Manchester United itakabiliwa na vita kali kwenye mchakamchaka wa kunasa saini ya kiungo Sofyan Amrabat baada ya mabingwa wa Italia, Napoli kutangaza nia ya kuhitaji huduma yake.
Amrabat, 27, alikuwa na wakati mzuri uwanjani msimu wa 2022-23, alipoisaidia Fiorentina kufika fainali ya Europa Conference League na kufungwa na West Ham United mchezo uliofanyika mjini Prague.
Amrabat alionyesha ubora mkubwa pia kwenye soka la kimataifa, alipong’ara na Morocco kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar, walipokomea kwenye hatua ya nusu fainali.
Tangu alipotua Fiorentina akitokea Hellas Verona kwenye majira ya kiangazi 2020, kiungo huyo mkabaji amecheza mechi 107 na kufunga bao moja katika kipindi cha miaka mitatu.
Kwa mujibu wa Gazzetta dello Sport, Napoli imeungana na Man United kwenye mbio za kumsajili Amrabat katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, ambalo limebakiza siku chache kufungwa.
Napoli ilinyakua taji la Serie A msimu uliopita ikiwa ni mara ya kwanza kwenye kipindi cha miaka 30, ilipomaliza pointi 16 juu ya timu iliyoshika nafasi ya pili Lazio.
Na sasa ripoti zinadai kwamba Napoli wanahitaji huduma ya Amrabat, dili ambalo litamfanya staa huyo aendelee kubaki kwenye mikikimikiki ya Serie A.
Hata hivyo, kiungo huyo anasubiria ofa ya kutoka Man United kutokana na matamanio yake ya kwenda kucheza kwenye Ligi Kuu England. Liverpool nao waliripotiwa kuhitaji saini ya kiungo huyo.