda nayo sare ya mabao 2-2, matokeo yenye faida kubwa kwa Arsenal.
Huu ulikuwa mchezo wa Ligi Kuu England uliokuwa unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka, huku wale wa Arsenal wakihamia upande wa United kwa muda.
Sare hii imeifanya Arsenal iendelee kuongoza ligi ikiwa na pointi 72 sawa na Liverpool lakini yenyewe ikiwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Liverpool ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Luis Diaz katika dakika ya 23, huku United ikisawazisha kupitia kwa Bruno Fernandez katika dakika ya 50 ya mchezo huo uliokuwa na kasi ya hali ya juu.
Kobbie Mainoo aliifungia Man United bao la pili baada ya uzembe wa mabeki wa Liverpool katika dakika ya 67 hali ambayo iliwafanya vijana hao wa kocha Jurgen Klopp kuanza kuliandama lango la Man United kama nyuki na kufanikiwa kusawazisha kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Mohammed Salah dakika ya 84.
United sasa imefikisha pointi 49, katika nafasi ya sita kwenye msimamo zikiwa ni kumi nyuma ya Aston Villa iliyopo nafasi ya nne baada ya kila moja imecheza michezo 31.