Imefichuka. Kumbe Manchester United ilionywa mapema, siku mbili kabla ya kumsajili winga Antony isikubali kulipa pesa nyingi kunasa saini ya Mbrazili huyo, hana hiyo thamani.
Man United ilimsajili Antony kwa ada ya Pauni 86 milioni kutokea Ajax dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka 2022. Tangu wakati huo, staa huyo mwenye umri wa miaka 23, ameshindwa kujipata Old Trafford, akifunga mabao manane na asisti tatu tu katika mechi 55.
Lakini, kabla hawajamsajili, kocha wa zamani wa Uholanzi, Bert van Marwijk aliwaambia mabosi wa Man United hakuna ulazima wa kulipa pesa nyingi. Kwenye kolamu yake katika gazeti la De Telegraaf, lililochapishwa siku chache kabla ya Man United kumsajili Antony kwa pesa nyingi, Van Marwijk aliandika:
“Ajax walifanya vizuri kuchukua Pauni 86 milioni za Man United. Ni kiasi kikubwa sana cha pesa ambacho wasingepata kwenye mauzo ya Antony. Nilisikia akikosolewa tangu yupo Ajax kwamba hawezi kufunga mabao 10 kwa msimu. Kama hafungi Uholanzi, hatakwenda kufunga England.“
Van Marwijk aliwashauri Man United wamsajili Cody Gakpo, ambaye Liverpool walifanya kweli na kunasa saini yake. Winga huyo wa Kidachi, Gakpo amefunga mabao 11 na asisti nne katika mechi 38 alizochezea Liverpool.