Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Man United inatia huruma

Man United Hurumaaaaa Man United inatia huruma

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Erik ten Hag ametetea mbinu zake za kimchezo alizotumia kwenye kipute cha Manchester derby – licha ya chama lake la Manchester United kuandikisha rekodi ya hovyo kabisa kwenye Ligi Kuu England baada ya kuchapwa na mahasimu wao Manchester City uwanjani Etihad, Jumapili.

Kocha huyo Mdachi amefika mbali baada ya kudai anadhani mtindo wake ulikuwa unafanya kazi vyema hadi hapo mastaa wake Marcus Rashford na Jonny Evans walipopata majeraha na kutoka uwanjani.

Rashford alifunga bao la utangulizi dakika ya nane tu ya mchezo baada ya kupiga shuti la umbali wa mita 30 na kuwaduwaza mashabiki waliokuwa wamefurika Etihad.

Baada ya bao hilo, Man United ilionekana kuwa tishio kwa kikosi hicho cha Pep Guardiola na kufanikiwa kwenda mapumziko ikiongoza 1-0, shukrani kwa Erling Haaland aliyekosa bao la wazi.

Phil Foden, aliyepiga mashuti tisa mwenyewe katika mechi hiyo, alisawazisha na kufanya ubao wa matokeo usome 1-1 wakati wachezaji hao wawili wa Man United, Rashford na Evans walipotoka.

Lakini, kilichotisha kwa Man United ni kwamba ilipiga mashuti matatu tu golini mechi nzima, huku bao jingine la Foden na lile la Haaland liliifanya Man City kushinda mechi kwa mabao 3-1.

Bosi huyo wa Old Trafford alisema: “Nafikiri mpango wetu ulikwenda vizuri. Kulikuwa na tofauti ndogo sana. Soka si kumiliki mpira tu. Sawa utahitaji kuwa na mpira ili kufunga mabao. Tulifunga bao zuri sana na dakika 20 za kwanza tulitengeneza nafasi nyingi. Nadhani tulikaba vyema kipindi ambacho hatukuwa na mpira, lakini wakati mzuri haukuwa upande wetu.”

Hata hivyo, takwimu za mchezo huo zinashtua na zinaeleza tofauti kabisa na anachokieleza Ten Hag.

Man United ilipiga mashuti matatu mechi nzima, shuti moja ndilo lililolenga goli ikiwa na maana kwamba ni mara moja tu iliwahi kupiga mashuti machache kwenye mechi tangu Opta ilipoanza kurekodi takwimu za soka mwaka 2003. Hiyo ni wakati ilipopiga mashuti mawili dhidi ya Liverpool, Aprili 2022.

Man United pia imetibua rekodi ya miaka 10 ya kutopoteza mchezo katika mechi 143, ambazo ilikwenda mapumziko ikiwa inaongoza, ambapo ilishinda 123 na sare 20.

Wakati huo, Man City, iliyomiliki mpira kwa asilimia 74, ilipiga mashuti 27 na manane yalilenga goli. Hiyo ina maana, Man City ilipiga mashuti mengi kuliko umiliki wa mpira wa Man United.

Man City pia ilipata kona 15 ukilinganisha na Man United kona mbili, wakati vijana wa Guardiola walipiga pasi 728 na Ten Hag timu yake ilipiga pasi 228.

Akishuhudia Man United ikipoteza mechi ya 11 kwenye Ligi Kuu England msimu huu, mechi mbili zaidi ya msimu uliopita, nahodha wa zamani wa Man United, Roy Keane alisema: “Kitu kimoja kinachotisha zaidi ni unapoifikiria Man United inavyoruhusu mabao ya kutosha na vichapo.”

Keane aliongeza: “Sitaki kuwasema sana Man United kwa sababu Man City walikuwa vizuri. Walionyesha kwanini ni mabingwa. Kitu ambacho Man City inafanya ni kutafuta makosa yako. Wanakufanya ushindwe kupata pa kujificha. Ni kama ulingo wa masumbwi. Tena hapo Haaland na (Kevin) De Bruyne hawakuwa kwenye ubora wao, Foden alisimamia shoo. Nadhani ni kuwapa sifa zaidi Man City kuliko kuwakosoa Man United. Bado kuna maswali mengi kuhusu hii pia na bahati mbaya hata kwa kocha wao pia.”

HIZI TAKWIMU ZA MCHEZO

MAN CITY v MAN UNITED

-Mashuti golini - Man City 8, Man United 1

-Mashuti yote - Man City 27, Man United 3

-Mashuti yaliyozuiwa - Man City 11, Man United 0

-Umiliki mpira - Man City 74%, Man United 26%

-Pasi zote - Man City 792, Man United 288

-Pasi sahihi - Man City 728, Man United 228

-Kupiga takolin - Man City 5, Man United 18

-Kucheza rafu - Man City 5, Man United 10

-Mipira ya kona - Man City 15, Man United 2

Chanzo: Mwanaspoti