Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Man United hakuna namna

Harry Maguire Ajishtukia Manchester United Harry Maguire

Sun, 7 May 2023 Chanzo: mwanaspoti

Hakuna namna. Erik ten Hag atalazimika kupiga bei mastaa kibao ili anase wakati wapya kwenye dirisha lijalo.

Hilo linakuja baada ya Manchester United kutokuwa na uhakika wa ishu yake ya kupigwa bei itakuwaje.

Wamiliki wa klabu hiyo, familia ya Glazer wapo kwenye mchakato wa kuipiga bei Man United, mkwanja ambao utavunja rekodi ya dunia ya Pauni 6 bilioni baada ya kuimiliki timu hiyo kwa miaka 18.

Wamepokea ofa mpya kutoka kwa mfanyabiashara Mwingereza, Sir Jim Ratcliffe na tajiri wa Qatar, Sheikh Jassim na sasa kinachosubiriwa ni mchakato utakavyokuwa kuona nani atashinda vita hiyo ya kuimiliki Man United.

Lakini, ripoti zinadai kwamba kocha Ten Hag kwa sasa bajeti yake ya usajili ni Pauni 100 milioni bila ya kujali kitakachotokea kwenye mchakato wa mauzo ya klabu hiyo na kuwa chini ya umiliki mpya.

Kinachoelezwa ni kwamba Man United kwa sasa haitakuwa na matumizi makubwa kwenye usajili kutokana na taratibu za Financial Fair Play. Na kocha Ten Hag hataki kuficha kwamba mpango wake ni kuleta wakali kadhaa wa kiwango cha dunia kwenye kikosi chake ili kuwa na timu itakayokuwa na uwezo wa kushindana kuwania mataji.

Lakini, sasa atalazimika kupiga bei mastaa kibao kama anataka kuboresha bajeti yake ya usajili awe na nguvu kubwa sokoni. Kama hatauza, basi Man United itakuwa na uwezo wa kufanya usajili mmoja tu mkubwa kwa bajeti yao.

Man United inasaka kipa mpya baada ya sasa kuwa kwenye mashaka makubwa juu ya David De Gea, ambaye mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na bado hakuna dili jipya lililofikiwa makubaliano ya kusaini.

Kocha Ten Hag anahitaji pia straika mpya, kiungo mpya na winga mpya. Lakini, kama hakutakuwa wamepatikana wanunuzi wa wachezaji kama Harry Maguire na Donny van de Beek, Ten Hag atalazimika kubaki na bajeti yake ya Pauni 100 milioni kwenye usajili wa dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Alipoulizwa kuhusu pesa atakazokabidhiwa endapo Man United itauzwa, Ten Hag alisema: “Sina nguvu kwenye hilo na pia sifahamu. Kitu ambacho nafahamu ni kwamba Man United ni moja ya klabu kubwa kabisa na mengine ni moja kati ya klabu mbili kubwa zenye mashabiki wengi duniani.

“Ila sidhani kama klabu inashindana kwenye michuano mikubwa duniani, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England. Lakini, kwenye soka la kisasa nunahitaji kuwa na pesa kutengeneza timu. Viwango vya wachezaji wako ndivyo vitakavyoamua ufanikiwe au ufeli. Kila mtu anafahamu tunahitaji pesa kutengeneza kikosi. Wachezaji wa viwango vikubwa wana gharama kubwa sana.

“Huu ni mpango wetu. Mpango ni wa usajili, ubaborsha timu kwa kuleta wachezaji unaowahitaji na kuondoa wengine ambao huna kazi nao ili kufanya kikosi kuwa kwenye uwiano mzuri wa kuwa na wachezaji wazoefu na vijana. Lakini, mwisho wa yote tunataka tuwepo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, tunataka tupambane huko na kuwatupa watu nje, twende katika mwendo huo.”

Ten Hag anahitaji mastaa kama Harry Kane, Victor Osimhen, Declan Rice na wengine kibao, ambao wote hao kunasa saini zao, unahitaji kuwa na mkwanja mrefu. Asipouza mastaa ambao hawataki Old Trafford itakuwa ngumu kuwanasa wote anaowataka kwa bajeti ya Pauni 100 milioni.

Chanzo: mwanaspoti