Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo 5 mazito usiyoyatua Simba Day

Samia Awashukuru Simba Mambo 5 mazito usiyoyatua Simba Day

Tue, 8 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Simba juzi ilisherehekea tamasha lake la kila mwaka, 'Simba Day', ilipocheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.

Waliofurika uwanjani na kuangalia kwenye televisheni walishuhudia kutangazwa benchi la ufundi na wachezaji wote wa kikosi cha msimu wa 2023/24, wakiwamo wachezaji wapya na wanaorejea tena kwenye kikosi hicho.

Baadhi ya hao ni Aubin Akramo aliyesajiliwa kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast, Willy Onana kutoka Rayon Sport ya Rwanda, Che Fondon Malone aliyechukukuliwa kutoka Cotonsport ya Cameroon, pamoja na urejeo wa winga wa zamani wa timu hiyo, Luis Miquissone.

Mbali na hilo kulikuwa na burudani mbalimbali za muziki wa dansi pamoja na wanamuziki mbalimbali wa Singeli, Hip Hop na Bongo Fleva, waliokuwa wakitumbuiza kabla ya mechi yenyewe kuhitimisha tamasha hilo.

Limekuwa ni tamasha la 15 tangu lilipoasisiwa mwaka 2009 na aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu hiyo mwaka huo, Hassan Dalali 'Field Marshal', ambapo wanachama na mashabiki wa klabu hiyo huanza kwa kufanya kazi na shughuli za kijamii, ikiwamo kutoa misaada kwenye vituo vya watoto yatima, hospitalini, magereza.

Shughuli hizo hufanyika kwa matawi mbalimbali ya wanachama nchi nzima, pamoja na kuchangia damu ili kuwasaidia wahitaji.

Makala haya inawaletea rekodi ambazo zimewekwa tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo 2009 ilipocheza kwa mara ya kwanza dhidi ya SC Villa ya Uganda na kushinda bao 1-0.

#1. Hakuna mchezaji wa 2009 lilipoanzishwa

Simba juzi ilicheza mechi yake ya 15 ya tamasha lake bila kuwa na mchezaji yeyote aliyekuwamo kwenye kikosi kilichocheza mechi ya kwanza 2009.

Rekodi inaonyesha kuwa mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam (sasa Uhuru), Agosti 8, mwaka huo, Simba ikishinda bao 1-0 lililofungwa na Hilary Echessa dakika ya nane ambaye alikuwa amesajiliwa kwa mara ya kwanza kutoka nchini Kenya.

Ikiwa chini ya kocha Mzambia Patrick Phiri, ikiwa na baadhi ya wachezaji kama Emmanuel Okwi na Joseph Owino, ambao nao walikuwa wamesajiliwa kwa mara ya kwanza kutoka Uganda.

#2. Mkude nje baada ya miaka 12

Aliyekuwa kiungo mkabaji wa timu hiyo, Jonas Mkude alikosekana kwa mara ya kwanza kwenye Simba Day baada ya miaka 12.

Kwa mara ya kwanza Mkude alitambulishwa msimu wa 2011/12 akiwa amepandishwa kutoka kikosi cha pili na muda mrefu amekuwa kwenye kikosi hicho na mpaka msimu uliopita alikuwa ndiye mchezaji aliyekaa miaka mingi Simba na mwenye Simba Day nyingi zaidi kuliko yeyote yule.

Angeendelea na rekodi hiyo kama angebakishwa na klabu yake ili kufikisha miaka 13, lakini alionyeshwa mlango wa kutokea na sasa amesajiliwa na Klabu ya Yanga.

#3. Tshabalala aongoza Simba Day

Beki wa kushoto wa klabu hiyo, Mohamed Hussein 'Tshabalala' au 'Zimbwe Jr', ndiye aliyecheza mechi nyingi za Simba Day kuliko mchezaji mwingine yeyote kwa sasa katika kikosi hicho.

Juzi alitambulishwa mara ya 10 kwenye tamasha hilo, akiwa pia mchezaji wa muda mrefu aliyebaki kwenye kikosi hicho aliyecheza mfululizo.

Mchezaji huyo aliibukia kwenye kikosi cha pili cha Azam FC chini ya miaka 19, mwaka 2013 na akachukuliwa na Kagera Sugar akicheza kwa msimu mmoja wa 2013/14 kabla ya kunyakuliwa na Simba 2014 ambapo tangu hapo si tu amekuwa kwenye kikosi hicho kwa misimu yote mfululizo, bali akiwa tegemeo pia.

#4. Kapombe mkongwe aliyerejea

Kama si kuihama timu hiyo na kurejea tena 2017, Shomari Kapombe ndiye angekuwa mchezaji pekee aliyecheza Simba Day nyingi zaidi.

Angekuwa amecheza mara 13 na kuweka rekodi hiyo kama asingeondoka kwenda Cannes ya Ufaransa mwaka 2013 na hata aliporejea alijiunga na Azam FC mwaka 2014 hadi 2017 ndipo aliporejea tena klabu ya Simba na kuitumikia hadi leo hii.

Amezikosa Simba Day nne kuanzia 2013 hadi 2016, hivyo amecheza tisa ingawa si kwa mfululizo kama Tshabalala ambaye ana 10 zilizonyooka.

Kapombe alijiunga na Simba mwaka 2011 akitokea Polisi Morogoro na kuanza moja kwa moja kuchezeshwa mechi za Ligi Kuu kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho, hasa uwezo wake wa kucheza namba nyingi uwanjani, ingawa alikuwa amesajiliwa kama mchezaji wa kikosi cha pili, kabla ya kupandishwa msimu uliofuata.

#5. Simba Day ya kwanza kwa Miquissone

Utashangaa kuona kuwa juzi ilikuwa ni Simba Day ya kwanza kwa winga Luis Miquissone kwenye kikosi cha Simba kama wachezaji wenzake waliosajiliwa msimu huu.

Pamoja na kwamba aliwahi kuichezea msimu wa 2021/22, lakini wakati wa tamasha hilo aliomba ruhusa kwenda kwao Msumbiji kuoa, msimu uliofuata hakuweza tena kutambulishwa kwa sababu aliuzwa Klabu ya Al Ahly ya Misri.

Mchezaji huyo alithibitisha hilo mwenyewe kabla ya mechi ya juzi.

"Nimerudi kwa sababu ya mashabiki wangu, mara ya kwanza nipokuwa na timu hii sikuwapo kwenye Simba Day, nilikwenda kuoa, mara ya pili nilikuwa nimeshaondoka kwa hiyo natarajia kufurahia sana siku hiyo kwa sababu itakuwa ni Simba Day yangu ya kwanza," alisema Miquissone kabla ya mechi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live