Ligi zimesimama na mchakamchaka wa michuano ya kimataifa unaendelea. Kwa Ligi Kuu England mambo ni matamu, huku Arsenal, Erling Haaland na timu tisa za mkiani kwenye msimamo zinapaswa kutuliza akili ili kujiweka sawa kwenye mambo 10 yanayopambaniwa kwenye mchakamchaka wa ligi hiyo kwa msimu huu wa 2022/23.
Kwenye Ligi Kuu England hadi ilipofikia kwa sasa, kuna vita 10 zinazoshindaniwa, ambazo bado hazijapata mshindi. Twende kazi.
10) KIATU CHA DHAHABU
Inavyoonekana kama Erling Haaland ameshamaliza mchezo kwenye vita ya kunasa Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu England, lakini ukweli kuna mtu anaitwa Harry Kane ambaye ni kawaida yake kupindua meza kwenye dakika za mwisho.
Haaland amefunga mabao 28, lakini Kane ana mabao 21 na kuna mechi 10 za kucheza, hivyo vita hiyo ya kusaka Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England msimu huu bado mbichi. Tofauti ya mabao saba si kubwa sana kwa mchezaji mwenye uwezo wa kutupia kama Kane ukingatia bado kuna mechi nyingi za kucheza. Haaland ajiangalie.
9) GLOVU ZA DHAHABU
Glovu za Dhahabu ni tuzo inayotolewa kwa kipa bora wa msimu. Ederson na Alisson wamekuwa wakipokezana tuzo hiyo kwa miaka mitano iliyopita na msimu huu kila mmoja ana mechi 10 alizocheza bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa, ikiwa ndicho kigezo kikubwa katika utoaji wa tuzo hiyo.
Msimu huu, makipa Nick Pope na Aaron Ramsdale wanaongoza, kwa kucheza mechi 12 bila ya nyavu zao kuguswa. David de Gea, alikuwa kipa wa mwisho aliyekuwa Ederson au Alisson kushinda tuzo hiyo na msimu huu ana mechi 11 alizocheza bila kuruhusu bao. Vita bado mbichi.
8) TUZO YA MCHEZESHAJI
Kwenye Ligi Kuu England tuzo ya Mchezeshaji Bora ilianza kutolewa msimu wa 2017/18, akikabidhiwa mchezaji aliyetengeneza pasi nyingi za mabao kwa timu yake. Tuzo hiyo ilianzishwa ili kuwapa wachezaji wanaopiga asisti nyingi nao kuthaminiwa kwa ubora wao wa uwanjani uliochangia mabao hayo, ambayo kwa wafungaji wamekuwa wakipewa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu.
Msimu huu vita ni kali, Kevin de Bruyne akiwa na asisti 12, Bukayo Saka 10, Leandro Trossard mwenye asisti nane na Christian Eriksen na Mo Salah wenye saba kila mmoja.
7) MCHEZAJI BORA WA MWAKA
Lugha nyepesi, tuzo ya mchezaji bora wa mwaka itakwenda kwa timu mbili zinazoshindania ubingwa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu. Haaland anapewa nafasi kubwa, huku nyuma yake kutakuwa na mastaa kibao kama Martin Odegaard, Saka, De Bruyne na Gabriel Martinelli wanaopewa nafasi kubwa kwenye kinyang’anyiro hicho, huku wachezaji kama Marcus Rashford, Harry Kane na Casemiro nao wakitajwa kuwa na nafasi kwenye mchakato.
Zaidi ya yote, kuna wachezaji 427 tofauti watakuwa na nafasi kubwa ya kuwania tuzo hiyo ya ubora wa mwaka.
6) KUFUZU LIGI YA MABINGWA ULAYA
Arsenal, Manchester City na Manchester United unaweza kuwaona kuwa wapo salama kwenye vita ya kusaka tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini vita hiyo inayohusisha timu nne za juu kwenye msimamo wa ligi bado mbichi.
