Baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1, kutoka kwa majirani zao Manchester City, mashetani wekundu kutoka pale Old Trafford, Manchester United ni kama wamewapa urahisi mahasimu wao hao kwenye harakati za ubingwa.
Man City ambayo kwa ushindi huo imefikisha pointi 62, ikiwa ingepoteza na Arsenal kushinda basi wangeshushwa hadi nafasi ya tatu kwa sababu Arsenal ingefikisha pointi 61 na wao wangekuwa na pointi zao 59.
Ushindi huo umeifanya Man City kuwa nafasi yapili kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Liverpool yenye pointi 63.
Man United ndio ilikuwa yakwanza kupata bao kwenye kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wao Murcus Rashford dakika ya nane, kabla ya Man City kusawazisha kupitia kwa Phil Foden dakika ya 56 na baadae huyo huyo akaongeza bao lapili dakika ya 80 kisha Erling Haaland akamaliza kabisa mechi kwa bao lake la dakika ya 91.
Kipigo hicho kimezidi kuiweka Man United kwenye hatari ya kutoshiriki michuano ya kimataifa kwa msimu ujao kwani hadi sasa inashika nafasi ya sita ikiwa na tofauti ya pointi sita dhidi ya Tottenham iliyo nafasi ya tano.