Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo 10 yanayoifanya Yanga ya Gamondi kuwa tishio

Yanga 2023 24 Mambo 10 yanayoifanya Yanga ya Gamondi kuwa tishio

Wed, 30 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tangu msimu wa mwaka 2010/11 hakuna timu ambayo imewahi kucheza mechi mbili za awali za Ligi kufunga mabao 10 na kutoruhusu bao, iwe Simba, Yanga wenyewe, Lipuli, Singida au timu yoyote ile, lakini Yanga Sc ya Gamondi imeweza kufanya hivyo.

Yanga hii kwenye mechi mbili tu za Ligi imeonekana ni mwiba na tishio kwa msimu huu endapo wataendeleza moto huu waliouanza.

Haya ni mambo 10 ambayo Yanga ya Gamondi ni tishio;

1. Mfumo wa kiuchchezaji

Kocha Gamondi ni muumini wa mfumo wa 4-2-3-1 kwa maana ya mabeki wanne, viungo wawili wa ukabaji, viungo watatu wa ushambuliaji na mshambuliaji kinara mmoja. Mfumo huu ndiyo ulikuwa ukitumiwa na Kocha Nasreddine nabi tangu atue Yanga mwaka 2020, ni mara chache sana alibadilisha.

Gamondi anapita na mfumo huo huo ambao wachezaji wengi anaowatumia kikosini wameshauzoea huo mfumo wakiwa yanga tangu misimu ya Nabi. Lakini hata wageni waliosajiliwa msimu huu kama Yao na Pacome, kocha wao wa ASEC Mimosas alikuwa akitumia mfumo huo mpaka wakafika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho. Nzengeli ambaye ametoka Maniema kocha wao alikuwa akitumia mfumo huo.

Ujenzi wa mashambulizi unaanzia kwa kipa na mabeki wake, kisha viungo wa kati wanakuja kupokea. Mabeki wa pembeni wanaongezeka wanakuwa kama mawinga na mawinga wenyewe wanaingia ndani kuwa kama supportive strikers na inakuwa rahisi kumuadhibu mpinzani kwa sababu wanakuwa wengi kwenye box lake.

2. Pasi na kasi

Yanga wanahakikisha kila mchezaji anayeupata mpira usimtoke akaupoteza, lazima aufikishe kwa mwenzake bila kuupoteza. Yeyote anayepangwa anajua mpira ni mali ambayo haitakiwi kupotea miguuni mwao na wakifika eneo la mpinzani kasi yao ya kushambulia inaongezeka mara mbili.

Gamondi amesema hili kwenye kitabu chake cha ‘My Story My Life’ ambamo ameeleza falsafa yake ya direct football, anataka kasi na mpira wa kwenda mbele na si nyuma wala pembeni. Sasa utaona wachezaji wake wameanza kuzimeza falsafa zake.

3. Umiliki wa mpira na pressing

Yanga wanaamini kama mpira ni miliki yao, kwa hiyo hata ikitokea wakapoteza mpira, wanamzunguka wengi kwa mpinzani kuutaka mpira urejee kwenye miliki yao, wanafanya pressing ya nguvu ndani ya sekunde 4 mpaka 6 kuhakikisha wanauchukua na ikishindana wanarudi haraka kwenye eneo lao kwa ajili ya kukaba.

Hivyo wanamfanya mpinzani akose utulivu hata kama hawataupata basi kwa kumzonga mpinzani atalazimika kufanya maamuzi ya papara na kutoa nje au kubutua na mwisho wa siku wananauchukua.

4. Ubora na uwezo wa wachezaji

Kikosi cha Yanga kimejaa wachezaji wenye ubora mkubwa, uzoefu katika mashindano mbalimbali. Ukiwaangalia akina Aucho, Pacome, Aziz Ki, Diarra, Maxi, Pacome, Gift na wengine hawana presha na mechi kubwa wala ndogo, wameshaonyesha uwezo wao kutoka huko walipokuwa.

Ni wachezaji ambao ni rahisi kumeza mbinu za mwalimu, wakaongeza ujuzi na maarifa yao kisha wakaibeba mechi na kuamua matokeo katika nyakati nzuri na nyakati ngumu.

Kocha Gamondi amewaruhusu wachezaji wake kuonyesha vipaji vyao walichojaliwa na Mungu wakiwa na mpira, sio kocha anayetaka ufanye vilevile anavyokuagiza, mchezaji anaweza kufanya vitu vya ziada na utundu wake pengine kupiga chenga, tobo na vingine lakini mpira usipotee.

Mchezaji anaweza kuwa karibu na mwenzake akaacha kumpigia pasi akapiga chenga kisha ndio akatoa pasi, hii inawafanya wapinzani kushindwa kuitabiri timu na kushindwa kuelewa kwamba huyu mchezaji atatoa pasi au atapiga chenga.

5. Utimamu wa mwili na akili (Physical and mental fitness)

Hili linawafanya uwaone dakika ya kwanza ni kama dakika ya 90, uvujashi jasho, utashi, kupambana ili kuupata mpira. Yanga ni wagumu sana kuchoka, wanakimbia sana, wana nishati kubwa kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya mwisho, hiki kinawapa shida wapinzani wao shida kubwa.

