Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Man United kaa mbali, ikikukuta tu umeumia

Man United Man United kaa mbali, ikikukuta tu umeumia

Mon, 20 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati timu zilizoshika nafasi ya kwanza na yapili zinasua sua, Manchester United imeonyesha kuwa haina utani kwenye harakati za kulisogelea Kombe la Ligi Kuu nchini England baada ya kufanikiwa kuendelea kushinda tu.

Manchester iliibamiza Leicester City kwenye mchezo wa wikiendi iliyopita wa Ligi Kuu nchini humo kipigo cha mabao 3-0 na ikafanikiwa kufikisha alama 49, ikiwa ni baada ya kucheza mechi 24.

Mechi hiyo iliyopigwa pale dimba la Old Trafford ilikuwa ni mechi ya 27 kwa mashetani hao kushinda tangu kuanza kwa msimu na hiyo imeifanya kuwa timu pekee iliyoshinda mechi nyingi kuliko timu nyingine kwenye zile ligi tano bora barani Ulaya.

Murcus Rashford ambaye alifunga mabao mawili kwenye mechi hiyo aliweka rekodi yakuwa mchezaji wakwanza wa timu hiyo kufunga mabao 17 ya michuano yote katika msimu mmoja tangu Wayne Rooney afanye hivyo msimu wa 2011-12 ambapo alifunga mabao 19.

Mbali ya Rashford ambaye alifunga mawili dakika ya 25 na 56, Jadon Sancho aliyeingia akitokea benchi ndio alizimisha kabisa matumaini ya Leicester City baada ya kufunga bao la tatu dakika 61.

Kipigo hicho kimezidi kuiweka Leicester kwenye hali ngumu kwani imeendelea kwani imeendelea kusalia kwenye nafasi ya 14 ikiwa na alama 24 ambazo zinaweza kufikiwa na timu zilizokuwa kwenye hatari ya kushuka daraja, hivyo ikipoteza mechi moja au mbili zijazo huenda ikajikuta kwenye nafasi ya 18 au 19 ambazo ndio zile za mstari mwekundu.

Baada ya mechi hiyo Manchester United itakuwa inajianda na michuano ya Europa League katika mchezo wa hatua ya mtoano kuwania kucheza raundi ya 16 ya michuano hiyo ambapo itakutana na Barcelona Alhamisi ya wiki hii kwenye mechi ya marudiano baada ya ile ya kwanza iliyopigwa kule nchini Hispania kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Leicester itakuwa na wakati mgumu kwenye mechi yao ijayo kwani itakutana na vinara wa ligi, Arsenal February 25, kabla ya kukutana na Southampton machi 4, kisha Chelsea machi 11.

Msimu unaonekana kuwa mzuri zaidi kwa Man United hasa ikiwa nyumbani kwani hadi sasa imeshinda mechi tisa ikiwa kwenye dimba la Old Trafford, mechi mbili ikitoka sare na imefunga moja tu ambayo ilikuwa ni ile ya mwanzo wa msimu ilipopokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Brighton.

Ushindi huu umefanya mbio za ubingwa bado kuendelea kuwa mbili kwa Man United, Man City na Arsenal kwani mmoja kati yao akipata matokeo yasiyoeleweka kwenye mechi mbili tu huenda akashushwa kwenye nafasi aliyokuwepo na kutupwa chini kwani utofauti wa alama ni mdogo.

Kuanzia kwa Arsenal yenyewe ambayo ina kiporo cha mchezo mmoja ikiwa itatoa sare au kupoteza kiporo hicho utofauti wa alama kati yao na Man City utakuwa ni kati ya mbili na tatu na hapo bado ina mchezo mmoja dhidi ya matajiri hao wa Jiji la Manchester.

Upande wa Man United kwa sasa utofauti wa alama dhidi ya Arsenal ni tano nazo ni zinaweza kupungua kwenye mechi mbili tu, vilevile utofauti kati yake na Man City ni alama tatu ambazo ni suala la mechi moja.

Chanzo: Mwanaspoti