Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo matano ya kumbeba Okrah Yanga

Okrah Amevunjika Pua Mambo matano ya kumbeba Okrah Yanga

Fri, 5 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Usajili wa kiungo mshambuliaji, Augustine Okrah kutoka Bechem United FC ya kwao Ghana kwenda Yanga umezua majadala kwa wadau wa soka huku wengine wakiubeza kwa kusema unaweza usiwe na jipya maana mchezaji huyo alishindwa kuonyesha makali yake akiwa na Simba ambayo aliitumikia miezi saba iliyopita.

Hii itakuwa awamu ya pili kwa Okrah kucheza Ligi Kuu Bara, awamu ya kwanza alitua Bongo Julai 13, 2022 huku akibeba matumaini makubwa kwa mashabiki wa Simba kutokana na kile ambacho alikifanya akiwa Ghana lakini mambo yakawa tofauti na badala yake alijikuta akipewa mkono wa kwakheri ‘Thank You’ Msimbazi.

Okrah ambaye yupo Zanzibar na timu yake mpya, amerejea Tanzania akiwa katika mazingira yaleyale ya awali kwani ni kati ya wachezaji hatari ambao wanaongelewa Ghana, nini kipya ambacho atakionyesha? Hilo linaweza kuwa swali ambalo litakuwa vichwani mwa wengi ambao wanasubiri kwa hamu kumshuhudia.

Kutua kwa Okrah kunamfanya Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi kupumua kutokana na uhitaji ambao alikuwa nao wa mchezaji mpya ambaye anaweza kuongeza nguvu kwenye safu yake ya ushambuliaji, kilichopo ni kwa namna gani mchezaji huyo ataonyesha viongozi wa Yanga hawakufanya makosa kumrejesha Tanzania.

Kulingana na dodoso mbalimbali haya ni mambo matano ambayo yanaweza kumbeba Okrah akiwa na Yanga ambayo mbali na kuwa na jukumu la kutetea ubingwa wa ligi, ina kiburua cha kuvuka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

UZOEFU BONGO

Pamoja na kwamba hakutumika kwa kipindi kirefu kwenye kikosi cha Simba, Okrah anajua ushindani uliopo kwenye soka la Tanzania jambo ambalo atakuwa akipambana nalo ni kuzoeana tu wachezaji wenzake kwenye kikosi hicho.

Kujua kwake aina ya soka la Tanzania inaweza kuwa moja kati ya silaha muhimu kwa nyota huyo kufanya vizuri kwenye kikosi cha Yanga, wapo wachezaji ambao waliingia moja kwa moja kwenye vikosi vyao vipya na kufanya vizuri lakini wengine walihitaji muda wa kuzoea ligi kabla ya kuwa moto wa kuotea mbali.

Mfano mzuri ni mshambuliaji wa Simba, Jean Baleke ambaye alipotua tu alikuwa msaada kwa wekundu hao wa Msimbazi ambao kwa kipindi hicho walikuwa na pigo la kuumia kwa aliyekuwa kinara wa mabao kwenye kikosi hicho, Moses Phiri.

Mchezaji ambaye alishindwa kuonyesha makali yake ndani ya msimu wake wa kwanza ni Stephane Aziz Ki ambaye kwa sasa ni kama gari ndio limewaka, hivyo  uzoefu ambao aliupata Okrah wa kucheza Ligi Kuu Bara akiwa na Simba unaweza kumbeba.

KIU YA KUONYESHA

Shauku ya Okrah kutaka kuthibitisha ubora wake akiwa na Yanga inaweza kuwa moja ya sababu ambayo itachochea mchezaji huyo kufanya makubwa.

Licha ya kwamba alitua nchini akiwa mmoja wa wachezaji bora kabisa kwenye ligi ya Ghana, alishindwa kuonyesha ubora wake kwenye kikosi cha Simba kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kusumbuliwa na majeraha japokuwa alikuwa pia akitajwa kuwa ni mtovu wa nidhamu jambo ambalo lilimfanya asiwe na maisha marefu Msimbazi.

