Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo manne yanayomkabili bosi mpya United

Omar Berrada Mambo manne yanayomkabili bosi mpya United

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Jumamosi ya wiki iliyopita Manchester United ilithibiisha kuajiriwa kwa Omar Berrada ambaye atakuwa mtendaji mkuu wa timu hiyo.

Berrada ambaye ametokea kwa wapinzani wao wa jiji moja, Manchester City, amekuwa ndiye mtu wa kwanza kuajiriwa tangu Sir Jim Ratcliffe aliponunua hisa za asilimia 25 za Mashetani Wekundu.

Omar amechukua nafasi ya Richard Arnold ambaye aliondoka Man United Desemba mwaka jana na nafasi yake kukaimiwa na Mwanasheria Patrick Stewart.

Kigogo huyu ameichukua timu ikiwa haipo kwenye hali nzuri na atakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha anaijenga upya. Haya hapa ni mambo manne ambayo Berrada atatakiwa kuanza kuyafanyia kazi kwenye kikosi hicho.

KUONDOA WACHEZAJI

Tayari Jadon Sancho na Donny van de Beek wameshaondoka kwenye kikosi hicho. Sancho ametua Borussia Dortmund kwa mkopo na va de Beek ameenda Eintracht Frankfurt ambayo ina nafasi ya kumsajili mazima mwishoni mwa msimu kupitia kipengele kilichopo kwenye mkataba wake huo wa mkopo.

Anthony Martial na Raphael Varane wote mikataba yao inamalizika nwishoni mwa msimu huu na wana vipengele vya kuirefusha kwa miezi 12 zaidi ikiwa watahitajika kufanya hivyo. Lakini huenda wakaachwa. Kiungo wa Kibrazili, Casemiro, aliyejiunga akitokea Real Madrid kwa Pauni 70 milioni miezi 17 iliyopita naye amekuwa akihusishwa na kutaka kuondoka kwa sababu hivi karibuni haonekani kwenye sehemu kubwa ya mipango ya Kocha Ten Hag.

Harry Maguire ambaye ilishindikana kuuzwa katika dirisha lililopita naye ni mmoja kati ya wachezaji ambao mashabiki wa timu hii wanatamani kuona akiondoka kutokana na viwango vyao. Pia, wachezaji kama Victor Lindelof, Antony, Mason Mount, Andre Onana na Facundo Pellistri, pia wanatajwa kutakiwa kuuzwa.

Barrada atakuwa na kazi ya kumalizana na baadhi ya mastaa hawa katika dirisha la majira ya kiangazi ili kuanza kujenga upya kikosi hicho.

KUJADILI MKATABA WA TEN HAG

Ikiwa kocha huyu ataendelea kuwepo Manchester United, Barrada atatakiwa kujadili naye upya kuhusu mkataba wake ambao una kipengele cha kuwa na mamlaka ya kusajili mchezaji yeyote anayemhitaji.

Kipengele hicho kina nguvu na kimeisababishia Man United hasara kutokana na sajili ambazo Ten Hag ameziidhinisha ikiwa pamoja na ile ya Antony aliyetua kwa Pauni 82 milioni.

Wout Weghorst aliyesajiliwa kwa mkopo na Andre Onana aliyechukua nafasi ya David de Gea wote hawa wameshindwa kuonyesha viwango vilivyotarajiwa na wengi.

Ili kuweza kuleta ufanisi Berrada atakuwa na kazi ya kuondoa kipengele hicho kwa kocha huyo.

KUSAJILI WACHEZAJI SAHIHI

Mmoja kati ya watu muhimu waliofanikisha usajili wa wachezaji wengi kwenye kikosi cha Manchester City alikuwa ni huyu Berrada.

Moja kati ya mambo ambayo amekuwa akipongezwa nayo ni kukamilisha mchakato wa kusajiliwa kwa mshambuliaji, Erling Haaland ambaye hadi sasa amefunga mabao 71 kwenye mechi 75 za michuano yote alizoichezea timu hiyo na wakati anatua Man City alikataa ofa za Real Madrid na Barcelona.

Pia, Berrada amekuwa akisifika kwa kusajili mastaa wenye uwezo mkubwa kwa bei ndogo akifanya kazi hiyo kuanzia mwaka 2016 ambapo aliteuliwa rasmi kama mkuu wa masuala ya mpira wa miguu wa Man City na timu nyingine zinazomilikiwa na wamiliki wa Man City.

Alifanikisha kusajiliwa kwa mastaa kama Ruben Dias, Jeremy Doku, Rodri, Bernardo Silva, Julian Alvarez, Manuel Akanji, Josko Gvardiol na Ederson. Asilimia kubwa ya mastaa hawa wameonyesha viwango bora, kazi hii atatakiwa aihamishie kwa Man United ambayo imekuwa ikisajili mastaa kwa bei kubwa lakini wanashindwa kuonyesha viwango bora.

UWEKEZAJI KWENYE MIUNDOMBINU

Licha ya ukweli kwamba jambo muhimu kwa sasa ni kujenga kikosi, mashabiki pia wanahitaji kuona maboresho ya miundombinu ya timu hiyo.

Kwa takribani miaka 20 iliyopita Old Trafford kilikuwa moja kati ya viwanja bora England lakini sasa kinazidiwa na Emirates, Wembley, Etihad, Anfield na hata Uwanja wa Tottenham.

Mbali ya uwanja wa kuchezea pia uwanja wao wa mazoezi bado ni wakizamani ukilinganisha na viwanja vingi vya za England.

Licha ya kwamba kuna mazungumzo na wawekezaji juu ya kuingia mkataba wa kuboresha viwanja hivyo, jambo ambalo Barrada atatakiwa kuhakikisha linafanikiwa ni hili.

Chanzo: Mwanaspoti