Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo 7 ya kusisimua kwenye EPL wikiendi iliyopita

Mambo 7 Mambo 7 ya kusisimua kwenye EPL wikiendi iliyopita

Mon, 2 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

MASHABIKI wa Ligi Kuu England hatimaye wamepata pumzi baada ya wikiendi ambayo ilikuwa ya kusisimua na kushangaza, lakini mjadala bado unaendelea kutokana na mambo yaliyojitokeza katika mechi mbalimbali kwenye viwanja tofauti.

Michezo tisa kati ya 10 iliyopangwa tayari imefanyika, lakini wikiendi iliyopita tuliona mizengwe ya kila aina, mabao, kadi nyekundu na uamuzi mwingi wenye utata.

Kwa mujibu wa gazeti la Mirror yafuatayo ni mambo saba ya kusisimua yalitokea katika Ligi Kuu England wikiendi iliyopita.

VAR YAZUA GUMZ0

Licha ya Liverpool kupokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Tottenham Hotspur, kifaa cha teknolojia cha kumsaidia mwamuzi (VAR) kilizua gumzo baada ya bao la wazi lililowekwa kimiani na Luis Diaz kukataliwa ikidaiwa kuwa aliotea. Hata hivyo, mabosi wakuu wa waamuzi (PGOML) walikiri kutokea kwa dosari hiyo iliyosababishwa na makosa ya kibinadamu.

Wadadisi wa mambo baada ya kurudia picha za marudio ya mechi ilionekana wazi Diaz alikuwa sehemu sahihi. Naye kocha wa Liverpool alicharuka baada ya mechi kumalizika: "Sijawahi kuona mechi kama hii, mazingira yasiyo ya haki, maamuzi ya kichaa kabisa. Kadi nyekundu ya kwanza, hata kadi ya njano ya Diogo Jota, bao alilofunga Diaz ni halali kabisa."

Postecoglou matumaini kibao kwa Richarlison

Ushindi wa Tottenham wa mabao 2-1 dhidi ya Liverpool umempa mwangaza Richarlison kwani kocha Ange Postecoglou alimuacha acheze dakika 90 licha ya kutocheka na nyavu. Mbrazil huyo alikuwa akisumbuliwa na msongo wa mawazo kipindi cha mapumziko ya mechi za kimataifa na kuthibitisha kwamba amepanga kuonana na mtaalamu wa mambo ya kisaikolojia.

Kocha huyo alisema: "Tutamsapoti Richarlison na kumuongoza hadi atakapojisikia furaha tena. Niwaambie hivi Richarlison atacheza sana tu."

Richarlison aliifungia timu yake akitokea benchi dhidi ya Sheffield United mwezi uliopita na kushangiliwa na wachezaji wenzake.

Hojlund presha juu

Harry Kane alihusishwa na Man United katika usajili wa dirisha la kiangazi lakini mwisho akajiunga na Bayern Munich.

Baada ya kuaminika kwamba Kane hatajiunga na Old Trafford, mabosi wa Man United walimsajili Rasmus Hojlund. Straika huyo wa zamani wa Atalanta bado hajaonyesha makali katika EPL lakini kuna pesha imekuwa kubwa dhidi yake. Straika huyo licha kupambana dhidi ya Crystal Palace alishindwa kuisaidia timu yake kuepuka kipigo cha bao 2-1.

Man United imeshinda mechi tatu katika mechi saba za Ligi Kuu England, huku Bruno Fernandes akifunga zaidi ya bao moja akiwazidi mastraika.,

Southgate asimpuuze Watkins

Ukizungumzia mastraika, Ollie Watkins alidhihirisha wikiendi iliyopita kwamba ana kitu msimu huu. Straika huyo wa kimataifa wa Ligi Kuu England alifunga hat-trick katika ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Brighton matokeo hayo yaliwashangaza kila mtu. Kabla ya kufunga hat-trick Watkins alikuwa na bao moja tu.

Wachambuzi hawakumjadili Watkins sana lakini mambo yalikuwa tofauti baada ya ushindi huo dhidi ya Brighton. Lakini straika huyo ambaye alifunga mabao 15 msimu uliopita bado ana nafasi ya kufunga zaidi katika msimu huu. Anachohitaji Watkins kwa sasa Southgate amfuatilie kila mechi jukwaani pengine atamshawishi.

Man City yapunguzwa kasi

Katika mechi sita za mwisho za Ligi Kuu England ambazo Manchester City ilicheza ilionyesha kwamba haina masihara hata kidogo na inataka kuendeleaza mafanikio yao kama ilivyokuwa msimu uliopita. Kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Newcastle kwenye Kombe la Carabao, kilikuwa ni kengele ya tahadhari, lakini baada ya kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Wolves katika mechi ya Ligi Kuu England wikiendi iliyopita imeonyesha taswira ya wanakoelekea City msimu huu.

Lakini kocha Pep Guardiola alisema wazi kwamba kuna tofauti katika mechi hizo mbili. Anaamini kocha wa Wolves, O'Neil alistahili ushindi kwani walionyesha kiwango bora. Pia tofauti nyingine ni kwamba Man City haikuwa na malengo makubwa katika mbio za kuwania Kombe la Carabao msimu huu.

Arsenal mwendo mdundo

Arsenal ilitisha wikiendi iliyopita kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Bournemouth katika mechi ya Ligi Kuu England langoni akisimama kipa David Raya bila ya kuruhusu bao. Katika mechi saba za EPL, Arsenal imepata ushindi mechi sita na kutoa sare mechi moja.

Kabla ya mchezo huo, Arsenal ilitinga raundi ya nne ya michuano ya Kombe la Carabao kwa kuichapa Brentford bao 1-0 lililowekwa kimiani na Reiss Nelson.

Luton City yaona nuru

Wadadisi wa mambo ya soka walishindwa kuitabiria ushindi Luton mwanzo wakati msimu unapoanza. Kocha wa timu hiyo alipokea kichapo kizito dhidi ya Brighton na Chelsea, hata walipocheza nyumbani dhidi ya West Ham mambo yalikuwa magumu.

Lakini timu hiyo iliimarika kutokana vichapo hivyo na wikiendi iliyopita ilipata ushindi wa kwanza tangu ilipopanda ligi msimu huu. Tom Lockyer na Carlton Morris walifunga mabao katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Everton uwanja wa Goodison Park na kuchomoka mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu England. Na huenda leo ikajipinda dhidi ya Burnley ambayo haijapata ushindi mpaka sasa kufuatia ushindi huo.

Chanzo: Mwanaspoti