Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Man United ilikuwa sahihi kuachana na David de Gea?

Onana D Gea Man United ilikuwa sahihi kuachana na David de Gea?

Tue, 10 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Imeanza kuonekana ni Manchester United imepigwa katika usajili wa kipa wa kimataifa wa Cameroon, Andre Onana ambaye amekuwa na mwanzo mbaya wa maisha yake ya soka huko Old Trafford.

Uhamisho wa Onana wa pauni 47 milioni msimu wa joto kwenda Manchester United kutoka Inter Milan ya Italia ulionekana kuwa unaweza kuleta mapinduzi kwenye kikosi cha Erik ten Hag.

Ilikuwa ni mara ya kwanza tangu enzi za Sir Alex Ferguson ambapo Mashetani Wekundu walimsajili mchezaji anayechukuliwa kuwa bora zaidi kwa wakati huo katika nafasi yake.

United ilishinda Kombe la Carabao na kumaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi wakati wa msimu wa kwanza wa kufurahisha wa Ten Hag huku kwa De Gea huo ukiwa mwisho wake Old Trafford. Kocha huyo hakuonekana kuwa na mpango na kipa huyo na badala yake alimwona Onana kama kipa ambaye anaweza kutekeleza vyema kile ambacho alikuwa akikihitaji kutokana na kuwa kwake na uwezo mzuri wa kuanzisha mashambulizi.

Lakini miezi mitatu tu ya maisha ya kipa huyo wa Cameroon, imewafanya mashabiki wa timu hiyo kumkumbuka De Gea namna ambavyo alikuwa kizingiti kwa kuokoa michomo mingi ya hatari.

Onana ameruhusu mabao 18 katika mechi 10 za kwanza za Mashetani Wekundu katika mashindano yote msimu huu, na wamepoteza sita kati ya hizo.

Kikosi cha Ten Hag kimeporomoka hadi nafasi ya 10 kwenye Ligi Kuu ya England, na baada ya kichapo cha kushangaza cha mabao 3-2 kutoka kwa Galatasaray kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, kina kibarua kikali mbele yao kutinga hatua ya mtoano barani Ulaya kwenye Ligi ya Mabingwa.

Bila kujali kiwango cha wapinzani, United wanafunguliwa wapendavyo, na Onana hafanyi vya kutosha kama safu ya mwisho ya ulinzi.

Hakuna shaka kuwa Onana amekuwa na wakati mgumu akiwa na jezi ya United hadi sasa, na hilo limepelekea idadi kubwa ya mashabiki kuishutumu klabu hiyo kwenye mitandao ya kijamii kwa kushindwa kumpa De Gea mkataba mpya. Mhispania huyo alikua mtu maarufu katika kipindi cha miaka 12 ya uchezaji wake Old Trafford, na alishinda tuzo ya Ligi ya England ya Golden Glove mara mbili, pamoja na tuzo nyingi za Mchezaji Bora wa Mwaka wa Wachezaji wa Ndani.

Lakini United ilipoanza ukame wa miaka mitano kati ya 2017 na 2022, De Gea alikuwa na hatia ya makosa mengi katika kipindi hicho. Katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona msimu wa 2018-19, alimzawadia Lionel Messi bao lake la pili katika mchezo huo huku United wakipoteza kwa jumla ya mabao 4-0.

Chelsea iliishinda United 3-1 katika nusu-fainali ya Kombe la FA msimu uliofuata baada ya De Gea kumwachia Oliver Giroud aliyekuwa karibu na nguzo kumpita na kushindwa kudaka shuti kali la Mason Mount na kutinga wavuni. Aliigharimu United pointi za thamani kwenye Ligi mara kwa mara pia, akiruhusu mabao ya kawaida dhidi ya Arsenal, Watford na Everton.

Kushuka kwa kiwango cha De Gea kuliendelea hadi katika msimu wake wa mwisho. Kabla ya uamuzi wa kuamua kuchana na De Gea, United ilipaswa kumleta Onana huku ikiendelea kusalia na kipa huyo huenda changamoto ya namba ingemfanya kuwa bora zaidi na kuwa msaada kipindi hiki.

Chanzo: Mwanaspoti