Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Man United rekodi mbovu zatawala

Man United Loose Man United rekodi mbovu zatawala

Tue, 26 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Klabu ya Manchester United, imeendelea kuweka rekodi chini ya kocha Erik ten Hag, lakini kwa bahati mbaya rekodi hizi sio za kujivunia kabisa.

Mashetani Wekundu wamekuwa na mwendelezo wa matokeo mabovu kufuatia kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya West Ham wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa London Stadium, shukrani kwa mabao ya Jarrod Bowen na Mohammed Kudus yaliyozidi kuipaisha timu ya kocha wa zamani wa United, David Moyes.

Kichapo hicho kimeishusha United hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya Tottenham Hotspur iliyokuwa katika nafasi ya nne.

Timu ya Ten Hag imepoteza mechi 13 katika mashi-ndano yote msimu huu kabla ya Sikukuu ya Krimasi ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo tangu mwaka 1930.

Pia kichapo kutoka kwa West Ham kinakuwa cha 20 kwenye kalenda ya mwaka 2023, kitu ambacho hakijawahi kutokea tangu mwaka 1989.

Kikosi cha Ten Hag pia kimetoka bila ya kufunga bao kwa mechi ya nne mfululizo, hii pia ni mara kwanza tangu mara ya mwisho ilipofanya hivyo 1992 ilipokuwa chini ya Sir Alex Ferguson.

United imeweka rekodi nyingine mbovu ya kucheza dakika 336 bila kufunga bao, cha kushangaza mfungaji wa bao la West Ham, Kudus amecheka na nyavu mara sita zaidi ya washambuliaji wanne wa Mashetani Wekundu msimu huu.

Pia ilikuwa siku mbaya kwa straika Rasmus Hojlund aliyesajiliwa kwa Pauni 72 milioni ambaye bado anasubiri kufunga kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu tangu alipotua.

Fowadi huyo alifanyiwa mabadiliko baada ya dakika 57 dhidi ya West Ham, inamaanisha kwamba amecheza mechi 14 bila ya kufunga mabao wala kutoa asisti.

Tena Hag alikiri wazi kwamba timu yake ipo chini ya kiwango msimu huu baada ya kupoteza mechi ya nane kwenye ligi kufuatia kichapo dhidi ya West Ham.

“Tulitawala mchezo kwa dakika 72 ambazo hatukuweza kuzitumia kufunga. Tulistahili kuongoza bao dhidi ya West Ham. Kwa kipindi hiki timu ipo chini ya kiwango, ukiangalia mechi iliyopita tulitoka sare na moja ya timu kubwa, vijana walikaba vizuri, hatukuweza kufunga. Tulipata nafasi nzuri lakini tukashindwa kutumia, lakini kipindi hiki tunatakiwa kuungana na kuangalia cha kufanya,” alisema Ten Hag.

Kocha huyo pia akasisitiza kuwa Marcus Rashford hakugoma kuwapigia makofi mashabiki waliosafiri hadi London kwa ajili ya kuwasapoti na kuingia moja kwa moja katika vyumba vya kubadilishia nguo akiwa na hasira baada ya kipigo hicho.

Wakati huo huo, mkongwe wa Mashetani Wekundu, Paul Scholes, amesema mbinu za Ten Hag kwenye mechi za ugenini ni za kawaida sana ndo maana matokeo yao yamekuwa sio mazuri.

“Walipata wakati mgumu kwenye mechi za ugenini msimu uliopita, pia imenishangaza unakwenda kucheza mechi ya ugenini ukiwa na kiungo mkabaji mmoja, wengine wote washambuliaji haileti maana yoyote.”

Wakati Man United ikiendelea kuboronga msimu huu, mashabiki wa wameonywa kutokuwa na matumaini kwamba watafanya usajili mkubwa mwezi Januari baada ya ujio wa Sir Jim Ratcliffe.

Inasemekena mwekezaji huyo atatangazwa rasmi mwezi ujao baada ya kufanikiwa kununua hisa kwa asilimia 25 zilizogharimu Pauni 1.25 bilioni.

Pia kutakuwa na mabadiliko ya uongozi kwani, Mtendaji wa Mkuu wa klabu hiyo Richard Arnold anatarajia kuachia ngazi mwisho wa mwezi huu, na mchakato wa kusaka mrithi wake unaendelea.

Chanzo: Mwanaspoti