Klabu ya Manchester City ipo katika wakati mgumu baada ya taarifa kutolewa na bodi ya Ligi Kuu England, wanashtakiwa kwa makosa 100 kwa kukiuka kanuni za mapato na matumizi kwenye masuala ya usajili.
Endapo Man City itakutwa na hatia kutokana na mashtaka hayo, itakumbana na adhabu kutoka bodi ya ligi, vilevile klabu hiyo huenda ikawakosa baadhi ya mastaa wake.
Kuna taarifa zimeripoti mpango wa kumsajili kiungo anayekipiga Borussia Dortmund, Jude Belligham umeanza kuingia dosari kutokana na kashfa hiyo.
Miamba hiyo ya Etihad imejikuta ikiingizwa hatiani baada ya maofisa wanaoshughulika na mambo ya pesa na matumizi kuifanyia uchunguzi klabu hiyo kwa muda wa miaka minne.
Jambo lingine ni Man City inaweza kupokwa pointi 15 kama adhabu baada ya kukiuka kanuni hizo kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa.
Vile vile, kocha anayeinoa timu hiyo Pep Guardiola akaachana na klabu hiyo licha ya kusaini mkataba wa miaka miwili mwaka jana baada ya klabu hiyo kuingizwa matatani.
Hatima ya Guardiola inategemea na hukumu itakayotolewa endapo Man City itakutwa na hatia kutokana na mashtaka hayo makubwa yaliyofanyiwa uchunguzi kwa muda wa miaka minne.
Kutokana na sakata hilo huenda mastaa hawa wakaondoka endapo Man City ikikutwa na hatia ya kutenda makosa hayo.
Joao Cancelo Licha ya kutolewa kwa mkopo Bayern Munich hadi msimu ujao huenda asirudi tena Etihad kutokana na kinachoendelea ndani ya klabu hiyo. Kipengele cha mkataba wa Joao unasema Beyern inaweza kumnunua jumla endapo itakubali kufanya biashara na Man City msimu utakapomalizika.
Imeelezwa Joao atauzwa kwa kitita cha Euro 70 milioni endapo Bayern itakuwa tayari kumchukua jumla.
Beki huyo wa kimataifa wa ureno alijiunga na miamba hiyo kutoka Bundesliga dirisha dogo la usajili la Januari.
Ilkay Gundogan Kiungo huyo mkataba wake unaelekea ukingoni kumalizika mwishoni mwa msimu, amehusishwa na Barcelona tangu dirisha la kiangazi la usajili lakini Man City ikachomoa.
Kutokana na uzoefu wake kiungo huyo wa kimataifa wa Ujerumani ana uzoefu mkubwa na uwezo wake bado unatambulika barani ulaya.
Huyu ni nyota mwingine ambaye anaweza akatafuta mlango wa kutokea endapo Man City itakutwa na hatia ya kukeuka kanuni za matumizi mabaya ya fedha.
Bernardo Silva Kiungo mwingine aliyehusishwa na Barcelona tangu dirisha la usajili la kiangazi. Itakuwa ngumu Silva kubaki Etihad endapo mambo yataharibika kutokana na kashfa inayowakabili Man City.
Kiungo wa zamani wa Monaco alionyesha nia ya kuondoka msimu uliopita lakini kutokana sakata hili, huenda kiungo huyu tamaa zake za kutaka kuondoka zikaibuka upya.
Silva ametoa mchango mkubwa katika mafanikio waliyopata Etihad ikiwemo kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England mfululizo.
Ruben Dias Beki kisiki na muhimu kwa klabu ya Man City. Ruben huenda akatafuta mlango wa kutokea endapo klabu hiyo itapewa adhabu ya kupokwa pointi 15 au kushushwa daraja? Haya ni maswali na majibu yatayokuja endapo Man City itakutwa na hatia.
Beki huyo ana kiwango cha hali ya juu kukipiga katika klabu kubwa Ulaya. Kutokana na sakata linalowakabili huenda hiyo ikawa ndio sababu kubwa wa yeye kusepa na kutafuta maisha sehemu nyingine.
Erling Haaland Itakuwa taarifa mbaya endapo straika huyu wa kimataifa wa Norway ataondoka. Haaland amekiwasha Ligi Kuu England tangu alipotua akitokea Borussia Dortmund kwa kitita cha Pauni 51 milioni.
Mpaka sasa Haalanda ameshaweka kambani mabao 31 katika mechi 31 alizocheza tangu alipojiunga na Man City. Haaland alihusishwa na timu kibao kama Real Madrid, Manchester United na Paris- Saint Germain kabla ya kutua Etihad.
Straika huyu mwenye uwezo wa kupachika mabao bado anazitoa udenda timu kubwa kibao Ulaya. Kutokana na majanga ya Man City yanayowakabili huenda ikawa nafasi pekee kwa klabu hizi kugombe saini siku za usoni.