Tottenham, Newcastle, Brighton na hata Liverpool nazo zina nafasi ya kukamatia tiketi hiyo kutokana na kutofautiana pointi chache kwenye msimamo na bado kuna mechi 10 na zaidi za kucheza kabla ya msimu kufika tamati. Kitu kizuri ni kwamba timu hizo zinazoshindania nafasi bado kuna mechi ya kumenyana zenyewe.
5) KUFUZU EUROPA LEAGUE
Timu zitakazoshindwa kwenye vita ya kusaka nafasi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, zitakuwa na fursa ya kucheza kwenye Europa League. Spurs wana nafasi kubwa ya kucheza Europa League msimu ujao, huku vita ya kucheza kwenye michuano hiyo ya ngazi ya pili kwa ukubwa huko Ulaya baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, inaweza kuzihusu pia, Newcastle na Brighton kama zitafeli katika vita kubwa.
Liverpool wamezoeleka kuonekana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini wakizubaa watajikuta kwenye michuano hiyo sambamba na vigogo wenzao Chelsea.
4) KUFUZU EUROPA CONFERENCE LEAGUE
Europa Conference League ni michuano ya tatu kwa ubora kwa Uefa na kwenya Ligi Kuu England kuna timu kibao zitachuana kuwania tiketi ya kucheza kwenye michuano hiyo.
Nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ndiyo inayotoa tiketi ya kucheza michuano hiyo na kwenye ligi msimu huu, Brentford, Fulham, Chelsea na Aston Villa zinaweza kuwa kwenye vita kali ya kusaka tiketi hiyo ya kucheza kwenye michuano ambayo ubingwa wake wa kwanza ulibebwa na Jose Mourinho akiwa na kikosi cha AS Roma ya Italia. Itakuwa aibu kwa Chelsea kama watacheza huko.
3) KOCHA BORA WA MSIMU
Tuzo ya Kocha Bora wa msimu mara nyingi imekuwa ikibebwa na kocha wa timu inayobeba ubingwa kwa msimu husika. Mara 12 kati ya 30 tuzo hiyo imebebwa na makocha ambao timu zao zilichukua ubingwa.
Jurgen Klopp alinyakua tuzo. Msimu huu, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amekuwa kwenye nafasi nzuri ya kunyakua tuzo hiyo kama ataendelea kuifanya Arsenal kuendelea kubaki kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo hadi mwisho wa msimu na kunyakua ubingwa. Pep Guardiola ni tishio kwake sambamba na Erik ten Hag wa Man United.
2) KUSHUKA DARAJA
Mechi za kimataifa zimekuja kupunguza presha kwenye vita ya kushuka daraja. Kuna timu nane zimetofautiana kwa pointi nne tu, huku kuna baadhi ya timu zimebakiza mechi 12 na nyingine 10 kwenye orodha ya timu hizo zinazopambana kugombea kubaki kwenye ligi.
Crystal Palace imempiga chini Patrick Vieira kwa hofu ya kushuka daraja, huku vita hiyo ikiwahusu makocha wengine kama David Moyes, Brendan Rodgers na Steve Cooper. Southampton inaburuza mkia, lakini bado wana uwezekano mkubwa wa kubaki kwenye ligi kama watashinda mechi zao zilizobaki.
1) VITA YA UBINGWA WA LIGI
Uwezekano wa Arsenal kushangilia kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu haupo mbali sana kukamilika. Uongozi wao wa pointi nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu England dhidi ya timu inayoshika nafasi ya pili, Manchester City na bado wamebakiza mechi 10. Man City wao wana mechi 11 za kucheza na kuna mchezo mmoja wa kuwakutanisha wenyewe kwa wenyewe.
Kwa maana hiyo, vita ya ubingwa wa ligi bado kali na si Arsenal wala Man City inayohitaji kuangusha pointi na timu itakayofanya hivyo, basi imekwisha. Hii hii ni tamu zaidi. Ngoja tuone.