Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Man United wahamishia majeshi kwa Kudus

Mohammed Kudus Ds Ds.jpeg Mohanmmed Kudus

Sun, 8 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kumkosa Cody Gakpo aliyetimkia Liverpool, Manchester United imeanza kumuwinda nyota wa Ajax, Mohanmmed Kudus ikiamini ataimarisha safu yao ya ushambuliaji.

Inaripotiwa kuwa kocha Erik ten Hag ameanza kuishawishi Ajax aliyowahi kuinoa kabla ya kujiunga na Manchester United iridhie mpango wa timu yake kumnasa nyota huyo wa Ghana mwenye umri wa miaka 22.

Kiwango bora kilichoonyeshwa na Kudus akiwa na kikosi cha Ghana kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Novemba 20 hadi Desemba 18 mwaka jana, kimeonekana kumshawishi kocha Ten Hag ambaye aliwahi kumfundisha nyota huyo kabla ya kuondoka Ajax.

Katika fainali hizo za Kombe la Dunia, Kudus alifunga mabao mawili katika mechi tatu alizoichezea Ghana huku akiteuliwa kuwa mchezaji bora wa mechi mara moja.

Ripoti zinasema kuwa Erik ten Hag ameamua kuhusika moja kwa moja katika harakati za kuishawishi Ajax kuwauzia Kudus akiamini klabu yake hiyo ya zamani itakubali kupunguza dau ililotenga kwa ajili ya kumuuza Kudus akiamini kwamba ni kubwa kuliko uhalisia.

Ajax inatajwa kuwa iko tayari kumuuza Kudus kwa timu yoyote ambayo itakuwa tayari kutoa kitita cha Pauni 40 milioni (Sh 113 bilioni) na sio chini ya hapo, kiasi ambacho Manchester United inaonekana haipo tayari kukitoa kwa ajili ya kumnasa nyota huyo wa Ghana.

Awali, Ajax ilikuwa tayari kumuuza mshambuliaji huyo kwa dau la Pauni 35 milioni (Sh 99 bilioni) lakini baada ya fainali za Kombe la Dunia, wamepandisha ghafla bei yake kutokana na kile ambacho nyota huyo alikifanya Qatar.

Inaonekana Ten Hag anataka kutumia ukaribu wake na klabu hiyo pamoja na Kudus ili kufanikisha mpango wa kumnasa mshambuliaji huyo ambaye ni miongoni mwa nyota wanaozitoa udenda klabu mbalimbali barani Ulaya.

Kocha huyo anaamini kwamba itakuwa rahisi kwa Ajax kuwauzia Kudus ikiwa yeye mwenyewe atahusika katika mazungumzo na timu hiyo kama alivyofanya hapo nyuma kwa usajili wa beki Lisandro Martinez na winga Anthony.

Kilichofanywa na Kudus katika Kombe la Dunia ni muendelezo tu wa makali ya kufumania nyavu ambayo nyota huyo wa Ajax amekuwa nao tangu alipojiunga na timu hiyo 2020.

Kuthibitisha hilo, katika msimu huu, hadi sasa mshambuliaji huyo ameshapachika mabao 10 katika mechi 21 alizoitumikia Ajax huku kati ya mabao hayo, matano amefunga katika mechi 14 za Ligi Kuu ya Uholanzi.

Chanzo: Mwanaspoti