Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo ni magumu zaidi kwa Simba, Yanga

Simba X Yanga 1 Mambo ni magumu zaidi kwa Simba, Yanga

Mon, 4 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Gazeti la Mwananchi jana Jumapili limeripoti katika ukurasa wake wa michezo wa nyuma kwamba “Simba, Yanga mambo magumu Afrika”, likizungumzia matokeo ya mechi mbili za kwanza za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Wakati Simba imeambulia pointi mbili katika mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana na Asec Mimosas ya Ivory Coast zote zikiisha kwa sare, Yanga imejikuta ikiondoka na pointi moja tu katika mechi mbili baada ya kufungwa mabao 3-0 na CR Belouizdad ya Algeria na kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Al Ahly ya Misri kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba inashika nafasi ya tatu kwenye Kundi B, huku Yanga ikiburuta mkia wa Kundi D.

Imekuwa ni kawaida kwa mashabiki na viongozi kutegemea ushindi wakati timu zinapocheza nyumbani na hivyo kuutumia kusonga mbele mashindanoni, ndio maana maofisa habari wamekuwa wakizungumzia kirahisi kuzifunga hata timu kubwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Lakini mechi mbili zilizochezwa msimu huu hazijaweza kutoa matokeo hayo, huku Yanga ikiponea chupuchupu kuondoka mikono mitupu kwa vigogo wa soka barani Afrika, Ahly juzi Jumamosi usiku.

Kama Mwananchi ilivyoandika, hali ni ngumu kwa Simba na Yanga kwenye michuano ya Afrika mwaka huu, ingawa kumekuwa na utetezi kuwa hata mwaka jana Simba ilianza kwa vipigo viwili nyumbani na ugenini, lakini ikaja kuzinduka na kupata matokeo mazuri mechi zilizofuata hadi ikavuka kwa kishindo kwenda robo fainali.

Historia haichezi uwanjani na vilevile inaweza kutumiwa na wapinzani kujiweka vizuri zaidi dhidi ya Simba katika mechi zinazofuata endapo wataamini kuwa vigogo hao wa Tanzania huzinduka katika mechi za mwisho na hivyo kujipanga vizuri zaidi kuzuia isizinduke kama kawaida yake.

Mechi dhidi ya Al Ahly, Asec Mimosas, Jwaneng Galaxy na Belouizdad zinaweza kukupa picha kuwa wawakilishi wetu walikutana na timu bora, hivyo walistahili matokeo waliyopata, lakini soka linabadilika Afrika na hivyo uwezekano wa kukutana na timu dhaifu unazidi unakuwa finyu zaidi.

Ukanda wa Kusini mwa Afrika, ambako zinatoka timu za Galaxy, Mamelodi Sundowns, Petro de Luanda umekuwa ukizidi kuimarika siku hadi siku na kuzalisha timu mpya na bora. Petro si mgeni katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, wakati Galaxy wamefikia tena hatua hiyo baada ya kuwashangaza Watanzania kwenye Uwanja wa Mkapa walipogeuza kipigo cha mabao 2-0 walichopewa nyumbani na Simba na kuwa ushindi wa 3-1 Kwa Mkapa uliowawezesha kusonga mbele kwa sheria ya bao la ugenini, wakienda kinyume na kaulimbiu ya “Kwa Mkapa Hatoki Mtu”.

Ikiwa imezaliwa mwaka 2015, Jwaneng Galaxy, kama zilivyo timu nyingi za ukanda wa Kusini mwa Afrika, inanufaika na programu nyingi za nchi na za umoja wa ukanda huo, maarufu kwa jina la Cosafa, wa kukuza vipaji na maendeleo ya soka kwa ujumla.

Sikuona ajabu wakati Lesotho, timu nyingine kutoka ukanda huo, ilipoilazimisha Nigeria kwenda sare ugenini na baadaye Zimbabwe kulazimisha matokeo kama hayo kwa Nigeria na Comoro kuilaza Ghana kwa bao 1-0 nyumbani, matokeo ambayo yasingetarajiwa kutoka nchi ambayo imekuwa begi la mazoezi kwa nchi za Afrika Mashariki.

Yapo matokeo mengine mazuri kwa timu za ukanda huo katika michuano ya awali ya Kombe la Dunia yanayoonyesha ubabe wa soka Afrika unaanza kuwa na uwiano ambao ilani tosha kwa timu zetu katika michuano ya Afrika.