Hiyo kimbia yao na nishati yao inakuwa ni mateso kwa mpinzani wao hasa kuanzia eneo la kati kwenda langoni mwa mpinzani hivyo wanamnyima mpinzani utulivu na mwishowe kuwalazimu kufanya makosa mengi.

Yanga hawakwenda pre-season nje ya nchi, walichagua kubaki Avic Town Kigamboni ambako kuna kila kitu kuhusu mazoezi, na haya ndiyo matokeo ya walichokichagua Wananchi.

6. Subira

Yanga wana subira kwenye mechi, hawana haraka ya kufunga kama mpinzani ameweka ukuta mgumu, wanapasiana sana lakini kama mpinzani anazuia, wataendelea hivyo hivyo, watakuja, watakuja tena, zaidi na zaidi mpaka mpinzani anachoka na kupitika kirahisi ama kufanya makosa kirahisi na Yanga wanafufaika.

Subira ni siri ya mafanikio ya Yanga katika hizi mechi chache alizocheza.

7. Kuhamisha mipira (switching)

Yanga wanapomiliki mpira kwenye eneo moja la uwanja wanaweza kukushangaza, unakaba huku wao wakauhamisha umbali mrefu kwenda upoande mwingine.

Yanga wana watu wanaoweza kufanya hiyo kazi ya kuhamisha mipira kwa usahihi, Mkude, Sure Boy, Job, Mwamnyeto, Nzengeli, Aziz Ki na Djui Diarra hii inawasaidia sana Yanga kupata matokeo kwa sababu mpira unapohamishwa eneo hilo linakuwa na idadi ndogo ya wapinzani hivyo ni rahisi kwao kufanya madhara kwa mpinzani kwa kanuni ya numerical advantage.

8. Yeyote anafunga

Yanga hawamtegemei sana mshambuliaji kinara, mabao yanafungwa na kila mchezaji mpaka Yao na Dickson Job ambao ni mabeki wanafunga. Mpinzani anapojipanga kumdhibiti mshambuliaji kinara, mabao yanapita kushoto, kulia na maeneo mengine ya uwanja tofauti na msimu uliopita walikuwa wakimtegemea Fiston Mayele na Aziz Ki. Katika mabao 10 ya Ligi kwenye mechi mbili za Yanga hakuna mshambuliaji kinara aliyefunga bao zaidi ya Konkoni ambaye ana bao moja tu.

9. Kikosi kipana

Yanga katika mechi hizi mbili wamethibitisha kuwa wana kikosi kipana, hawana wachezaji wengi. Unaweza kuwa na rundo la wachezaji wenye majina makubwa lakini kikosi kikawa chembamba.

Kocha Gamondi ameonesha ana kikosi kipana na amekuwa na jeuri ya kuonyesha hilo kwa kufanya rotation kubwa kila mechi mpaka golikipa Diarra anaacha kumpanga anampa nafasi Metacha Mnata na wote wamepata clean sheet.

Kikosi cha gamondi huwezi kukiotea, anweza kumweka benchi Mwamnyeto, Aucho, Sureboy, Mudathir, pacome kifupi ni mchezaji yoyote anaanza na yoyote anawekwa benchi nab ado timu yake inapata matokeo na kucheza soka lenye quality ile ile. Mchezaji anayeingia anakuwa hatofautiani na mchezaji aliyeanza.

10: Benchi la ufundi, uongozi

Yanga wana benchi bora sana la ufundi kuanzia kwa Kocha gamondi, Msaidizi wake Mussa N’daw, makocha wa viungo na makipa, madaktari na maofisa wote wa timu wanafanya kazi kubwa sana kuhakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yake ipasavyo. Yanga ni kama wame-copy na ku-paste alichokuwa akikifanya Nabi lakini safari hii wameongeza vitu vizuri zaidi.

Gamondi ni mwalimu mzoefu hilo halina shaka, ni mbobezi na ana mbinu nyingi za kisoka ambazo matunda yake wameanza kuyafaidi Wananchi mapema tu hata mechi tano hazijafika. Anao uwezo wa kumsoma mpinzani kabla ya mchezo na wakati wa mchezo kisha akafanya mabadiliko au maelekezo ya kimbinu ambayo yanakwenda kuzaa matokeo chanya.

Uongozi wa Yanga chini ya raia wao Eng. Hersi Said, makamu Arafati Haji pamona na viongozi wengine wapo makini mno kuhakikisha wanafuatilia kila kinachoendelea kwenye timu yao.

Usajili walioufanya Yanga haukuwa wa kuziba mapengo bali mahitaji ya kikosi chao. Tazama hamasa wanazozifanya na utekelezaji wa mipango madhubuti kwa ajili ya kuifanya timu yao iwe bora, wanashirikiana vizuri na benchi la ufundi, wachezaji pamoja na mashabiki, kwa nini Yanga isipate matokeo?

Kumbuka Yanga ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC na wana lengo la kuendelea kuchukua ubingwa huo tena.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: