Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo matano ya Amaan Complex

Uwanja Wa Amaan ZNZ KKK.jpeg Mambo matano ya Amaan Complex

Mon, 3 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, Zanzibar, wenye uwezo wa kuingiza watazamaji zaidi ya 15,000, bado upo kwenye maboresho.

Uwanja huo ambao umeipa heshima Yanga kwa kutetea ubingwa wao wa Kombe la Shirikisho (FA) kwa kuifunga Azam penalti 6-5, umekuwa wa kisasa zaidi tofauti na hapo awali.

Mwaka 1970 uwanja huu ndiyo ulijengwa na Serikali ya China ambapo ni wa kwanza kujengwa na Serikali hiyo katika ‘project’ yake kwa nchi za Afrika.

Baada ya kutumika kwa takribani miaka 40 ukiwa na nyasi za asili, hatimaye mwaka 2010, ukafanyiwa maboresho na kuwekwa nyasi bandia. Katika Kipindi chote hicho, ulikuwa ukiitwa Uwanja wa Amaan.

Miaka 13 mbele kutoka 2010 hadi 2023, yakafanyika maboresho mengine ambayo awamu hii yameufanya uwanja huo kuwa wa kisasa zaidi huku zikiwekwa nyasi zingine bandia.

Desemba 27, 2023, katika uzinduzi wa uwanja huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi aliridhia ushauri wa kuubadili jina na kuitwa New Amaan Complex.

Rais Mwinyi ambaye ndiye aliyeweka jiwe la uzinduzi wa uwanja huo, aliridhia ushauri huo uliotolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro alipokua akitoa salamu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk. Ndumbaro alisema: “Kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuufanya uwanja huu kuwa wa kisasa na wenye viwango vya kimataifa, mimi naomba niubadilishe jina uitwe New Amaan Stadium.”

Kwa mujibu wa Meneja wa Uwanja wa Mao Zedong ambaye hapo awali alikuwa akiusimamia pia Uwanja wa Amaan kabla ya kupisha maboresho, Mohamed Hilary 'Tedi', New Amaan Complex bado maboresho yake yanaendelea, hivyo haujakabidhiwa rasmi na wakandarasi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Licha ya kwamba bado maboresho yanaendelea, lakini uwanja huu umeruhusiwa kutumika kutokana na kukamilika kwa kiasi kikubwa katika sehemu mbalimbali ikiwemo ile ya kuchezea, majukwaa, vyoo, vyumba vya kubadilishia nguo kwa wachezaji na waamuzi sambamba na vyumba maalum vya waandishi wa habari.

Kinachoendelea kwa sasa ni mafunzo mbalimbali yanayotolewa na wakandarasi wa uwanja huo kwenda kwa watu maalumu wanaoandaliwa kuusimamia pindi maboresho yatakapokamilika kwa asilimia 100.

Ukiachana na uwanja mkubwa ambao ndiyo ulifanyika mchezo wa fainali, pia pembeni kuna viwanja vidogo viwili ambavyo navyo vinachezewa mechi mbalimbali zikiwemo zile za Ligi Kuu ya Zanzibar.

Hapa kuna mambo matano Mwanaspoti inakupatia kutoka katika uwanja huo wenye uwezo wa kutumika nyakati zozote, iwe usiku, asubuhi, mchana, jioni, kipindi cha jua au mvua kutokana na ulivyojengwa.

UTARATIBU WA KUINGIA UWANJANI

Umewekwa utaratibu mzuri wa kuingia uwanjani New Amaan Complex ambapo watazamaji hawapati usumbufu wa aina yoyote.

Hilo limeshuhudiwa katika mchezo mkubwa wa fainali ya Kombe la FA ambao Yanga ilitwaa ubingwa kwa ushindi wa penalti 6-5 kwani licha ya kwamba watazamaji kujivuta kuingia uwanjani na kujikuta wakiwa wengi magetini saa tatu kabla ya mechi, lakini utaratibu uliowekwa ulikuwa rafiki.

Ukiachana na mageti makubwa yaliyopo nje kabisa katika uzio, lakini yale mageti ya kuingilia majukwaa yamewekwa kwa mpangilio mzuri na wa kuvutia.

Mtazamaji ukiwa na tiketi yako, unaangalia imeandikwa geti namba ngapi, ukienda hapo unaingia jukwaani kwako. Kuna mageti zaidi ya kumi. Hiyo inaondoa usumbufu wa watu kujazana kwenye geti moja wakati wa kuingia kama ilivyo viwanja vingine.

MAZINGIRA

Hali ya usafi ndani ya uwanja wa New Amaan Complex inaridhisha kwa kiasi kikubwa. Ikiwa imepita takribani miezi sita tangu kuzinduliwa kwake, lakini bado umeonekana kuwa kwenye nzuri ya usafi. Ukienda vyooni hukutani na harufu mbaya, wala mikojo kusambaa.

SEHEMU YA KUCHEZEA

Kwa sasa kuna nyasi bandia, lakini hapo baadaye zitatolewa na kuweka nyasi asilia ikiwa ni maandalizi ya kuelekea michuano ya AFCON 2027 ambayo itafanyika kwenye nchi tatu za Ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania, Kenya na Uganda. Kwa Tanzania, Zanzibar utatumika Uwanja wa New Amaan Complex, Benjamin Mkapa (Dar es Salaam) na uwanja utakaojengwa Arusha.

MAJUKWAA

Maboresho ya sasa yameufanya uwanja kuwa na viti majukwaa yote tofauti na awali ambapo kule V.I.P ndipo kulikuwa na viti pekee, lakini majukwaa mengine hakukuwepo.

Kama unavyoona Uwanja wa Uhuru, Sokoine na vinginevyo vya Tanzania Bara katika majukwaa ya mzunguko, ndivyo ilivyokuwa awali Uwanja wa Amaan, lakini hivi sasa kote kuna viti kama Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Changamoto moja iliyopo kwenye majukwaa ya karibu na V.I.P A, ukikaa vibaya unaweza usione matukio yote kwa sababu kuna sehemu inayotenganisha majukwaa hayo kuna ukuta, hiyo inasababisha watazamaji kuacha viti vilivyopo eneo hilo na kukaa kwenye ngazi.

RUNINGA NNE

Katika kona nne za Uwanja wa New Amaan Complex, kuna runinga zinazoonyesha matukio ya uwanjani ikiwemo matokeo ya mechi na dakika, hii inawafanya watazamaji waliopo uwanjani kuangalia kirahisi matukio hayo. Viwanja vingine ikiwemo Benjamin Mkapa na Azam Complex kuna runinga moja pekee.

Chanzo: Mwanaspoti