Kwa sababu kanuni za ligi za nchi hizo haziruhusu idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni kama huku tunakoruhusu wachezaji 12 wakiweza kuingia uwanjani, ni dhahiri kuwa matokeo ya timu zao za taifa yanaakisi kiwango cha soka cha ndani, au kwa maana nyingine cha klabu zao.

Katika mechi mbili ambazo Botswana imecheza za michuano ya awali ya Kombe la Dunia, imepoteza moja nyumbani dhidi ya Msumbiji na kuilaza Guinea. Kwanini Jwaneng Galaxy isiwe tishio?

Kuna nchi kama Djibouti, ambayo haijaweza kuwa na uwakilishi katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, inaendelea kupiga hatua kwa hatua kupandisha soka lake. Kitendo cha kukaribisha wanasoka wastaafu soka barani Ulaya, kama Alex Song, kuja Djibouti, si tu kumalizia soka lao, bali kuongoza programu za watoto, kinaonyesha sababu ya klabu za nchi hiyo kuanza kuwa ngumu tofauti na ilivyozoeleka.

Kwa hiyo, ingawa bado timu za Afrika Kaskazini zinatawala michuano ya klabu Afrika, kuna mabadiliko makubwa yanakuja kutoka nchi za kanda nyingine, Kusini ikiwa mojawapo, ikiongozwa na Mamelodi Sundowns iliyotwaa ubingwa wa Afrika na sasa ikiwa ni wababe wa michuano mipya ya Ligi ya Soka Afrika (African Football League), njiani wakiwa wameziondoa timu mbili za Afrika Kaskazini.

Afrika Magharibi ilikuwa na timu bora za taifa kutokana na wachezaji wake wengi kwenda Ulaya au kukulia Ulaya, lakini haikuwa ikitamba katika ngazi ya klabu. Timu kama Enyimba ikiwa klabu ya kwanza ya Nigeria kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa. Hata hivyo, programu za watoto na vijana zimeibua klabu mpya na ambazo zinapiga hatua taratibu barani humu.

Asec Mimosas inaongoza kwa timu za ukanda huo kuzalisha vipaji na kujenga timu imara za vijana. Vituo kama hivyo vimejaa nchini Ghana, ingawa bado hakujajengwa klabu imara za kutetemesha Afrika.

Kwa kifupi, maendeleo ya soka yanazidi kutapakaa kwa nchi ambazo zimezinduka kiakili na tulichokiona katika raundi mbili za kwanza ni matokeo ya kuwa au kutokuwa na program imara za maendeleo, ubora wetu ukitegemea zaidi wageni ambao pia ni vigumu kuwapata wale wazuri kutokana na uwezo wa kiuchumi wa klabu zetu.

Ingawa wawakilishi wetu wanaweza kubadili mwelekeo huko mbele, lakini somo kubwa ni kwamba kuna ugumu zaidi ya kukutana na Al Ahly, Belouizdad, Wydad Casablanca, Raja, Zamalek au Pyramids.

Sasa hata Galaxy, Petro de Luanda, Asec Mimosas, Mamelodi Sundowns au Medeama si timu rahisi kama ilivyokuwa huko awali.

Na si ugumu wa kukutana na timu kutoka nje ya ukanda wa kaskazini, hata ule wepesi wa kupata hizo pointi tisa tunaojiapiza Kwa Mkapa haupo tena. Kwanza pointi tisa zimeshatibuka na kubakia sita tu.

Soka sasa si la kutegemea uwanja wa nyumbani wala urahisi kwa nchi zisizo za Kiarabu. Hata Waarabu sasa wanacheza ugenini kutafuta ushindi au sare tofauti na ilivyokuwa zamani.

Mambo ni magumu kuliko tunavyofikiria na mechi za mwisho za mzunguko wa kwanza zitathibitisha kwamba soka la Afrika linazidi kubadilika kutoka ule wepesi wa kucheza nyumbani au kucheza na timu zinazodhaniwa kuwa ni vibonde hadi kupambana kwa nguvu zote katika kila mechi.

Kumalizia mzunguko wa kwanza, Simba itakutana na Wydad, wakati Yanga itakutana na Medeama. Mechi hizo mbili zitatoa picha ya mwelekeo wa wawakilishi wetu Afrika, lakini ugumu uko palepale na hivyo kunahitajika jitihada kubwa kuhakikisha ugumu huo unalainishwa ili tunuse tena robo fainali na ikiwezekana nusu, na Mungu akiruhusu basi iwe fainali.

Chanzo: Mwanaspoti