Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo sita yatakayomkwamisha Ten Hag msimu huu

Rashford Vs Ten Hag Mambo sita yatakayomkwamisha Ten Hag msimu huu

Sun, 27 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Manchester United imefunga bao moja tu katika ufunguzi wa Ligi Kuu England ambalo limewekwa kimiani na beki wa kati Raphael Varane kwa hiyo inatakiwa kuimarika katika safu ya ushambuliaji katika mechi nyingine zinazofuata.

Man United ina historia nzuri ya kuanza msimu kwa kasi na kufunga mabao mengi lakini imekuwa tofauti katika misimu miwili chini ya kocha Erik ten Hag.

Msimu wa 2021-2022 ilianza ligi kwa kishindo kwa kuichapa Leeds United mabao 5-1, msimu wa 2019-2020 iliwachapa Chelsea mabao 4-0 siku ya ufunguzi wa ligi. Katika msimu wa kwanza wa Jose Mourinho walifunga mabao matano katika mechi zao mbili za kwanza.

Katika misimu miwili chini ya Ten Hag wamefunga bao moja tu katika mechi mbili za kwanza. Baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wolves, Man United ilichezea kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Tottenham Hotspur.

Ikumbukwe katika msimu wa kwanza wa Mdachi huyo Man United ilipokea kichapo cha mabao 4-0 dhidi ya Brighton kisha kufungwa mabao 2-1 dhidi Brentford katika mchezo unaofuata. Lakini Man United iliimarika zaidi na kuifunga Liverpool mabao 2-1 katika mechi ya tatu ya msimu uliopita huku ikionyesha kiwango bora.

Malengo ya Ten Hag yalikuwa ni kurekebisha eneo la safu ya ushambuliaji kwa kufanya usajili wa straika ndio maana akamsajili Rasmus Hojlund kwa Pauni 72 milioni kutoka Atalanta.

Licha ya kutumia Pauni 165 milioni katika usajili huu wa kiangazi bado kikosi cha Ten Hag kimeonekana kuwa butu hususani katika safu ya ushambuliaji. Haya hapa mambo sita yanayoweza kuwa kikwazo kwa Man United msimu huu wa 2023-2024.

USHAMBULIAJI BUTU

Rasmus Hojlund alisajiliwa kwa mkwanja mrefu akitokea Atalanta lakini vipimo vyake viligundulika ana matatizo ya mgongo tangu alipokuwa huko kwa hiyo Ten Hag akashauri apewe muda zaidi kabla ya kuanza kupiga mzigo uwanjani.

Awali, ilidhaniwa straika huyo mwenye umri wa miaka 20 angekuwa suluhisho la matatizo ya Man United katika safu ya ushambuliaji matokeo yake alikosa mechi mbili za Ligi Kuu England dhidi ya Wolves na Tottenham huku wakiwa na matumaini ya kwamba atarejea dimbani hivi karibuni kabla ya mechi dhidi ya Arsenal itakayochezwa Septemba 3.

Msimu uliopita Man United ilianza msimu bila ya kuwa na mshambuliaji sahihi huku Anthony Martial akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, bila kumsahau Cristiano Ronaldo ambaye alikuwa katika mgogoro na klabu hatimaye akaondoka. Hapo ndipo Ten Hag akafanya uamuzi wa kumsajili Wout Weghorst kwa mkopo kutoka Burnley, hata hivyo, hakukidhi mahitaji ya timu.

RASHFORD KUWA NA.9

Kutokana na Hojlund kuwa majeruhi Rashford amelazimika kucheza kama namba tisa nafasi ambayo anaichukia. Fowadi huyo aliweka wazi kwamba anafurahia zaidi kucheza akitokea pembeni, kauli ambayo aliisema kupitia kipindi cha Overlap kinachotangazwa na Garry Neville.

Katika mechi mbili za ligi zilizopita alipata tabu kwa hiyo Ten Hag ana kazi kubwa ya kufanya labda Hojlund arejee kikosini endapo atakuwa fiti hapo ndipo mfumo ubadilike. Msimu uliopita nyota huyo wa kimataifa wa England alikuwa na mchango mkubwa, alimaliza msimu akiwa amefunga mabao 30 na akaisaidia timu yake kufuzu michuano ya Ligi Mabingwa Ulaya.

