Jeuri ya pesa. Manchester United imewafunika majirani zao Manchester City kwenye ishu za matumizi ya pesa kwa miaka michache iliyopita huku kocha Mhispaniola Pep Guardiola akiwacheka chinichini.
Bosi huyo wa Man City, Guardiola bila ya shaka atakuwa anawapiga kijembe Man United kwa uwekezaji mkubwa kwenye mambo ya usajili na kitu pekee ambacho Mashetani Wekundu wamepata ndani ya muda huo ni Kombe la Ligi tu.
Man United iliichapa Newcastle United uwanjani Wembley, Jumapili iliyopita na kushinda taji lao la kwanza tangu mwaka 2017, na Guardiola alisema ni suala la muda tu kabla ya klabu hiyo ya Old Trafford kuanza kuwa washindani tena kutokana na pesa walizotumia kwenye kuboresha kikosi chao.
Tangu Guardiola achukue mikoba ya kuinoa Man City, 2016 Man United imetumia Pauni 1.077 bilioni kwenye usajili, ikiwazidi kidogo sana Man City, ambao wametumia Pauni 1.074 bilioni.
Lakini, Man City kwenye pesa taslimu iliyotumia ni Pauni 478 milioni tu, kwa sababu ilivuna pesa nyingi kwa kuuza wakali wake akiwamo Raheem Sterling, Gabriel Jesus na Oleksandr Zinchenko kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi. Man United wao wametumia Pauni 835 milioni taslimu kwa kipindi cha miaka saba katika dirisha la usajili kwa maana ya pesa walizolipa kununua mastaa wapya ukitoa zile walizopata kwenye mauzo ya wachezaji wao.
Guardiola anaamini kwamba klabu hizo mbili sasa zimeanza kuonyesha ubora ndani ya uwanja baada ya kuwaona Man United wakifanya kile walichofanya Wembley, Jumapili iliyopita.
Guardiola alisema: “Nawapongeza Man United kwa kushinda Carabao Cup. Ingewezekana tu kama si sasa basi baadaye, sivyo? Karibuni vitani. Man Unitd wanapaswa kuwapo hapo. Wapo kwenye nafasi yao wanayostahili kuwa. Ukweli ni kwamba hizi timu mbili, Liverpool na sisi Man City, tumefanya vya kutosha ukizingatia kwenye ishu ya takwimu. Nao sasa wamekuja.”
Alipoulizwa kama Man United sasa ni mahasimu wao wakubwa, Guardiola alisema huku akiwa ana tabasamu: “Pengine. Kama wataendelea kutumia pesa tena kidogo, inawezekana. Nilipokuja hapa, siku zote nilitambua Man United wapo, historia yao na kila kitu na sasa Erik ten Hag anafanya kazi nzuri. Na wachezaji nao wamekuwa wakijitolea, wanafanya kazi kwa pamoja na kujaribu kumaliza huu ukame wa miaka mitano au sita ya kutoshinda ubingwa wowote.”
Kuhusu matumizi ya pesa, Man United ilitumia mkwanja mrefu kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, ilipolipa Pauni 200 milioni kuwasajili Antony, Lisandro Martinez na Casemiro.
Uhamisho mwingine wa pesa nyingi uliofanyika tangu mwaka 2016 uliwahusisha pia Jadon Sancho, Harry Maguire na Romelu Lukaku, ambao wakali hao kila mmoja aliwagharimu Pauni 80 milioni.
Paul Pogba, ambaye alijiunga na timu hiyo msimu wa 2016/17 anaendelea kubaki mchezaji ghali wa muda wote wa Man United wakati saini yake iliponaswa kwa Pauni 89 milioni akitokea Juventus.
Kwa upande wa Man City, usajili wao ghali ni ule wa Jack Grealish, ambaye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kwenye Ligi Kuu England kusajiliwa kwa Pauni 100 milioni wakati alipohama kutoka Aston Villa kwenda Etihad mwaka 2021.
Erling Haaland, Ruben Dias, Joao Cancelo na Riyad Mahrez ni masta wengine wachache waliosajiliwa kwa pesa nyingi kwenye klabu hiyo ya Man City katika kipindi ambacho kocha Guardiola amekuwa akifanya kazi Etihad.
MATUMIZI YA MAN CITY NA MAN UNITED KWENYE USAJILI TANGU 2016
Man City - usajili, Pauni 1.074bilioni
-Man United - usajili, Pauni 1.077bilioni
-Man City - kuuza, Pauni 596 milioni
-Man United - kuuza, Pauni 242 milioni
-Man City - matumizi kamili, Pauni 478milioni
-Man United - matumizi kamili, Pauni 835milioni