Bila shaka Okrah atataka kuonyesha kuwa Yanga haikufanya makosa kumrejesha tena nchini, hivyo hiyo itakuwa chachu ya kuona kilichobora kutoka kwake.

UBORA WA KIKOSI

Muda mwingine ubora wa kikosi unaweza kumbeba mchezaji na kuwa katika daraja lingine tofauti kabisa na vile ambavyo alikuwa akitazamiwa.

Ukiitazama Yanga inaonekana kuwa ni timu iliyokamilika kwenye kila idara ni upungufu ni mchache sana ambao umekuwa ukionekana kwenye kikosi chao ukilinganisha na timu nyingine ndio maana msimu uliopita ilitwaa ubingwa wa ligi, Kombe la ASFC, Ngao ya Jamii na hata upande wa kimataifa ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kama hayo hayatoshi msimu huu imeonakana kuwa kwenye moto uleule licha ya kupoteza kwenye Ngao ya Jamii, ipo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ipo kwenye nafasi ya kutetea ubingwa wa ligi na Kombe la ASFC.

Ubora wa mchezaji mmoja mmoja kwenye kikosi cha Yanga ni mkubwa na hata timu kwa ujumla, hivyo Okrah anaweza kubebwa na hilo na kujikuta akifanya vizuri.

UBORA WAKE 

Okrah anaweza kubebwa na uwezo wake wa kucheza katika maeneo yote ya ushambuliaji, ni mzuri akishambulia akitokea pembeni, kulia au kushoto lakini pia ana uwezo wa kucheza kama namba 10 yaani nyuma ya mshambuliaji wa mwisho.

Hakuna ubishi kuwa utatu wa Yanga, Maxi Nzengeli, Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoa umebamba kwelikweli lakini ujio wa Okrah utatoa machaguo zaidi kwa Kocha Miguel Gamondi hasa mmoja kati ya hao anapopata majeraha au kushindwa kutekeleza vyema majukumu yake.

Akimuongelea Okrah katika moja ya mahojiano yake na gazeti hilo, kocha Gamondi alisema, “Sihitaji kuzungumza mambo mengi sasa kuhusu mchezaji huyo, nitampa nafasi aonyeshe ubora wake, utakaompa nafasi ya kucheza zaidi, akishindwa kufanya kile tunachokitarajia kutoka kwake atawapisha wengine wacheze.”

 WANAMJUA (NIDHAMU)

Kama ambavyo Yanga imemudu kuishi na Jonas Mkude basi inaweza kutafuta namna bora ya kuishi na Okrah ambaye naye anatajwa kuwa  ana mambo mengi nje ya uwanja.

Zipo namna nyingi za kudili na mchezaji mwenye tabia kama za Okrah, kisa cha Jose Mourinho na Douglas Maicon ni mfano mzuri, unajua ulikuwaje? wakati Mourinho ni kocha wa Inter Milan, alipewa taarifa juu ya mienendo ya wachezaji wengi wa Kibrazili, wengi wanapenda kuwepo nyumbani wakati sherehe mbalimbali.

Sasa Maicon ni mmoja kati ya nyota ambao Kocha Mourinho alitahadharishwa nao, wakati wanaelekea Sienna kwa ajili ya mechi, Mourinho akamuita Maicon na kumueleza tayari una kadi za njano nne zimefuatana, hivyo najua leo utapata kadi ya tano ya njano ili ukose mchezo unaofuata ili uelekee Brazil kwa ajili ya Krisimasi nakuomba usithubutu.

Maicon akamuuliza kocha vipi kama akifunga goli atampa ruhusa? Mourinho akamwambia afunge mawili atamruhusu.  Beki huyo wa kulia alipiga soka la kufa mtu ili apate hizo goli mbili kisha apewe ruhusa, ni kweli Maicon alifunga bao  kisha akafunga bao la pili, akavua jezi akashangilia na akapata ruhusa ya kwenda kwao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live