Fainali za 34 za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zinaendelea Ivory Coast. Kwenye fainali hizo kuna mambo mengi unaweza ukawa umeyaona na unajiuliza maswali mengi bila majibu ya kukushibisha ikiwamo fainali hizo za 2023 kuchezwa mwaka huu. Kwenye makala haya utapata majibu ya kile unachojiuliza.
AFCON 2023 KUFANYIKA 2024
Fainali hizo zilipangwa kufanyika Julai 2023. Sababu kubwa ni kuepusha migongano na klabu za Ulaya na wachezaji wake wengi wa Afrika huenda kuwakilisha mataifa yao.
Julai, ligi nyingi hasa za Ulaya humalizika na wachezaji hurudi kwenye mataifa yao ikiwamo mapumziko na majukumu ya timu za taifa kama kuna mashindano. Hivyo, hilo halithiri klabu za Ulaya kwa kuwakosa wachezaji muhimu kama zilivyokuwa fainali za Afcon 2019 zilizofanyika Misri.
Hata hivyo, fainali za 2023 zililazimika kufanyika mwaka huu (2024) baada ya serikali ya Ivory Coast kutuma maombi maalumu katika Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kubadilisha ratiba ya mashindano hayo kutoka Julai, 2023 hadi Januari 2024 kutokana na sababu za Kijiografia.
Hii ni kwa sababu Julai nchini humo huwa ni kipindi cha mvua kubwa ambazo zingeathiri fainali hizo kuchezwa na CAF kuzisogeza na kuanza Januari hadi Februari, mwaka huu.
Hata hivyo, jina la fainali hizo limebaki ‘Afcon 2023’ kwa sababu za kiudhamini na nyaraka nyingi zilishatengenezwa na promosheni kubwa ilifanyika mwaka huo.
GUINEA ZA KUMWAGA
Kwenye Afcon za mwaka huu nchi tatu zina majina yanayofanana. Guinea, Guinea-Bissau na Guinea ya Ikweta (Equetorial Guinea).
Ni hivi. Guinea ni jina lenye asili ya lugha ya Kireno ‘Guiné’ na maana yake ni ‘watu weusi’.
Wareno walifika Afrika Magharibi, Kusini mwa Mto Senegal miaka ya 1500 na kuwakuta watu weusi ‘Guiné’ kwa lugha yao, na eneo hilo wakaliita hivyo. Hii ikasababisha sehemu kubwa ya eneo la Afrika Magharibi kuitwa Guinea.
Mataifa mengine ya Ulaya yakafika eneo hilo na kujigawia ardhi, kila mmoja akajichukulia eneo lake na kuliita Guinea yake.
Ufaransa ikajikatia eneo na kuliita French Guinea yaani Guinea ya Ufaransa, Wahispania nao wakajikatia eneo lao na kuliita Spanish Guinea yaani Guinea ya Hispania na Ureno ikaliita eneo lake Portuguese Guinea yaani Guinea ya Ureno.
Miaka ikapita na kila Guinea ikaanza kupigania uhuru. Ile ya Ufaransa ikawa ya kwanza kupata uhuru, mwaka 1958 na kujiita ‘Guinea’ kwa kuwa ndiyo ilikuwa ya kwanza kuwa huru. Hii ndiyo Guinea inakotoka klabu ya Horoya AC na mji mkuu wake ni Conakry.
Guinea zingine zilipokuja kupata uhuru ikabidi zitafute njia ya kujitofautisha na Guinea iliyotangulia. Ndipo ile Guinea ya Wareno ikajiita Guinea Bissau, ikitumia mji mkuu wake kujitofautisha.
Ile ya Wahispania ikajiita Equatorial Guinea yaani Guinea ya Ikweta, kwa sababu inapitiwa na mstari wa Ikweta.
NYIMBO ZA TAIFA KUFANANA
‘Mungu Ibariki Afrika’. Ni wimbo wa Taifa wa Tanzania. Ni mojawapo wa nyimbo za taifa zinazovuta hisia kali za uzalendo.
Wimbo huu unafanana na nyimbo za taifa za Zambia na Afrika Kusini na kwenye fainali za Afcon zinazoendelea Ivory Coast ulivuta hisia za watu kutokana na kutumiwa na nchi hizo.
Kwenye mchezo wa Tanzania dhidi ya Zambia Februari 21, ulikonga nyoyo za watu kwa kuusikia mara mbili kutokana na kufanana kwake.
Ulikoanzia
Kiasili huu wimbo unatokea Afrika Kusini na ulitungwa 1897 na Enoch Sontonga, aliyekuwa mwalimu katika shule iliyokuwa ikimilikiwa na kanisa la Methodist mjini Johannesburg.