MAWINGA WANAZINGUA

United imekuwa maarufu kwa uchezaji wao wa kuvutia wa kutumia mawinga kama Ryan Giggs, Cristiano Ronaldo enzi hizo. Antony bado ana mengi ya kujifunza na kuwashawishi mashabiki baada ya kusajiliwa kwa Pauni 85 milioni kutoka Ajax.

Winga huyo huyo hakuanza vizuri msimu huu na alikuwa na mchango katika mechi mbili za ligi zilizopita dhidi ya Wolves na Tottenham. Mwingine ni kinda wa timu hiyo Alejandro Garnacho ambaye aling’ara msimu uliopita pia alikatisha tamaa kwa kuonyesha kiwango kibovu.

Kwa upande wa Jadon Sancho anastahili kuanza badala ya kinda huyo katika mchezo wa leo dhidi ya Nottingham Forest badala ya kumweka benchi. Hata hivyo Winga huyo amepoteza kujiamini kwake kutokana na timu hiyo kusuasua tangu alipotua akitokea Borussia Dortmund kwa Pauni 74 milioni.

KUPOTEZA NAFASI ZA KUFUNGA

Ingawa United haijacheza vizuri katika mechi zake mbili za mwanzo, angalau ilitengeza nafasi za kufunga na kuashiria kwamba tatizo ambalo linaitafuna timu hiyo kwa sasa ni straika.

Katika mchezo dhidi ya Tottenham, United ilipiga mashuti 14 katika kipindi cha kwanza ikiwa ugenini kwa mara tangu mwaka 2008 ilipocheza dhidi ya Blackburn na kipindi hiki Man United ilikuwa ndio bingwa mtetezezi wa ligi.

Rashford na Antony walipoteza nafasi nyingi za kufungua katika mchezo wao uliopita dhidi ya Spurs lakini zigo lingine la lawama likamwangukia Bruno Fernandes ambaye alipoteza nafasi ya wazi zaidi ya kufunga kwa kichwa baada ya kuwekewa krosi na Luke Shaw. Baada ya mchezo huyo Ten Hag akasisitiza umuhimu wa kufunga bao la kwanza katika ligi.

MOUNT KUTUMIKA KIUNGO WA ULINZI

Ten Hag alipomsajili Mount kutoka Chelsea mashabiki walipinga sana wakidai uhamisho huo hautakuwa na manufaa katika timu. Lakini Mholanzi huyo akasisitiza kwamba kiungo huyo ataleta ubunifu katika safu ya kiungo msimu huu ndio maana alisamjili.

Lakini baada ya kucheza mbili za ligi kiungo huyo alipata tabu na kushindwa kutoa mchango kwa timu yake. Mount hakuonyesha kiwango kizuri pia katika mechi za maandalizi ya msimu kwani alitumika kiungo cha chini nafasi ambayo hakuwahi kuicheza wakati alipokuwa Chelsea.

Katika mechi dhidi ya Spurs kiungo hiyo aligusa mpira mara 26 tu na kupiga pasi 14 tu zilizowafikia walengwa, takwimu ambazo ni mbovu zaidi ya wachezaji 11 walioanza kikosi cha kwanza katika mchezo huo.

BAADHI WAMECHOKA

Katika mechi za mwanzo wa msimu wa ligi baadhi wachezaji wa Man United walionekana kuchoka sana akiwamo Casemiro.

Ziara za mechi ya maandalizi ya msimu hazikuwasaidia licha ya kucheza mechi nane za kirafiki ndani ya siku 25 katika nchi tano tofauti. Vijana wa Ten Hag walipokuwa katika ziara Marekani walitembelea miji mbalimbali kama San Diego, Houston kabla ya kumalizia Las Vegas.

Ingawa ziara hizi zina thamani kubwa kibiashara kwa United, lengo kuu kabla ya msimu mpya ni kuwatayarisha wachezaji kwa kucheza mechi za ushindani lakini ziara hiyo imekuwa na matokeo tofauti.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live