Moja kati ya stori kubwa zilizotikisa vichwa vya habari ilikuwa ni kuhusu Manchester United kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tottenham.
Nahodha wa Mashetani Wekundu, Bruno Fernandez hakuamini kabisa kama timu yao imefungwa kutokana na udhaifu bali ni makosa ya waamuzi ambao walishindwa kuwapa penalti. Bruno alidai kwamba chama cha soka cha waamuzi nchini England kinatakiwa kitoe taarifa ya kuomba msamaha kutokana na tukio hilo.‘
Wiki iliyopita walifanya jambo zuri (kuomba msamaha) baada ya kushindwa kuipa Wolves penalti dhidi yetu nataka kuona wiki watafanya nini, nataka kuona ikiwa watakuja kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kuomba msamaha kama walivyofanya kwa Wolves.”
Baada ya Bruno, kocha wake Erik Ten Hag yeye alilia na safu yao ya ushambuliaji ambapo alidai kuwa ni moja ya sababu za wao kupoteza mechi.
“Umeona kilichotokea, kipindi cha kwanza tulicheza vizuri, lakini hiyo haisaidii inabidi ufunge mabao, ndio maana tumesajili straika, kama kila kitu kitaenda sawa Anthony Martial atarejea kikosini, Rasmus Hojlund naye pia anarejea, hivyo tutakuwa na wachezaji wengi watakaoweza kufunga mabao.”