Lugha ya asili ya wimbo huu ni Xhosa (tamka Kosa) moja ya makabila makubwa nchini humo na jina lake ni ‘Nkosi Sikeleli Afrika’ yaani Mungu Ibariki Afrika.
Hicho kilikuwa kipindi cha ubaguzi wa rangi na chama cha kupigania haki za weusi cha ANC kikauchukua na kuufanya kuwa wimbo wa kuhamasishana.
Tanzania iliuchukua wimbo huu na kuurafsiri kwa Kiswahili na kuongezea kidogo baadhi ya maneno na kuufanya kuwa wimbo wa taifa tangu 1961 baada ya Uhuru.
Kwa kufanya hivyo, Tanzania ikawa nchi ya kwanza kuutumia kama wimbo wa taifa. Zambia nayo ilipopata uhuru wake mwaka 1964 ikaufanya kuwa wimbo wa taifa.
Namibia ilipopata uhuru wake mwaka 1990 nayo ikaufanya kuwa wimbo wa taifa. Lakini baadaye ikabadilisha na kutunga wimbo mpya.
Stori ya Namibia ni sawa na Zimbabwe ambayo nayo iliutumia wimbo huu kuanzia 1973 kisha ikaubadilisha na kutunga mwingine.
Baada ya kuanguka utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na ANC kushika dola, baadhi ya mashairi ya wimbo huu yakajumuishwa kwenye wimbo mpya wa taifa wenye beti nne za lugha nne tofauti zinazozungumzwa sana nchini humo; Xhosa, Zulu, Sesitho na Afrikaans.
RANGI ZA BENDERA
Bendera za mataifa mengi hasa ya Afrika Magharibi zina rangi nyekundu, kijani na njano. Tofauti pekee ya bendera hizo ni mpangilio wa rangi na vitu vidogo vidogo kama nyota ndani yake. Kimsingi hizo ni rangi za umajumui wa Afrika (Pan Africanism) na asili yake ni Ethiopia.
Oktoba 11, 1897, mwaka mmoja baada ya Ethiopia kufanikiwa kuilinda nchi yao dhidi ya uvamizi wa Italia ili kuitawala kama mkoloni, mtawala wao Menelik wa Pili aliamrisha itengenezwe bendera mpya ya taifa hilo yenye rangi tatu yaani nyekundu, njano na kijani.
Bendera hiyo ndiyo ikawa alama ya ushujaa wa Ethiopia kuwashinda wavamizi waliotaka kuitawala. Hii ndiyo sababu Ethiopia kuwa nchi pekee ambayo haijawahi kutawaliwa na wakoloni barani Afrika.
Japo mpangilio wa rangi wa bendera hiyo ulibadilika mara kwa mara kutokana na mabadiliko ya kiutawala nchini humo, lakini rangi zilibaki zilezile.
Watu weusi wote duniani waliziona rangi hizo kama rangi za ushindi dhidi ya ukandamizaji na kuzifanya kuwa rangi rasmi za umajumui wa Afrika.
Ghana ilipopata uhuru mwaka 1957 na kuwa nchi ya kwanza Kusini kwa Jangwa la Sahara kupata uhuru, iliamua kuzitumia rangi hizo kwenye bendera.
Rais wa nchi hiyo wa kwanza, Kwame Nkrumah alikuwa mwanamajumui mkubwa wa Afrika aliyeota ndoto ya kuiunganisha Afrika kuwa nchi moja.
Nkrumah alivutiwa na ushindi wa Ethiopia dhidi ya wakoloni. Nchi zingine za Afrika zilipopata uhuru zikapita njia ya Ghana kwa kuzichukua rangi hizo na kuziweka kwenye bendera zao. Guinea ilipopata uhuru mwaka 1958 ikafanya kama Ghana, lakini ikabadili mpangilio wa rangi kwa kuziweka wima rangi zake.
Bendera ya Mali ni kama ya Guinea, ila rangi ya kijani inatangulia na nyekundu mwishoni. Bendera ya Cameroon ni kama ya Mali, ila ina nyota ya njano. Bendera ya Senegal inafanana sana na ya Mali, tofauti ni nyota ya kijani katikati.
Nchi nyingine za Afrika zenye kutumia rangi hizo kwenye bendera ni pamoja na Togo, visiwa vya Comoro, Burkina Faso, Shelisheli, Guinea-Bissau, Sao Tome & Principe, DR Congo, Msumbiji, Zimbabwe, Mauritania na Benin.